Walengwa 175 wa TASAF wawanufaisha wakulima wa mpunga 230
Na, Haji Nassor
Sauti ya Mnyonge, Pemba
WALENGWA 175 waliomo kwenye mpango wa kunusuru kaya maskini unaoendeshwa na TASF III, shehia ya Kendwa wilaya ya Mkoani Pemba, wanatarajiwa kuwanufaisha wakulima wa mpunga 230 wa bode la Egeyani, kuwa na kilimo cha uhakika kuanzia msimu ujao.
Walengwa hao wapo kwenye bonde hilo kwa sasa wakiendelea na kazi ya kuchimba misingi ya kisasa, ambayo italiwezesha bonde hilo kuondokana na mfumo wa ziwa ambapo uwingi wa maji uliokuwepo kwa muda mrefu haukuwa ukiwanufaisha wakulima hao.
Mwandishi wa habari hizi, alishushuhudia kazi ya kuchimba misingi kwenye bonde hilo zikiendelea kwa kasi, ambapo miundombinu inayowekwa kwenye bonde hilo, sasa itakinga uwepo wa maji ya bahari.
Baadhi ya watendaji kazi kwenye bonde hilo, walisema eneo hilo limekuwa haliwapi mfumo mzuri wakulima kutokana na kujaa maji na kufanyika ziwa, lenye kina kirefu na wakati mwengine hata kuingia maji ya bahari.
Walisema kazi wanayoifanya wao kupitia mpango wa kunusuri kaya maskini, itawanufaisha na wakulima wengine 230, ambapo baada ya kazi hiyo, watakata ploti zaidi ya 100 ambazo zitawaruhusu wakulima hao kulima kwa utulivu.
Walieleza kuwa, bonde hilo kwa muda mrefu wakulima wake, hawakuwa na uhakika nzuri wa kuendesha kilimo hicho, kutokana na kukabiliwa na uwingi wa maji ya mvua na wakati mwengine hata ya bahari.
Msimamizi mkuu wa wanakaya hao waliomo kwenye mpango wa kunusuru kaya maskini shehiani humo, Salim Mbarouk Salim alisema kazi inayoendelea hapo ni kuchimba misingi ambapo lengo ni kuona maji ya mvua na yale ya chumvi yanakuwa na njia moja.
“Ilikuwa hapa wakulima wanalima lakini wakisalimika na maji ya mvua kuwa mengi, basi mpunga wao utakufa kutokana na maji ya bahari, maana hapa pana mto unaoruhusu maji ya baharini kupenya ,”alieleza.
Alisema kazi hiyo inatarajiwa kukamilika siku chache zijazo, matunda yake hayatonufaisha tu wale walengwa waliomo kwenye mpango, bali hata na wengine.
Hivyo amewataka wakulima wa eneo hilo, mara mpango utakapokamilika, kutumia jitihahada zao ili kuhakikisha miundombinu hiyo inaendelea kuwanufaisha hapo baadae.
Baadhi ya wakulima wa bonde hilo walisema mpango huo uliobuliwa na walengwa hao, unafaa kuenziwa na kulindwa maana matunda yake ni ya kudumu.
Ali Haji Makame alisema, kilichobakia kwa sasa ni kuufufua ule umoja wa wakulima wa bonde hilo, lili kijipangia mikakati ya kuendeleza bonde hilo.
Nae Asha Salim Hussein na Time Haji Mohamed, walisema sasa wanatarajia kuongeza pato lao kupitia kilimo cha mpunga, maana watakuwa na uhakika wa kilimo hicho.
“Ilikuw asisi tukishasia basi tutavamiwa na maji ya mvua, maana hapa pana ziwa, au maji ya chumvi yataingia na kutuharibia mpunga wetu, lakini sasa twashukuru,”alieleza.
Mratibu wa TASAF Pemba Mussa Said Kisenge, alisema malengo hasa ya miradi ya aina hiyo, inayoibuliwa na wananchi waliomo kwenye mpango wa kunusuru kaya maskini, ni kuwa na maendeleo endelevu.
Mradi huo wa upigaji misingi kwa ajili ya kuweka miundombinu bora ya upitishaji maji ya mvua na chumvi ili kuwapa uhakika wa kilimo wakulima, ni aina ya pekee kisiwani Pemba, unaofadhiliwa na TASAF.
Comments
Post a Comment