Soma namna watoto wa wanyonge wanavyosomea chini ya mti mkoani Mtwara
Na, Florence Sanawa
Sauti ya Mnyonge, Mtwara
WANAFUNZI wanyonge zaidi ya 200 wasomea chini ya mkorosho baada ya madarasa yao yaliyojengwa kwa udogo kubomolewa hali ambayo imewalazimu kusomea chini ya miti huku wakihofia kung’atwa na siafu miguu.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Omary Kipanga ameagiza madarasa hayo kubomolewa haraka huku wanafunzi hao wakianza kusomea chini ya miti ya mikorosho.
Akizungumzia hali hiyo Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Kipanga alisema kuwa majengo hayo yalijengwa kwa utashi wa wananchi bila kushirikisha halmashauri hiyo.
“Kile kilichokuwa kimejengwa sio kwa maagizo ya ofisi yangu mimi nilipita mwezi wa kumi shule zote kukagua lakini sikuona majengo kama yale kama ni kujenga wamejenga wananchi tena kama sio Novemba itakuwa Desemba…….
“Hata mwongozo wa wizara ya elimu hausemi tujenge darasa kama lile hata jiko hatukuambiwa tujenge mfano ule hatukuagiziwa yale sio madarasa hata ingekuwa ya muda yale sio madarasa ule ni uchafu ulipo sio mahala pake ndio maana nimeagiza yabomolewa”
Nae Mwalimu Mkuu Mitambo Shule ya Msingi Rashid Chalido alisema kuwa baada ya kikao cha wazazi na walimu kilichofanyika mwaka jana mwishoni walikubaliana kujenga madarasa hayo ili kuwanusuru watoto na kero za mvua zinazokuwa zinawakabili.
“Mwaka jana tulifanya kikao tuliona tatizo ni kubwa na watoto wanaathiriwa na mvua shuleni ndio maana tuliamua kujenga midule ya muda ili watoto wapate pakujishikiza lakini tumepata agizo kutoka uongozi wa juu ikitutaka tuvunje hiyo midure ili kuanza ujenzi wa madarasa manne ambao unaanza mara moja” Chalido
Kwa upande wake mwenyekiti wa Kijiji cha mitambo Salum Akola alisema kuwa kutokana na wazazi kuona adha waliyokuwa wakipata watoto shuleni hapo walilazimika kujenga madarasa ya muda ili kuwasaidia watoto hao.
“Kwakweli sisi tulikwama hata ukiangalia wanafunzi wengi wamekwua wakitapakaa hovyo nje hali ambayo inamfanya mwalimu kushindwa kuwadhibiti kutokana uhaba wa madarasa hivyo kufanya utoro kuongezeka nyakati za masomo” alisema Akola
Katibu Msaidizi Mtandao wa Mashirika yasiyokuwa yakiserikali Wilaya ya Mtwara (MTWANGONET) Fidea Luanda alisema katika mradi wa Ufuatiliaji wa Matumizi ya Rasilimali za Umma katika sekta ya elimu ulitembelea shule sita na kubaini uwepo wa hali mbaya ya mazingira ya shule hizo ikiwemo Mitambo.
Alisema kuwa mbali na shule hiyo kuwa na madarasa matano yaliyojengwa kwa udogo na kuezekwa kwa makuti bado mlundikano wa wanafunzi katika madarasa hayo ulikuwa mkubwa zaidi kutokana na kuchanganyishwa kwa madarasa mawili.
“Yaani kutokana na uhaba wa madarasa walimu wanafundisha darasa la saba huku darasa la sita wako darasani, na ukifatilia utaona kuwa zipo shule zina madarasa mawili watoto wako awali hadi darasa la saba niambie watasoma vipindi vingapi kwa siku ndio maana utoro umekuwa mkubwa watoto wanasoma kwa kupishana hii ni hatari” alisema Luanda
Comments
Post a Comment