Wazazi watakiwa kufichua watoto wenye maradhi ya moyo

Na, Haji Nassor
Sauti ya Mnyonge, Pemba

WAZAZI na walezi wa watoto wenye maradhi ya moyo Zanzibar, wametakiwa kuwafichua watoto wao, na kuwapeleka katika kliniki za hospotali za serikali, ili kufanyiwa uchunguuzi na kisha kupatiwa matibabu ya haraka.

Ushauri huo umetolewa na aliekuwa mgonjwa wa mwanzo Zanzibar kufanyiwa operesheni mbili ndani ya mwezi mmoja nchini Is-rail mwaka 1999  Arafa Abdulla Ali alipokua akizungumza na mwandishi wa habari hizi kisiwani Pemba.

Alisema ugonjwa wa moyo unatibika na unapona na kurudi katika hali ya kawaida, hivyo hakuna sababu kwa wazazi au walezi kuwavundika ndani watoto wao.

Alisema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia wizara yake ya Afya, imekuwa na ushirikiano mzuri wa kimatibabu na nchi za India na Is-rail, hivyo kwa sasa wazazi hawana sababu ya kuogopa gharama za matibabu, kwa vile hilo hubebwa na nchi husika.

Alieleza kuwa, yeye alifanikiwa kupona maradhi hayo ya moyo kutokana na wazazi wake, kumfikisha mapema hospitali ya Mnazi mmoja, na kisha baada ya uchunguuzi alipelekwa Muhimbili na kisha kusafirishwa nchini Is-rail.

Hivyo alisema wakati umefika sasa kwa wazazi na walezi hao, kuona kwamba wanawaepusha watoto wao na maradhi hayo ambayo athari yake ni kubwa.

“Wazazi waitumie fursa ya serikali iliopo ya matibabu bure, ambayo hutokana msaada kutoka kwa nchi mbali mbali kama vile Indie na Is-rail,”alieleza.

Katika hatua nyengine Arafa, alisema ni vyema kwa wazazi hasa walioko kisiwani Pemba kuzitumia kliniki zilizoanzishwa katika hospitali za Mkoani, Chakechake, Wete na Micheweni kwa ajili ya uchunguuzi.

Aidha amewataka watoto na watu wengine kujiunga na Jumuia ya watoto wenye maradhi ya moyo Zanzibar, ili kuwa na sauti moja ambayo itaharakisha haki yao ya matibabu.

Akizungumzia kuhusu gharama za hati ya kusafiria “pass port book” ameiomba serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kukaa pamoja na serilali ya Muungano, kuona watoto wanaondoshewa gharama hizo.

Alisema wapo baadhi ya wazazi wamekuwa wakishindwa hata kupata fedha za kugharamia hati hiyo, na wakati mwengine kukosa kwenda matibabuni nje ya nchi, au kuchelewa sana.

“Serikali yengebuni chanzo chengine cha mapato, lakini sio kuwabana hata wagonjwa tena watoto, jambo ambalo wakati mwengine huwaongezea maradhi,”alieleza.

Mapema Mwenyekiti wa Jumuia hiyo dk Omar Mohamed Suleiman, alisema miongoni mwa malengo ya jumuia hiyo, kupata haki za msingi za matibabu kwa wagonjwa wa moyo.

Alitaja malengo mengine kuwa ni, kuunga mkono matibabu ya wagonjwa mayo kwa kushirikiana na serikali, kuhamasisha matibabu ya wagonjwa wa myoyo, kujenge uwelewa katika jamii na kujua athari za kukosa uchunguuzi wa maradhi ya moyo.

“Jamii iendelee kutuunga mkono katika mampambano dhidi ya maradhi ya moyo, maana sasa hata kliniki zipo katika hospitali za Mkoani, Wete, Chakechake, Micheweni, Kivunge, Mnazi mmoja na Makunduchi,”alieleza.

Baadhi ya wazazi na walezi, wamesema wamekuwa na woga wa kuwapeleke watoto kuchunguuza maradhi hayo, kutokana na kutomudu gharama za matibabu.

Mwanamkasi Omar Haji wa Madungu Chakechake, alisema hakuwa na taarifa zozote za kuwepo kwa klinik hizo, ambapo kwa sasa atampeleka mwanawe hospitali ya Chakechake.

Khadija Mmanga Omar, alisema ugonjwa wa moyo ambao matibabu yake ni nje ya nchi, wamekuwa wakishindwa na gharama zake ambazo ni wastani wa shilingi milioni 40, hadi shilingi milioni 45.

Arafa Adulla Ali aliezaliwa mwaka 1995, ni miongoni mwa wagonjwa watano wa kwanza kutoka Zanzibar kupelewa nchini Is-rail kufanyiwa operesheni wa tundu mbili alizokuwa nazo za moyo, na sasa ni mwaka 19 akiendelea na maisha, ambapo ni mjumbe kwenye Jumuia ya watoto wenye maradhi ya moyo Zanzibar ‘OCHZ’.

Comments

Popular posts from this blog

Wananchi wajenga wodi baada ya kuchoshwa na kujifungulia sakafuni

Sita wapotea katika mazingira tatanishi wilayani Wete

Jaji Mkuu Zanzibar awashukia mahakimu wanaonyanyasa watuhumiwa