Miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar na harakati za kupambana na rushwa
Na Haji Nassor
Sauti ya Mnyonge, Zanzibar
AZMA moja ya Mapinduzi ya Zanzibar, yalioasisiwa mwaka 1964, na jemedari wa Mapinduzi hayo, na rais wa kwanza wa Zanzibar marehemu Amani Abeid Karume, ilikuwa kuondoa ujinga, maradhi na rushwa.
Sasa ni miaka 54, ya Mapinduzi ya Zanzibar tokea, jemedari huyo kutukomboa sisi wazanzibari, katika mikono ya wanyonyaji na wakandamizaji waliokuwa wakila matunda ya wazalendo .
Aliwahi kusema kuwa“ leo wananchi sasa tuko huru, lazima tupambane na maradhi, ujinga na rushwa, maana hawa ndio adui wa haki” ni matamshi yake kati ya moja ya hutuba zake, akiwahutubia wanajeshi .
Kumbe wazo, fikira, busara na nia ya kuwakomboa wananchi wa Zanzibar na rushwa, kwa kiongozi huyu na rais wetu wa kwanza wa rais, ilianza zamani na leo ni miaka 54 sasa.
Maana kihistoria hata mtawala wa Zanzibar aliekuwepo ndani ya mwaka 1934 , alionekana kijibabaisha, kuwa eti anapamba na rushwa, wakati akiwakandamiza wazalendo.
Kwenye sheria Adhabu “Pin decree’ cap no 13 ya mwaka 1934, hasa sehemu ya 10, kwenye vifungu vyake vya 80 hadi 90 ilitaja kupambana na rushwa.
Ingawa wakati huo bado, jemedari wetu ambae ameshatangulia mbele ya haki, tokea mwaka 1972 kwa kuwawa na wapinga maendeleo, akiwa anasuka mipango ya kuwatimua watawala wa Zanzibar.
Sheria hiyo ya Adhabu, iliendelea kufanyiwa mabadiliko ya hapa na pale, hadi ilipofika mwaka 1975, wakati sisi tukisherehekea, miaka 11 tokea tuwe huru, ilibadilishwa jina.
Hapo sasa wazanzibari tukawa tunafanya mambo yetu, wenyewe, maana ule uhuru wa kufanya shughuli zetu ulikuwepo, kwa vile ule utawala wa kibaguzi na kidhalimu ulishaondolewa Zanzibar.
Kadri siku zilivyokuwa zikienda na mbele ya jemedari, ambae yeye aliuwawa na wapinga wa maendeleo mwaka 1972, fikra zake ziliendelea kutanua wazo la kupambana na rushwa, maana mwaka 1976 hadi mwaka 1979 ilifanyiwa tena marekebisho sherua hiyo.
Hadi mwaka 1985, wakati tukisherehekea miaka 21 ya Mapinduzi ya Zanzibar, ile sheria ya Adhabu, ilifanyiwa tena marekebisho, ingawa mamlaka hayo ya kupambana na rushwa, kama ilivyokuwa huko, nyuma walikabidhiwa tena Jeshi la Polisi.
Si unajua tena, wakati wa ukoloni wa waarabu na hata waengereza waliotawala hapa Zanzibar, hakukuwa na mzalendo aliekuwa na haki au fursa ya kufanya lolote hata la maendeleo.
Maana Asha Mansour (68) wa Wambaa, anasema hakukuwa na mwanamke wala mwanamme alikuwa na nguvu ya kufanya jambo, pasi n amri ya mabwana wakati huu.
“Leo tunapambana na rushwa wenyewe kikweli kweli, maana tumeletewa utawala bora, leo tunauwezo wa kutoa taarifa za rushwa popote”,anasifia.
Kubwa analoliona hapa, kwamba miaka 54 ya Mapinduzi Zanzibar, sio kusherehekea tu, kupata maji safi na salama, huduma za afya, elimu lakini hata kuwa na utawala bora na kupinga rushwa kwa vitendo”,anasema.
Kwenye miaka hiyo ya 1985, wakati Polisi ndio waliokuwa wakiongoza mapambano hayo, “Anti Corruption Police Squared”
Haya kama ukiamua kutaka kuyadadavua, basi ndio matunda na neema alizotuachia jemedari wa Mapinduzi ya Zanzibar, ambae alikuwa ndio rais wa kwanza wa Zanzibar.
Mapambano hayo ya rushwa waliokabidhiwa Jeshi la Polisi, kwa wakati huo chini Kamanda wa Idd Juma Msilimiwa, ilifanya kazi kwa mfumo wa madawati ndani ya jeshi hilo.
Hapo, wapo waliowahi kukamatwa hata Polisi mmoja, alikamatwa na rushwa ya shilingi 500 kwa wakati huo na kushitakiwa.
ASP Asha Talib kutoka Jeshi la Polisi Mkoa wa kusini Pemba, kwa sasa, akishikilia ukuu wa dawati la wanawake na watoto, alisema anakumba kuwa yupo Polisi aliewahi kukamatwa kwa rushwa.
“Huu ndio utawala wa wazalendo, maana tunafanya kazi wenyewe bila ya kusimamiwa, na tunaelekea kwenye utawala bora, ambao ulikuwa ndoto, leo tunamahakama na Polisi wetu”,anasema.
Kwa vile wazanzibar sasa wameshajitawala wenyewe ndani ya Miaka hii 54 ya Mapinduzi Zanzibar, basi nayo dhana ya utawala bora ikabisha hodi ndani ya visiwa hivi.
Namkumbuka sana aliewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa kusini Meja Mstaafu Juma Kassi Tindwa, wakati akiwahutubia wananchi wa wilaya ya Mkoa, akisherehekea miaka 48 ya Mapinduzi, ya Zanzibar alisema sasa utawala bora umefika kila pahala.
“Maana sasa ndani ya miaka hii 48 (kwa wakati huo), kila mmoja anasema na kuzungumza apendavyo, au kukosoa, jambo ambalo kabla ya mwaka 1964, halikuwepo.
Kwenye mwaka 2010, hadi mwaka 2011, na dhana ya utawala bora ilishika kasi, sana hapa visiwani, na ukichunguuza kama vile ndio azma na fikira za kufanyika kwa Mapinduzi Zanzibar.
Wakati mapambano ya kupinga rushwa, yakiendelea kushika kasi, hapo wadau na watu mbali mbali na hata vyama vya siasa walipendekeza sasa kuwe na chombo maalum cha kushughulikia rushwa.
Hapa wadau hawa wa Zanzibar ambao wako huru, walipendekeza pia, sasa kazi hiyo waondolewe Jeshi la Polisi na ikabidhiwe kwa taasisi husika.
Maana kabla na baada ya mapinduzi, mapambano ya rushwa, yalikuwa chini ya Jeshi la Polisi, kwa kutumia kikosi maalum, ingawa sasa baada ya sisi kujitawala watu walitamani kuwe na chombo maalum.
Ndipo ipofika mwaka 2012, wakati tukiwa kwenye maadhimisho ya miaka 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar, sasa yakatimia, kupitia chombo chetu cha kutunga sheria, Baraza la wawakilishi kwa kuipitisha sheria, no 1 ya mwaka 2012 ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar.
Ambapo kwa sasa, ndani ya miaka hii 54 Mapinduzi, kizuri ni kwamba mapambano ya rushwa yako kwenye taasisi kama inayojitegemea, badala ya kuwa chini ya Jeshi la Polisi ambayo inashughulikia mambo mengi.
Kassim Ali Omar, anasema kumbe Mapinduzi ya Zanzibar hayakuja tu kuwapa makaazi bora na elimu bora wananchi hawa, lakini hata suala la kuimarisha utawala bora.
Yeye anaamini sasa uwepo wa ZAECA ndani ya miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar wananchi, wake wanapata pahala pa kushitaki, kulalamika au kutaka ufafanuzi wakihisi wameonewa.
“Kabla ya Mapinduzi ulikuwa unadhalilishwa, unapigwa, unaonewa au kudiwa rushwa na wala huna pa kwenda kushitaki, lakini leo ZAECA ipo, na sasa wanyonge hawana wasiwasi”,anasema.
Hapa nilimuibukia Mdhamini wa ZAECA mkoa wa kusini Pemba, Suleiman Ame Juma, akisema wanacho cha kujivunia tokea ianzishwe Mamlaka hiyo, ikiwa ni pamoja na kuziokoa shilingi milioni 84.7.
Anasema kwa vile, sasa suala la Rushwa limechanganywa na kosa la kuhujumu uchumi, ambalo halijawahi kuingizwa kwenye makosa ya rushwa, ndio maana wameokoa mashamba ya serikali 30.
Hapa ZAECA, kutokana na kujitawala wazanzibar na kuamua kuanzisha chombo kipya chenye mamlaka ya kuzuia rushwa na uhujumu wa uchumi, ina uwezo wa kuingia kwenye chombo au wizara yoyote ya serikali, kufuatilia uhujumu wa uchumi.
Ndio maana hivi karibuni, walipiga kambi kwenye zoezi la ukodishaji wa mashamba ya mikarafuu, na kutokana udanganyifu uliofanywa na baadhi ya watendaji wa wizara ya kilimo, bado walifanikiwa kuyaokoa mashamba hayo.
Kumbe sasa ZAECA kwa mujibu wa Mdhamini wake mkoa wa kusini Pemba, Suleiman Ame Juma, anasema Mapinduzi ya Zanzibar, yameleta jambo jipya la kupambana na rushwa na uhujumu wa uchumi.
“Tokea mwaka 1934 hadi mwaka 2011, Zanzibar haijawahi kuwa na sheria nzuri ya kupambana na rushwa, kama hii iliopo sasa ya no 1 ya mwaka 2012, ambayo imeingiza na uhujumu wa uchumi, sasa lazima wazanzibar wajivunne”,anasema.
Kumbe yeye anasema heko jemedari wetu wa Mapinduzi Zanzibar, heko rais wa sasa wa Zanzibar Mhe: dk Ali Mohamed Shein, kwa kusimamia hilo hadi kuwa na sheria nzuri kuliko hata ile ya TAKUKURU Tanzania bara.
Mdhamini huyu, anasema ndani ya Miaka hii 54 ya Mapinduzi, sasa ZAECA inazo ofisi tatu, Pemba zikiweko mbili, kwa maana ya kusini na kaskazini, na moja ikiweko Unguja.
Kabla ya Mapinduzi ya Zanzibar yalioasisiwa mwaka 1964, hakukuwa na malalamiko yaliokuwa yakipokelewa na kikosi kazi cha Polisi cha mtawala, ingawa kwa sasa tena kwa kisiwani Pemba, ZAECA imeshapokea malalamiko 75.
Malalamiko 55 yanaendelea kufanyiwa uchunguuzi na watendaji wa ZAECA, wakati majadala nane (8) yako mezani wa DPP, na kesi mbili tayari ziko mahakamani.
ZAECA wanajigamba kuwa, Mapinduzi haya ya Zanzibar yaliofanyika mwaka 1964, yanaendelea kuokoa fedha za uuma, ambazo wachache wanazinyemelea, ili wajinufaishe wao, kwa mfano shilingi milioni 80 za shirika la Nyumba.
“Wapo wanaokodi nyumba za serikali, walijikusanyia deni kisha walipotakiwa kulipa, wakaanza kujitia kizungu mkuti, lakini sisi ZAECA tulitia timu na fedha hizio zikalipwa”,anasema kwa furaha.
Mkuu wa wilaya ya Mkoani Hemed Suleiman Addulla, anasema uwepo wa ZAECA, ndio inayonyesha dira na kusudio la Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.
“Aliekuwa hakuyafahamu Mapinduzi ya Zanzibar, basi aangalie kazi na malengo ya ZAECA, ni kuwatoa wananchi kwenye maonevu na kuwaweka kwenye utawala bora, ndio azma na nia ya Mapinduzi”,anafafanua.
Mwenyekiti wa Baraza ka Vijana wilaya ya Mkoani, Ali Said anasema kazi ilioridhiwa na Jemedari wa taifa hili, sasa linaendelea kufanywa kwa vitendo.
“Mimi napongeza sana kazi za ZEAC, maana hata viongozi wa serikali waliotumia madaraka yao vibaya, sasa wanahemea rumande na wengine washakosa kazi”,anasema.
Omar Khatib Omar na Mchanga Said Kombo wote wa Wawi, wanasema kazi inayofanywa na ZAECA, lazima iungwe mkono na kila mmoja, ili kutimiza ndoto na azma ya Mapinduzi.
Kwa hili hongera ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, hongera marehemu na jemedari wetu Aman Abeid Karume lakini heko rais wetu wa Zanzibar Mhe: dk Ali Mohamed Shein, kwa kuendelea kuyasimamia Mapinduzi ya yetu.
Comments
Post a Comment