Mrajisi ataka wananchi kufika mahakamani kutoa ushahidi
Imeandaliwa na Haji Nassor
Sauti ya Mnyonge, Pemba
Mrajisi wa Mahakama jimbo la Pemba, Hessein Makame Hussein
JAMII imetakiwa kujipinda na kuacha kazi zao zote, na kufika mahakamani kutoa ushahidi, ikiwa ni njia moja wapo ya kutomeza vitendo vya udhalilishaji viliovyoonekana kushamiri katika siku za hivi karibuni.
Hayao yameelezwa na Mrajisi wa mahakama jimbo Pemba Hessein Makame Hussein, alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi juu ya athari wanayoipata kwenye mahakama kwa jamii kutopenda kutoa ushahidi mahakamani.
Alisema, utamaduni wa kukimbia Mahakamani na kuacha kutoa ushahidi, unadhoofisha kwa asilimia kubwa, mikakati ya kuwaadabisha wanaofanya vitendo vya udhalilishaji.
Alieleza kuwa, kama jamii haikuungana pamoja hasa kwa kufika mahakamani kutoa ushahidi, kusitarajiwe kutiwa hatiani kwa mkosaji yeyote wa matendo ya udhalilishaji.
Mrajisi huyo alieleza kuwa, suala la kupiga vita vitendo hivyo vya udhalilishaji, haliuhusu mahakama pakee, bali kila mmoja anaweza kushiriki na ikawa sehemu ya kutokomeza vitendo hivyo.
“Jamii ikiacha kufika mahakamani kutoa ushahidi, lakini wao ikiwa wanapiga kelele washitakiwa hawatii hatiani, basi ni kutokana na wao kutofika mahakamani”,alifafanua.
Nae Mwanasheria dhamana Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka, Ali Rajab Ali, alisema waendesha Mashitaka na wanasheria wengine mahakamani, wote ni wageni wa matukio, hivyo wa kuwathibitisha ni mashahidi.
Nae Sheha wa shehia ya Shamiani Mwambe Safia Khami Ngwali, alisema inawezekana jamii imekuwa na ulege ulege kufika mahakamani kutoa ushahidi, kutokana kesi hizo kuchukua muda mrefu.
“Kesi hizi huchukua hata mwaka mmoja, sasa mashahidi hukata tama na mapema, na kisha kufika mahakamani kutoa ushahidi, bila ya kujali athari zake”,alieleza.
Katibu wa baraza la vijana shehia ya Chambani Zuwena Salum Nassor, alisema bado elimu zaidi inahitajika kwa jamii ili kuelewa umuhimu wa kutoa ushahidi mahakamani.
Nae Mratibu wa wanawake na watoto shehia ya Kangagani Awena Salum Kombo, alisema ni vyema sasa kukaandaliwa sheria maalum ya wale wanaokataa kutoa ushahidi ikawaadhibu.
“Mtu atakujia kifua moto kwamba mwanawe kabakwa, lakini kesi ikishafika mahakamani, huwa ajitia sababu na haendi tena kutoa ushahidi hatimae kesi inafutwa”,alifafanua.
Mzazi wa mtoto ambae mwanawe alibakwa wa Mchanga mdogo, alisema jamii kama haikuungana katika kutokomeza matendo ya udhalilishaji wa kijinsia, kusitarajiwe mabadiliko yoyote.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa kaskazini Pemba, Haji Khamis Haji alisema wanazo kumbu kumbu za kesi 25 za udhalilishaji zilizofutwa, ambazo 21 zilifutwa kituo cha Polisi Wete na kesi nne (4) zimeondolewa mahakamani, kutokana na kukosena kwa ushahidi, kuanzia mwaka 2015 hadi Oktoba mwaka huu.
Nae Afisa Ustawi wa Jamii wilaya ya Wete Haroub Suleiman Hemed alieleza kuwa, kesi 11 za udhalilishaji zilifungwa na kufutwa kuanzia mwaka 2015 hadi oktba mwaka huu, kutokana na wanajamii kukimbia kutoa ushahidi.
Comments
Post a Comment