Jaji Mkuu Zanzibar awashukia mahakimu wanaonyanyasa watuhumiwa


Na, Haji Nassor,
Sauti ya Mnyonge, Zanzibar

JAJI mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu, amewauliza mahakimu kisiwani Pemba, wamezitoa wapi sheria zinazowapa mamlaka ya kuwalazimisha watuhumiwa, kuwa na wafanyakazi wa serikali au barua za masheha kama kigezo  wanapoomba dhamana dhidi ya kesi zinazowakabili.

Alisema anashangaa kuona baadhi ya mahakimu, kuwawekea masharti magumu watuhumiwa, kwa lengo la kutafuta sababu ya kuwapelekea rumande, jambo ambalo sio sahihi maana huko sio kwahali kwema kwa kukaa mwanadamu.

Jaji Mkuu huyo alieleza hayo, kwa nyakati tofauti, walipokuwa akizungumza na watendaji wa mahakama za mwanzo Wingwi, Konde na Wete, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku nne kisiwani Pemba.

Alisema lazima mahakimu waelewa kuwa, kumpeleka mtuhumiwa rumande ni hatua ya mwisho, na sio iwe ndio kipaumbele chao, kwa kuwekea masharti magumu au kima kikubwa cha fedha taslimu.

Alieleza kuwa, yeye binafsi hajaona popote kwenye sheria, kuwa mtuhumiwa anatakiwa ili kutimiza masharti, kwamba awe na mtu anaefanyakazi serikalini, au barua ya sheha kwamba ndio kigezo, na mtuhumiwa akishindwa na hayo, apelekwe rumade.

“Jamani wale ni binadamu, wapo waliotenda makosa, wapo walioteleza na wengine wamezuliwa sasa na nyinyi mkishawishika kwa kuwapeleka rumade tena kwa masharti magumu, mtakuwa hamkuwatendea haki tumieni elimu yenu,’’alieleza.

Katika hatua nyengine Jaji Mkuu huyo wa Zanzibar alisema, mahakimu lazima wafanye kazi kisayansi na sio kufanya kazi kwa mashindikizo ya wanasiasa, maana wakifanya hivyo watakuwa hawaitendei haki fani yao.

“Lazima muelewa mahakimu wetu kwamba, kuna kupanda daraja kwa mujibu wa kazi zenu, lakini kama mnafanyakazi kwa chuki, mashindikizo basi msitarajie kupanda ngazi,”alieleza.

Nae Mrajis wa Mahakama kuu Zanzibar Mohamed Ali Mohamed, alisema sasa watakuwa na makini na mahakimu watoro na wanaopenda kusafiri bila ya dharura maalum.

“Wapo mahakimu unawaona Unguja mara kwa mara bila ya safari maalum za kikazi, na huku wameziacha kesi juu ya meza na kuwatia watu tabu, sasa hawa tutapambana nao,”alieleza.

Nae Mrajisi wa jimbo mahakama kuu Pemba Hussein Makame Hussein, alisema changamoto kadhaa wamezisikia hawa walipowatembelea wanafunzi, juu ya kucheleweshea mienendo ya kesi, jambo kwa sasa wanajitahidi.

Ziara ya Jaji Mkuu Zanzibar akiwa na Mrajisi na Manaibu Warajisi, itaendelea tena kesho kwa kulikagua jengo la Mahakama Kuu Chakechake kabla ya kuzungumza na watendaji wake, na kukamilisha ziara yake ya siku nne kisiwani Pemba.

Comments

Popular posts from this blog

Wananchi wajenga wodi baada ya kuchoshwa na kujifungulia sakafuni

Sita wapotea katika mazingira tatanishi wilayani Wete