Utukufu wa viongozi wa dini unavyotiwa dosari na wachache wao
Na Zuhura Juma
Sauti ya Mnyonge, Pemba
VIONGOZI wa dini ni watu watukufu katika jamii, ambao husikilizwa na waumini wao kwa kila wanachokisema na hufuatwa kwa kila wanachokiongoza.
Miaka ya hivi karibuni, hali hiyo imekuwa ni tofauti kutokana na wachache wao kujihusisha na vitendo vya udhalilishaji kwa wanawake na watoto.
Mwandishi wa makala haya alianza safari yake hadi kufika shehia ya Shengejuu Wilaya ya Wete, ambapo alikutana na sheikh Khamis Hamad Nassor alimuelezea kuwa, viongozi wa dini wamekuwa nyuma katika kupinga vitendo vya udhalilishaji katika jamii, kutokana na baadhi yao kujinasibisha kufanya vitendo hivyo.
Yeye anaona kuwa, ukemeaji wao ni mdogo ukilinganisha kuwa, hilo ni jukumu lao la kila siku la kuamrishana mema na kukatazana mabaya.
“Masheikh na maimamu sisi ndio wasimamizi wakubwa kwa waumini wa kiislamu na ndio tunaosikilizwa na jamii, ingawa baadhi yaetu tumekuwa ni wahusika wa kutekeleza vitendo vya udhalilishaji katika jamii, kutokana kuwa mbele wakati wa suluhu”, alieleza.
Wapo baadhi ya masheikh, wakihutubia misikitini hawaelezi matukio yaliyopo ndani ya jamii, ambayo hutendeka kila siku, bali wanaelezea zaidi historia zilizopita.
“Sasa masheikh tujitahidi kuzungumzia kila siku suala ya ukatili kwa wanawake na watoto, ili kuweza kuipa jamii taarifa kwamba jambo hilo ni kosa, pengine huenda wakaogopa’’, alisisitiza.
Mwalimu wa madrasa shehia ya Mjini Ole Rashid Khamis Bakar anasema, wao ni wachunga na kila mmoja, ataulizwa alichokichunga, hivyo wawe mstari wa mbele kukataza matendo maovu kila wakati.
‘’Hivi sasa kuna wimbi kubwa la walimu wa madrasa wanaotuhumiwa kuwafanyia watoto udhalilishaji, kwa kweli hii inasikitisha sana, kwani wao ndio walezi wakubwa wa watoto, sijui hali hii ikiendelea jamii itakuaje hapo baadae’’, alihoji.
Juma Salim Suleiman mkaazi wa shehia ya Kangagani anasema, licha ya kuwa masheikh hukemea matendo hayo katika hotuba zao, hasa Ijumaa, lakini bado wako nyuma baadhi ya sehemu katika kupinga vitendo hivyo.
‘’Kuna baadhi ya sehemu ushiriki wa masheikh katika kupiga vita ukatili kwa watoto na wanawake, bado ni mdogo maana likitokea tatizo wao ndio wanaokwenda kwa familia husika na kutaka suluhu, hii inasikitisha sana’’, alieleza Juma.
Omar Khamis Othman yeye ni sheha wa shehia ya Kiungoni alihadithia kutokea tukio la mtoto wa miaka 16 katika shehia yake, ambapo alikwenda kisiwa jirani kwenda kuozeshwa mtoto huyo.
“Tunajua kuwa anaeozesha mke ni sheikh, kwa kweli wao wanashiriki kiasi fulani, katika kuongeza vitendo hivyo, iweje mtoto aozeshwe huku akiwa na ujauzito,” alisikitika sheha huyo.
Hanasa Ali Omar mkaazi wa shehia ya Kiungoni anasema, masheikh na maimamu wanajitahidi kukemea vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto, ingawa hofu yake imetanda kwa walimu wa madrasa, kwani baadhi yao wamekuwa wakiwafanyia watoto udhalilishaji.
‘’Kwa kweli inatusikitisha sana maana juzi tu, mtoto wangu alipigwa bakora nyingi sana pamoja na kuchomwa moto na mwalimu wake wa madrasa, jambo ambalo limesababisha kila nikimtazama mwanangu nabubujikwa na machozi’’, alisikitika mama huyo.
Mtoto wake wa miaka sita Nurdin Massoud Hamad, baada ya kupigwa bakora, alifungiwa chuoni na mwalimu huyo na kumuunguza moto mikono yake kwa sababu ya utoro.
‘’Walimu wa madrasa hasa hawa wasaidizi maana huwa ni vijana, wamekuwa wakiwadhalilisha watoto wetu sana, walimu wakuu wajitahidi kutusomeshea wenetu wasiwaachie vijana kuwafanyia ukatili’’, alisema mama huyo.
Mtoto Nurdin Massoud alieunguzwa moto na mwalimu wake wa madrasa Abdalla Gharib Hamad (19), anaelezea kwa masikitiko kuwa alimpiga bakora 20 na kuwasha kibiriti na kumchoma mikono yake huku akimuwekea vidifu, hali ambayo imemsababishia kufanya vidonda.
Sheha wa shehia hiyo, suala la kupigwa na kuchomwa moto kwa mwanafunzi huyo kuwa ni la kweli na kusema hakumtendea haki, kwani adhabu aliyompa hakupaswa kunfanyia mtoto huyo.
‘’Kwa kweli hawa walimu wasaidizi wa madrasa wamekuwa wakiwafanyia watoto wetu ukatili na unyama kabisa, mtoto mdogo unamchoma moto au unamlawiti au kumbaka, unatarajia nini kutoka kwa Muumba wako?’’, alihoji sheha huyo.
Kwa huzuni na masikitiko makubwa, baba mzazi wa mtoto wa miaka tisa aliyedaiwa kulawitiwa na msaidizi mwalimu wa madrasa (18) katika shehia ya Kiungoni, alieleza janga hilo, lilimkuta mwanawe wakati akiwa mtoni anaogelea na ndipo alipomtoa na kumpeleka kichakani.
“Nilivyoambiwa hospitali hajawahi kumlawiti na mtoto mwenyewe pia aliniambia kuwa hakuwahi, kwani walitokea watoto wenzake lakini kama si hivyo, angelimuumiza”, alihadithia.
Baba huyo anasema, masuala hayo iwapo yatafumbiwa macho hayatoweza kuondoka ndani ya jamii, kwani watendaji wanaona ni hali ya kawaida.
Khadija Henoick Maziku, ambae ni Mratibu wa wanawake na watoto shehia ya Mjini Ole, alisifu kuwa viongozi wa dini wanatoa mchango mkubwa katika kuhakikisha vitendo vya udhalilishaji vinaondoka baadhi yao hawajui nini ukatili wa kijinsia.
‘’Ili tuweze kuondosha vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto, ni vyema jamii yote ishirikiane, kwani jukumu hili sio la mtu mmoja pekee bali ni la jamii nzima’’, alishauri.
Katika shehia yake Mratibu huyo alipokea kesi tatu za ushalilishaji kwa wanawake na watoto kuanzia mwaka 2015 hadi Oktoba mwaka jana, ambapo zote ziko kituo cha Polisi Mchangamdogo.
Mratibu wa wanawake na watoto shehia ya Kinyikani Mauwa Said Khamis, shehia yake viongozi wa dini wanatoa elimu kwa akina baba na kuwahamasisha waelimishe familia zao.
‘’Waume zetu wanapotoka msikitini siku nyingi wanakuja kutwambia kuwa leo tumeambiwa kuhusu vitendo vya ukatili kwa watoto wetu, lakini kutokana na baadhi ya wanajamii kuyapa kisogo ndo maana hayaondoki’’, alisema.
Mauwa alitaja mradi wa kukuza usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake GEWE, ndio ambao unawaelimisha wanajamii juu ya kupinga vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto kwa kuviriporina na kukemea.
Mradi huo uliobisha hodi katika shehia sita kwenye Wilaya ya Wete pekee kwa Pemba, ikiwa ni pamoja na Kinyikani, Shengejuu, Mchangamdogo, Kangagani, Kiungoni na Mjini Ole, umekuwa ukitoa mchango mkubwa juu ya kuondosha janga hilo sugu kwenye jamii.
Salma Abdalla Hamad ambaye ni mratibu anaeshughulikia shehia ya shengejuu Wilaya ya Wete, alieleza viongozi wa dini wanaendelea kupiga vita vitendo vya udalilishaji, ambapo wanapendekeza zaidi hukumu zitolewe kwa kufuata sheria za dini ya kiislamu, kwani zitaondosha matendo hayo.
‘’Kama sheria za dini ya kiislamu zitafuatwa katika kutoa hukumu kwa wanaojihusisha na vitendo hivyo, basi vita dhidi ya ukatili kwa wanawake na watoto vitafanikiwa’’, alisimulia wanachokisema masheikh hao katika hotuba zao juu ya kupinga udhalilishaji.
Kwa Wilaya ya Wete pekee jumla ya kesi 758 ziliripotiwa kuanzia mwaka 2015 hadi Oktoba mwaka huu, ikiwa ni pamoja na Ofisi ya ustawi wa jamii 333, Kituo cha mkono kwa mkono 165, Dawati la wanawake na watoto 209 na shehia sita zilizofikwa na mradi wa GEWE 51.
Haroub Suleiman Hemed ambae ni Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Wete, anashangaa kuona madrasa nako kuna rushwa za ngono, kwamba watu walioaminiwa kupewa uongozi na kuwafundisha watoto elimu ya dini baadhi yao wamekuwa wakiwadhalilisha.
“Inasikitisha sana kwa mwalimu wa madrasa kufanyia kitendo cha ukatili mtoto, kwani wanaaminiwa na jamii nzima na kuachiwa ulezi kwa kipindi chote wanapokuwa chuoni”, alisikitika Afisa huyo.
Huku uso wake ukionesha huzuni alisema, kuwepo kwa suluhu na kesi kutochukuliwa hatua za kisheria ipasavyo, inarudisha nyuma juhudi za taasisi binafsi zinazopinga vitendo vya udhalilishaji ikiwemo GEWE.
“Pamoja na viongozi wa dini kuchukua juhudi za kuelimisha jamii juu ya vitendo hivi, lakini kuna baadhi yao wako mstari wa mbele kufanya suluhu hasa watoto kuwaoza waume, jambo ambalo linasababisha kupalilia vitendo hivyo”, alieleza.
Yeye alipokea kesi za kudhalilishaji 333 kuanzia mwaka 2015 hadi Oktoba mwaka jana, ikiwa ni pamoja na kubaka 47, kulawiti 15, kutorosha 61, shambulio la aibu 20, mimba 12, kupigwa mbili, utelekezwaji 130 na mvutano wa kimalezi 46.
Mussa Rashid Said ambae ni sheha wa shehia ya Kinyikani alisema, kutokana na elimu iliyotolewa na mradi wa GEWE, baadhi ya wanajamii sasa wamekuwa na mwamko wa kukatazana juu za vitendo hivi, ikiwemo hao masheikh, walimu wa madrasa na maimamu.
“Katika shehia yetu masheikh wanajitahidi kukemea vitendo viovu ikiwemo udhalilishaji unaotendeka katika jamii, kwani hilo ni miongoni mwa majukumu yao, ingawa jamii bado haijajikubalisha kupambana na hali hiyo”alisimulia sheha huyo.
“Viongozi wa dini wanajitahidi kukemea kupitia katika hotuba zao hasa za swala ya Ijumaa, lakini kuna baadhi yao tena kidogo mno ambao wanaharibu na kuonekana viongozi wa dini wanaotenda mambo maovu”, alisema mratibu wa Kangagani Awena Salim Kombo.
Khamis Faki Simai ambae ni Mkuu wa dawati la kijinsi la wanawake na watoto Mkoa wa Kaskazini Pemba alisema, kuwepo kwa suluhu kwa kesi hizo, ni tatizo kubwa linalorudisha nyuma juhudi za wanaopinga vitendo hivyo na kupelekea kuoengezeka siku hadi siku.
“Kuna kesi ya kulawiti iliripotiwa, iliyopewa namba IR 209 ya mwaka 2017 ikimuhusisha mwalimu wa madrasa katika sheia ya Kiungoni, ingawa ushahidi haukupatikana kwa daktari wala kwa wanafamilia .
Na tayari mtoto ameshabadilika sauti na maumbile, kinachotusikitisha walikukuja jamii nzima, ili kesi ifutwe kwa madai ya kuwa hakulawitiwa”, alisikitika.
Ofisi ya dawati Mkoa huo, ilipokea kesi 206 kwa Wilaya ya Wete, zilizofikishwa mahakamani ni 36, zilizofutwa Polisi 22, zinazoendelea mahakamani nne, zilizopo kwenye upelelezi 14, zilizopata hatia saba, moja imeachiwa huru na kesi tano inasubiri kipimo cha kinasaba (DNA).
Mratibu wa wanawake na watoto shehia ya Mchangamdogo Siti Khatib Ali alieleza, masheikh wana mchango mkubwa katika kupunguza vitendo vya udhalilishaji kwa kutoa elimu misikitini, pamoja na madrasa za watu wazima.
Yeye kwenye shehia yake alipokea kesi tano za udhalilishaji kuanzia mwaka 2015 hadi Oktoba mwaka jana, ambapo kubaka ni kesi mbili, ujauzito mbili na ulawiti moja.
Asma Mohamed Fasihi ambae ni Mratibu wa kituo cha mkono kwa mkono Wilaya ya Wete yeye husikia hotuba mbali mbali kwenye misikiti zinazungumzia suala la udhalilishaji linavyoathiri siku hadi siku katika jamii, ambapo huamrisha yakemewe, kwani ni kitendo ambacho katika dini ya kiislamu kimekatazwa.
“Binadamu tumekuwa ni watu dhaifu sana, kwani lile tunalokatazwa sisi ndio tunakimbilia kulifanya, kutokana na kumuweka sheitwani mbele, hivyo elimu inahitajika zaidi ili wanajamii wazidi kuelewa madhara ya vitendo hivyo”, alifafanua mratibu huyo.
Mratibu huyo alipokea kesi za udhalilishaji 165 kuanzia mwaka 2015 hadi Oktoba mwaka jana, ikiwa ni kubaka 38, kulawiti 13, kutorosha 46, shambulio la aibu 15, mimba 35 na kupigwa 1.
Sheikh Ali Mohamed kutoka Jumuiya ya Maimamu Zanzibar (JUMAZA) Pemba, katika mkutano wa kujadili jinsi gani ya kuweza kuondosha vitendo hivyo katika ukumbi wa TASAF, alisema viongozi wa dini wamekuwa wakielimisha jamii juu ya athari ya vitendo hivyo, ili kuondosha kabisa.
“Wanajamii bado hawajaelewa vizuri suala la udhalilishaji, lakini elimu tunatoa kila siku kwenye mihadhara, madrasa na misikitini kila wakati, ili kuweza kupunguza wimbi kubwa la vitendo hivyo”, alieleza sheikh huyo.
Faza Zeno Marandu kutoka Kanisa Katiliki Chake Chake, alisema suala la kupiga vita vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto, lipo katika utaratibu wao, ambapo hulikemea kila wanapokuwa katika ibada na wanapokutana kwenye vikundi.
“Kila mtu anatakiwa aheshimu utu wa mwenziwe tangia kuzaliwa mpaka kufa pasi na kudhalilishwa, kila mmoja amjali mwenziwe, ili vitendo vya udhalilishaji viweze kuondoka”, alisema Faza huyo.
Mkurugenzi wa TAMWA Mzuri Issa alisema, suala la kupinga vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto sio la mmoja pekee, bali ni la jamii nzima na kuwataka viongozi wa dini kuwa mstari wa mbele kukemea.
“Mradi wa GEWE umejikita katika kutoa elimu kwa jamii juu ya kupinga vitendo vya udhalilishaji na kuviripoti pindi vikitokea, ili viweze kuondoka kabisa”, alisema Mkurugenzi huyo.
TAMWA katika jitihada zake za kuondosha tatizo la ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto, imekuwa ikitoa elimu kwa wanajamii kupitia mradi wa GEWE.
Comments
Post a Comment