Wanyonge wahimizwa kuwapatia watoto malezi pa pamoja kumaliza ulawiti na ubakaji
Imeandaliwa na Zuhura Juma
Sauti ya Mnyonge, Pemba
KWA miaka mingi Zanzibar ilisifika kuwa ni visiwa vilivyoheshimika, kwa watu wake kuwa waungwana, wema, karimu na waliokuwa na ihsani iliyotukuka.
Watu wake, hasa majirani, waliishi kama ndugu na kusaidiana kwa shida, msiba na furaha katika malezi ya watoto.
Kila mzazi alimuona mtoto wa mwenzake kama ni wake, na aliyekuwa hana mapenzi ya watoto alionekana mtu wa ajabu na haeleweki.
Kwa bahati mbaya, visiwa hivi katika miaka ya karibuni vimeanza kupoteza sifa hizo na watu wengi wanaamini hii inatokana zaidi na kukosekana malezi bora ya pamoja.
Hali hii, ilielezwa vizuri na bibi kizee mmoja kwa kusema, ilikuwa kawaida wakati wa ujana wake kama hakumuona mwanawe nyumbani, baada ya sala ya Ishaa hakuwa na wasi wasi.
Hii ilitokana na kuwa na uhakika kwamba, aliamua kulala katika moja ya nyumba za jirani tena bila ya wasiwasi wala wahaka, kama uliopo sasa.
Lakini siku hizi, hilo likitokea mzee huwa roho juu na nanga zina paa kutokana na kuibuka wimbi la watoto kutoweka karibu kila pembe ya Visiwa, na baadaye kusikia kuwa alibakwa na kutupwa.
Matokeo ya kutoweka utamaduni wa majrani kuishi kama watu wa familia moja na kulea watoto wao kwa pamoja, ndio kulikopelekea kuongezeka vitendo visiokuwa na heshima na utu, kama vya vya ulawiti watoto wadogo na ubakaji.
Haya usingetaraji kuwepo kwa kuzingatia kuwa, zaidi ya asilimia 95 na wengine wakisema 99, ya watu wake ni Waislamu, mbao ungetegmea kuepewa maelekezo na makatazo ya dini yao katika maisha.
Ukifanya utafiti utaona wazazi na walezi wengi siku hizi, wameyaacha maadili ya zamani ya kushirikiana katika malezi na matokeo yake ni vitendo vya ulawiti kuongezeka katika jamii, mijini na vijijini.
Kwa mfano, katika Wilaya ya Wete Pemba, kuliripotiwa matukio zaidi 600 ya udhalilishaji, ambapo 63 yalikuwa ni ya ulawiti, kati ya hayo ya ulawiti, dawati la wanawake na watoto tisa (9), Kituo cha mkono kwa mkono 13, ustawi wa jamii 15, ofisi ya mkurugenzi wa mashitaka tisa (9), mahakama 11 na shehia za GEWE ni kesi sita (6).
Dini nyingi, pamoja na ya Kiislamu, imeharamisha ulawiti na hili limeelezwa wazi wazi katika Suratul Al-a’raaf, aya ya 81 na 82 , juu ya haramu ya kufanya uchafu huu.
Aya hio inabainisha kwa kueleza; ‘Hivyo nyinyi mnawaingilia wanaume kwa matamanio mkawaacha wanawake? Kumbe nyinyi ni watu wafujaji (81)’.‘Na haikuwa ya kaumu yake isipokuwa kuambizana: wafukuzeni katika mji wenu, maana hao ni watu wanaojitakasa (82)’
Hata serikali na taasisi mbali mbali katika juhudi za kutoa elimu kwa jamii, zimekuwa zikipigavita vitendo vya udhalilishaji kwa wananawake na watoto, ili kuondosha janga hilo.
Miongoni mwa taasisi hizo ni TAMWA kupitia mradi wa kukuza usawa wa Kijinsia na kuwawezesha wanawake (GEWE), umekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha vitendo vya udhalilishaji, vinaondoka kwa kutoa elimu kupitia waratibu wa shehia.
Ni shehia sita tu kwa Wilaya ya Wete kati ya shehia wastani wa 2, kisiwani Pemba, ambazo zimebahatika kufikwa na mradi huo, ambazo ni Kiungoni, Shengejuu, Mchangamdogo, Kinyikani, Kangagani na Mjini ole.
Khadija John (58) mkaazi wa shehia ya Mjini ole anasema sababu kubwa ya kushamiri kwa vitendo vya ulawiti ni kuyatupa malezi ya zamani, ambapo wazazi walishirikiana kumlea mtoto katika jamii.
“Miaka hii ya demokrasia, kila mzazi ndio mtoto kwa mwanae, maana, anamuogopa hata kumkataza jambo lenye faida kwake’’, alisema akiashiria hakuna malezi.
Mama, alitamka kuwa, wazazi wa kileo kama hawakuamua kuyarejesha malezi ya pamoja, ni vigumu kutokea mabadiliko ya kimaadili kwa watoto.
Fatma Faki Kombo (65), mkaazi wa shehia ya Mchangamdogo anakumbushia, wakati yeye akiwa mdogo alikuwa na kila mzazi katika kijiji chao na heshima na nidhamu, ilitawala ndani ndani ya kijiji.
Sheha wa shehia ya Kiungoni Omar Khamis Othman (68), nae haridhishwi na malezi ya kisasa, akisema hayana faida kwa watoto wao, na wala hayafuati maadili ya Kizanzibari.
Ndio maana kwa sasa matendo ya ukatili huwafika wototo na wazazi, kutokana na kuacha malezi ya pamoja ambayo ndio yaliokuwa suluhu ya matatizo.
“Tukiamua kwa imani thabiti kuanzia kijiji kimoja hadi chengine kuwa na malezi ya pamoja, watoto hawatokuwa na nafasi ya kufanya matendo maovu’’, alisema.
Rashid Ali Hamad (44) wa Kiungoni, yeye anakumbuka zamani ilikuwa hakuna matendo ya ulawiti, ingwa kwa siku hizi imekuwa fasheni.
Mkongwe Omar Mohamed (50) wa shehia ya Kinyikani anasema malezi ya zamani yameondoka, kutokana na wazazi kukosa elimu.
Mzazi aliyeathirika kutokana na mtoto wake wa kiume kulawitiwa, aliyekuwa na miaka mitatu, mkaazi wa Shehia ya Mchangamdogo (45), anahamasisha kuwa, uwepo wa malezi ya pamoja, ni jambo linaloepusha matendo maovu katika jamii.
“Malezi ya zamani hasa yanasaidia kuepusha kutokea kwa vitendo vya udhalilishaji kwa watoto wetu, mtoto wako anakuwa wa mwenzako na wa mwenzako anakuwa wako’’, alibainisha.
Mama huyo anasema, kungekuwa na malezi ya pamoja mtoto wake asingepata janga la kulawitiwa, kutoka na alipokuwepo kulikuwa na watu.
“Alikuwa kwa jirani tu hapo, lakini kutokana na kuwa hatushirikiani tena katika malezi, alichukuliwa na mtoto wa miaka 13 na kwenda kumlawiti”, anasema kwa masikitiko.
Pamoja na kwamba sasa malezi ya zamani yameshatoweka katika jamii, na kila mmoja kumlea mwanae anavyotaka, lakini serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka mazingira ya kumlinda mtoto kwa uwepo wa sheria namba 6 ya mtoto ya mwaka 2011.
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, sura ya 3, kifungu 11 (1) na (2), kimeeleza kuwa ‘binadamu wote huzaliwa huru, na wote ni sawa, na kila mtu anastahili heshima na kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake.
Inawezekana jamii ya leo ya kizanzibari tena ambayo kwa asilimia 99 wanafuata mfumo wa maisha ya dini ya kiislamu, imekuwa ikiwaangamiza watoto kwa kuwakosesha malezi ya zamani yenye maadili mema.
Inawezekana kwa kutokuwepo kwa malezi ya pamoja, kuanzia mwaka 2015 hadi mwaka 2017, katika Wilaya ya Wete pekee, yameripotiwa matukio 63 ya ulawiti.
Kwenye shehia sita zilizopitiwa na utafiti huu, chini ya mradi wa GEWE yaliripotiwa matukio sita (6), hii ni inaonesha kwamba bado wanajamii hawana uelewa wa kutosha juu ya kupambana na tatizo hilo.
Ofisi ya Ustawi wa Jamii Wilaya ya Wete, kumeripotiwa kesi (15) za ulawiti kwa watoto wa kiume, ambapo kwa shehia sita za mradi wa GEWE hazijaripotiwa kesi katika ofisi hiyo.
Haroub Suleiman Hemed ambae ni Afisa Ustawi wa wa jamii Wilaya hiyo, anasema mporomoko wa maadili, kutokuwepo malezi ya pamoja, ni sababu moja wapo inayopelekea kuongezeka vitendo vya ulawiti.
“Ingawa tuna sera na sheria kadhaa za kuwakinga wanawake na watoto wetu na janga la udhalilishaji, lakini kama hatukuwa na malezi ya pamoja, tutachelewa”, alieleza.
Mratibu wa wanawake na watoto shehia ya Mjini ole, Khadija Henock Maziku, anasema kwa kipindi cha mwaka 2015 hadi mwaka 2017, ilirpotiwa kesi moja (1) ya ulawiti, ambayo wanajamii wenyewe wamesuluhishana.
“Awali walikuja kwangu kifua moto, kwamba wamelawitiwa mtoto wao wa miaka 11, na kijana Khamis Ibrahim (18), lakini kisha nawasubiri twende Polisi, nikasikia kasha pigwa bakora”, alinibainisha.
Sheha wa shehia ya Kinyikani Mussa Rashid Said (69) aliweka wazi kuwa, kwa karne hii wazazi wamejisahau na kuwapa uhuru mkubwa watoto wao, bila kuwauliza chochote.
“Iwapo wazazi wataendelea kuwaogopa watoto wao na kuwapa kila wanachokitaka, basi vitendo vya ulawiti havitoondoka’’, alifafanua.
Mratibu wa shehia ya Mchangamdogo Siti Khatib Ali (40) anaeleza kuwa, kwenye shehia yake, mwaka 2015 hadi mwaka huu, amepokea matukio mawili (2) ya ulawiti, ambapo moja iko mahakamani ikisubiri hukumu na nyengine ushahidi haukupatikana.
Mchanga Said Hamad (42) Mratibu wa shehia ya Kiungoni anataja kesi mbili (2) zilizoripotiwa kuanzia mwaka 2015 hadi mwaka huu, ambapo moja (1) iko Polisi na nyengine wenyewe walikwenda kuifuta Polisi, kwa madai kuwa mtuhumiwa alisingiziwa.
“Tukiendekeza suluhu matendo haya ya ulawiti hayatoondoka abadani, kwani wanaofanya ukatili huo wanaona hawana hukumu wanayopewa, hivyo huendelea”, anasema kwa huzuni Mratibu huyo.
Kwa mujibu wa Mkuu wa dawati la jinsi na watoto Mkoa wa Kaskazini Pemba, Khamis Simai Faki, anasema, kesi za ulawiti kwa watoto zimekuwa ni changamoto kubwa, inaikabili jamii ya sasa, kutokana na wanajamii kukosa elimu juu ya kupiga vita vitendo vya ukatili.
Katika kipindi cha mwaka 2015 hadi mwaka 2017dawati hilo, liliripoti kesi tisa (9) za ulawiti, tatu (3) zimeripotiwa kutoka shehia sita zilizofikiwa na mradi wa GEWE.
Ambapo, moja (1) inaendelea mahakama ya Mkoa Wete, mbili (2) ziko kwenye upelelezi, moja (1) imefungwa Polisi, kesi mbili (2) zimefutwa, mbili (2) zinasubiri hukumu na moja imepata hukumu, ambapo mshitakiwa alifungwa miaka saba (7) na faini ya shilingi 400,000.
“Mtoto wa miaka 10, alifanyiwa ulawiti na kijana Said Juma Msheli (20), lakini kidogo, afadhali maana kwa sasa anahemea chuo cha mafunzo, kwa miaka saba na faini juu”, alinieleza.
Ingawa sheria ya Kanuni na Adhabu no 6 ya mwaka 2004, ukikiangalia kifungu chake cha 132 (1), kimebainisha iwapo mtu mzima atabainika kumlawiti mtoto mdogo wa kiume, basi adhabu yake ni kifungo cha maisha.
Mratibu wa kituo cha mkono kwa mkono Wete, Asma Mohamed Fasihi, anasema chanzo cha kesi hizo, ni kutokana na mporomoko wa maadili, ambapo watoto wa sasa wamekuwa wakiiga maadili ya nchi za kimagharibi.
‘’Katika kituo chetu tumepokea kesi 13 za ulawiti kwa mwaka 2015 hadi mwaka huu 2017 katika Wilaya ya Wete, mwaka 2015 kesi tatu, 2016 kesi saba na mwaka huu tatu”, alifafanua Mratibu huyo.
Sheikh Ali Mohamed kutoka Jumuiya ya Maimamu Zanzibar (JUMAZA) kisiwani Pemba, anasisitiza wazazi kujua majukumu yao ya kuwalea watoto katika maadili mema na kushirikiana pamoja.
Anaona kufanya hivyo haswa ndio, itakuwa mwarubaini wa kuwalinda watoto dhidi ya vitendo viovu, ikiwemo ulawiti na ubakaji, ambao umepamba moto katika jamii ya kileo.
Hivi karibuni Mkuu wa Wilaya ya Wete, Abeid Juma Ali, anashauri malezi ya pamoja yarudishwe, ili kumlinda mtoto na janga la ulawiti, ambalo ni jinamizi linalowamaliza watoto wa kiume.
Mratibu wa chama cha Uzazi na Malezi bora (UMATI), Rashid Abdalla Rashid anasema elimu zaidi inahitajika kwa jamii juu ya malezi bora kwa watoto, ili kumuepusha mtoto kujiingiza katika matendo maovu.
Mwanasheria dhamana kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kisiwani Pemba, Ali Rajab Ali anasema sheria ya Kanuni na Adhabu namba 6 ya mwaka 2004, kifungu cha 132 (1) kiinamtia hatiani mtuhumiwa aliyemlawiti mtoto wa kiume kuhukumiwa adhabu ya kifungo cha maisha jela.
Mwanasheria huyo anasema, hakuna mtuhumiwa wa kosa la utawiti aliyefungwa kifungo cha maisha kwa kipindi kirefu, na ndio anaona matendo ya ulawiti yanaendelea siku hadi siku.
“Katika ofisi yangu, tumepokea kesi tisa (9) za ulawiti kwa mwaka 2015 hadi mwaka huu, zilizoripotiwa kutoka katika Wilaya ya Wete pekee”, anasema.
Mahakama ya Mkoa Wete, imepokea kesi 11 za ulawiti kuanzia mwaka 2015 Oktoba mwaka 2017, ambapo zinazoendelea ni sita (6), zilizofutwa nne (4), moja imefungwa na kesi tano zimehukumiwa.
TAMWA katika harakati zake za kupinga vitendo vya udhalilishaji kwa wanawake na watoto chini ya mradi wa GEWE, tayari imewapa elimu wanajamii wa Wilaya ya Wete kwa Pemba na Wilaya ya Magharibi na Kusini kwa Unguja, ili kuondosha kabisa vitendo hivyo.
Comments
Post a Comment