Wakulima wataka ripoti ya soko la kimataifa wakapambane nalo huko huko

Na, Zuhura Juma
Sauti ya Mnyonge, Pemba

WAKULIMA wa mwani shehia ya Kiungoni Wilaya ya Wete Pemba, wameiomba Serikali kufanya utafiti wa kina juu ya Soko la kuuzia mwani Kimataifa, ili wajue jimsi ya kupambana nalo na kuweza kujipatia kipato cha kuridhisha kitakachowasaidia kuwakwamua na umaskini.

Walisema   wamekuwa wakilima kilimo hicho kwa muda mrefu sasa, ingawa bado Soko limekuwa ni kikwazo kikubwa kwao, kutokana na bei ndogo wanayouzia, ambayo huzorotesha shughuli zao za kilimo cha Mwani.

 Walieleza   iwapo Serikali itafanya utafiti wa kina kuhusu soko la kuuzia mwani Kimataifa na kujua kitu kinacholifanya soko hilo kuwa la kiwango cha  chini, ili kusaidia wakulima hao kujua kiwango kinachohitajika na kuweza kupambana na soko hilo na kujipatia kipato cha kuridhisha. 

“Tunataka tujue je ni kweli mwani una bei ndogo kimataifa au ni wanunuaji wa hapa kwetu tu wanatukomoa?, hivyo Serikali itakapofanya utafiti tutajua sababu ya bei kuwa ndogo”, walisema wakulima hao.

Mmoja wa wakulima hao, Chumu Ali Hamad, alisema ni vyema kwa Serikali kusimamia kwa kulifanyia uchunguzi jambo hilo, ili kuwarahisishia wakulima kujua kiwango kinachotakiwa na kujua bei ilioko katika Soko la  Kimataifa, jambo ambalo litaweza kuwasaidia kujikwamua na umasikini, ikiwa ndio lengo lao kubwa la kulima kilimo cha mwani.

“Tumeamua kulima kilimo hiki ili tujikwamue na maisha duni yanayotukabili, lakini bado bei ya mwani inatuumiza vichwa, kwani kazi kubwa na kipato kidogo”, alisema Chumu.

Alieleza   wamekuwa wakisikia tetesi za watu kuwa mwani una soko kubwa kimataifa, ingawa wao wanaofanya kazi kubwa ya kulima, ndio wanaoishia kuuza kilo moja ya mwani kwa shilingi 500/=, jambo ambalo linawasikitisha sana.

“Kwa huku kwetu familia moja haipungui watu saba, na shughuli yetu kubwa ni kulima mwani, kwa kweli bei hii inatuumiza sana, lakini hatuna la kufanya tu”, alisema Mkulima huyo.

Kwa upande wake, Fatma Salum Hamad, alieleza   wanahitaji vihori, kamba, na viatu vitakavyowasaidia kurahisisha shughuli zao za kilimo cha mwani.

“Pamoja na changamoto hizo ,lakini bado tunajituma kwa kilimo hicho, kwani hatuna njia nyengine ya kufanya, tunaiomba Serikali itusaidie kwani wananchi wake tunateketea”, alieleza. 

Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi Pemba, Sharif Mohamed Faki,  alisema   jambo linalosababisha soko kuwa ni la kiwango cha chini Duniani ni kutokana na kuwepo Kampuni mbili tu za kununulia Mwani, jambo ambalo linakosa ushindani kwani wanapanga wenyewe bei wanayoitaka.

“Kwa kweli bei ya Soko la dunia ni ya kiwango cha chini, ambapo makampuni hupanga bei wenyewe, hali iliyopelekea wakulima kulalamikia Soko kila siku, naamini kungekuwa na masoko mengi basi bei ingekuwa kubwa”, alisema Mkuu huyo.

Alieleza   pia ukosefu wa Ofisi maalumu ya kununulia Mwani inasababisha kuwepo kwa bei ndogo, kutokana  na gharama za usafirishaji kuwa ni kubwa kwa wanunuzi wa mwani.

Nae, Meneja wa Kampuni ya   kununulia Mwani  Tawi la Pemba, ‘ZANQUE AQUE FARMS’, Issa Khamis Mohamed, alisema    wanalazimika kununua mwani kwa bei ndogo kulingana na soko la Dunia kuwa wanapanga bei wenyewe kwa kuangalia zaidi gharama zao.

“Kwa kweli kipato ni kidogo kwa wakulima na hata sisi wanunuzi, kwani sasa hivi kilo ya mwani ni shilingi 500/=, jambo ambalo linazorotesha maendeleo ya kilimo hicho”, alisema Meneja huyo.

Hata hivyo ,Meneja huyo  aliwataka wakulima wa mwani kutovunjika moyo na badala yake waendelee kulima kilimo hicho kwa wingi, ili kupata kipato cha kutosha, kwani licha ya bei ndogo lakini iwapo watalima kwa wingi watajiongezea fedha zitakazowasaidia kujikwamua kimaisha.

Comments

Popular posts from this blog

Wananchi wajenga wodi baada ya kuchoshwa na kujifungulia sakafuni

Sita wapotea katika mazingira tatanishi wilayani Wete

Jaji Mkuu Zanzibar awashukia mahakimu wanaonyanyasa watuhumiwa