Pemba Kusini watakiwa kuharakisha hukumu

Na Zuhura Juma,
Sauti ya Mnyonge, Pemba

MKUU wa Mkoa wa Kusini Pemba, Hemed Suleiman Abdalla, amewataka watendaji wa mahakama kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa kusikiliza na kuzitolea hukumu kesi kwa muda mfupi zaidi, ili kuondosha usumbufu kwa wananchi.

Alisema ili kufanya shughuli zao za kimaendeleo, ni muhimu kwa mahakama kuharakisha kesi na kuzitolea maamuzi mapema, jambo ambalo halitoathiri shughuli za kimaendeleo za wananchi katika kujiwezesha kiuchumi.

Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya sheria Zanzibar,zilizofanyika  katika uwanja wa Tenis Mjini Chake Chake, alisema Serikali itashirikiana na mahakama ili kuhakikisha haki inapatikama na kuimarisha uchumi wa nchi.

“Mashauri yanapokaa muda mrefu mahakamani bila kupatiwa hukumu, inaweza kuathiri  uchumi, kwani shughuli za wananchi huzorotesha shughuli za wananchi kiuchumi”, alisema Mkuu huyo.

Kwa upande wake, Jaji wa mahakama kuu Zanzibar ,Abdul-hakim Ameir Issa, aliwataka majaji, mahakimu na makadhi watimiza wajibu wao sambamaba na kufanya kazi kwa kufuata sheria, ili kuondosha mrundikano wa kesi na kuhakikisha hukumu zinatolewa ndani ya siku 60 kama sheria ilivyoeleza.

“Ushirikiano unahitajika kati ya watendaji wa Mahakama na wadau wengine, ili kuondosha malalamiko kwa wananchi, hii itasaidia upatikanaji wa haki kwa wananchi”, alisema Jaji huyo.

Alisema, mwaka 2018 watahakikisha suala la mrundikano wa kesi linakuwa historia katika mahakama zote Zanzibar.

Nae ,Mwanasheria dhamana kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka Pemba, Ali Rajab Ali, aliwataka wanasheria pamoja na watendaji wa mahakama kutii na kusimamia katiba na sheria, ili kuimarisha utawala wa sheria na kukuza uchumi wa nchi.

“Ikiwa tutazitii ipasavyo sheria na katiba, basi utawala wa sheria umeimarika na ukiimarika utawala na uchumi utakuwa, hivyo viongozi wawajibike ili kuondosha matatizo kwenye jamii”, alisema Mwanasheria huyo.

Jumla ya kesi 1322 za jinai  zimefikishwa  katika mahakama Kisiwani Pemba, ambapo kesi za jinai 1911 na kesi za madai 68 zimetolewa maamuzi.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni”Imarisha Utawala wa Sheria katika kukuza Uchumi wa Nchi”.

Comments

Popular posts from this blog

Wananchi wajenga wodi baada ya kuchoshwa na kujifungulia sakafuni

Sita wapotea katika mazingira tatanishi wilayani Wete

Jaji Mkuu Zanzibar awashukia mahakimu wanaonyanyasa watuhumiwa