Wapinga mkutano mkuu wa dayosis hadi mgogoro utakapomalizika

Na, Florence Sanawa
Sauti ya Mnyonge, Mtwara

WAZEE wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Usharika wa Mtwara wamepinga kufanyika kwa Mkutano Mkuu wa Sinodi (Dayosisi) kabla ya kumaliza mgogoro  uliopo katika kanisa hilo dhidi ya askofu wa jimbo hilo Lucas Judah Mbedule uliodumu kwa zaidi ya miaka miwili sasa.

Kanisa hilo liliingia katika mgogoro baada ya kumtilia mashaka na kumtuhumu Askofu huyo kuwa na matumizi mabaya ya fedha  na kujimilikisha mali na viwanja vya kanisa hilo kinyume na taratibu za kanisa.

Akitoa tamko hilo wakati wa ibada leo mmoja wa waumini wa kanisa hilo aliyeteuliwa na wazee Steven Macha alisema kuwa  takribani miaka miwili sasa kanisa hilo limekuwa na  mvutano kati ya washirika hao wanaohitaji kuondolewa kwa Askofu huyo.

Alisema kuwa askofu huyo amekuwa akitenda mambo yasiyozingatia mafundisho ya kikristo kwa kwenda kinyume na madhabahu na kusababisha kuvurugwa kwa utaratibu wa heshima ya cathedral na kanisa kwa ujumla.

Macha alisema kuwa mkutano huo wa Sinodi uliopangwa kufanyika mwezi Mei 17-18 mwaka huu umewaalika maaskofu saba (7) akiwemo askofu mkuu wa kanisa hilo Askofu Dk Fredrick Shoo bila wazee wa kanisa hilo kushirikishwa hali ambayo imepelekea kuwepo kwa maamuzi ya kupinga mkutano huo.

Aidha wazee hao wamesema kuwa mbali na kiti cha uaskofu kurejeshwa pia kumekuwa na mambo yanayofanyika katika kanisa yenye sura ya kishirikina na kuwataka waumini wavae mavazi meusi na kuzuia ibada kufanyika za nyumba kwa nyumba wala mikusanyiko yoyote ya maombi katika wiki hiyo.

“Tumeona kuwa ipo michango inayoendelea kutolewa kwaajili ya kuuwezesha mkutano huo mkuu wa sinodi unatarajiwa kufanyika ndani ya usharika wetu tunaisitisha kwakuwa haijafata utaratibu wa kanisa letu endapo yakiendelea haya hatutasita kujitenga na Dayosisi  hii ya Kusini Mashariki…..

 “Tunafahamu zipo tetesi kuwa taaratibu zinazofanywa za kumteua Askofu wa Usharika wa Lindi kuja hapa ndiyo maana baadhi ya watu ambao waliacha kufika kwenye ibada wameanza kurudi bila hata ya kutubu kuna hoja za msingi za wakristo ambazo hazijajibiwa kuhusu fedha na viwanja” alisema Macha

Kwa upande wake Mwinjilisti wa Kanisa hilo Geofrey Mposola alisema maamuzi ya kanisa lazima ashirikishwe jambo ambalo limesemwa na wazee halitambui wala hakushirikishwa katika maamuzi hayo.

“Tumeshapeleka barua nyingi kwa Askofu mkuu tumsubiri yeye aje kuamua tuzungumze naye kwa upendo kwamba hapa kanisani kuna tatizo hili hivi kulukuwa na haja gani ya kuja kutangaza mambo haya hapa madhabahuni wakati tulishampelekea Askofu Mkuu barua zetu….

“Mimi hapa ni kama nipo hapa kama mbuzi wa kafara wakati mwingine  huwa ninajuta hata kwa nini Mungu alinileta hapa lakini ninajua kuwa lipo kusudi la Mungu kuwa hapa maazimio yaliyotolewa hapa mimi sijashirikishwa na sijayaandaa kabisa  kanisa litambue hilo tusifanye mambo kwa visasi…….

“Maamuzi yanapotolewa kanisani mimi kama mwinjilisti napaswa kushirikishwa lakini nilisafiri kama wiki tatu zilizopita niliporudi nakuta maazimio haya  nawaambia hatutaweza kupata malaika ambaye aataliongoza kanisa hili  bila kukosea lazima tujiongoze wenyewe lakini” alisema Mposola

Comments

Popular posts from this blog

Wananchi wajenga wodi baada ya kuchoshwa na kujifungulia sakafuni

Sita wapotea katika mazingira tatanishi wilayani Wete

Jaji Mkuu Zanzibar awashukia mahakimu wanaonyanyasa watuhumiwa