Waomba gharama za ‘passport’ kufutwa kwa wagonjwa wa moyo
Na, Haji Nassor,
Sauti ya Mnyonge, Zanzibar
JUMUIYA ya watoto wenye maradhi ya moyo Zanzibar ‘OCHZ’ imesema, wakati umefika kwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Zanzibar, kukubalia ili kuondoa gharama za hati ya kusafiria “pass port” kwa wagonjwa wa moyo, kwa lengo la kuepusha kukosa kufanyiwa matibabu nje ya nchi, baada ya wafadhili kukubali kugharimia matibabu yao.
Mwenyekiti wa Jumuia hiyo dk Omar Mohamed Suleiman, alisema wakati mwengine wagonjwa hao wengi wao wakiwa watoto, hupata ufadhili kutoka kwa mashirika mbali mbali ya kimataifa na watu binafsi, ingawa wapo waliokwama kwa kutokuwa na gharama za pasi ya kusafiria.
Akizungumza kwenye mkutano wa siku moja kwa madaktari, wadau wa maradhi ya moyo na wanahabari uliofanyika hospitali ya Chakechake, Mwenyekiti huyo alisema, gharama ya pasi ya kusafiria imekuwa ikiwakwaza, baadhi ya wazazi wenye kipato cha chini, ingawa wakati mwengine huwa wameshapa ufadhili wa matibabu hayo.
Alieleza kuwa kupitia Jumuia hiyo, wamekuwa wakiwahangaikia, watoto hao na wazazi wao, ingawa wakati mwengine hukwazwa na gharama ya lazima ya kuomba ‘pasport’ jambo ambalo kama halikuondolewa linaweza kuwa sababu ya kuongezeka kwa wagonjwa hao.
Hivyo Mwenyekiti huyo wa Jumuia ya watoto wenye maradhi ya moyo, alisema ni wakati mwafaka sasa kwa serikali, kuliangalia hilo kwa umakini, ili kuona wagonjwa wanaopata ufadhili wa kwenda nje kwa matibabu ya moyo, wanaondolewa gharama za hati ya kusafiria.
“Sisi kama Jumuia tumekuwa tukiwafuatilia na kuwaibua wagonjwa wa moyo, lakini hata ikitokezea tumewapata na vipimo vinaonekana wanahitaja kusafirishwa haraka sana, huwa kikwazo na gharama za hati ya kusafiria, hivyo serikali iandae mazingira ili isiwe kikwazo,”alieleza.
Katika hatua nyengine Mwenyekiti huyo aliwataka wazazi na walezi, kuwafichua watoto wanaoonekana na dalili za maradhi ya moyo, ikiwa ni pamoja na uvuvi wa kupindukia, kukosa hamu ya kula au kunyonya.
Dalili nyengine alioitaja Mwenyekiti huyo ambae pia ni daktari wa hospitali ya Mnazi mmoja, kuwa ni sauti yenye kukoroma, kunyonya na kukatisha na kisha kulia, kubadilika kwa rangi ya ngozi pamoja na ukuaji hafifu wenye kuambatana na kupungua uzito.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Jumuia hiyo, dk Helwa Abdulla Abdulla, alisema jambo kubwa ambalo linafanywa na Jumuia hiyo kwa sasa, ni kuishawishi serikali kupitia wizara ya Afya ili kuanzisha kliniki za maradhi ya moyo kisiwani Pemba.
Alieleza kuwa, katika hospitali zote za serikali kisiwani Pemba, hakuna kliniki hiyo, ingawa kuanzia mwezi Mei mwaka huu wanatarajia wawe na kliniki saba Zanzibar.
“Kliniki nne ni kwa hospitali za Mkoani, Chakechake, Wete na Micheweni kwa Pemba, na Mnazi mmoja ambayo ipo zitongezwa nyengine katika hospitali za Kivunge na Mkunduchi kwa Unguja,”alieleza.
Akiwasilisha mada ya kuutambua moyo na maradhi yake, daktari kutoka Hospital ya rufaa ya Mnazi mmoja Leila Mohamed Suleiman, alisema wakati umefika sasa kwa madaktari, kuwafanyia uchunguzi wa mapigo ya sauti watoto wote mara wanapozaliwa.
“Tunashauri sasa kuangalia uwezekano watoto wakishazaliwa na hasa wale wenye sura mfanano, wanafanyiwa vipimo ili kugundua iwapo wana maradhi ya moyo, na kisha iwe ni endelevu uchunguzi wao,”alieleza.
Daktari dhamana wa hospitali ya Chakechake Ali Habib Ali, alisema elimu na uhamasishaji bado inahitajika kwa jamii, ili kwanza wazitumie kliniki zitakazoanzishwa na kuelezwa dalili za wazi za maradhi ya moyo.
Jumuia ya watoto wenye maradhi ya moyo Zanzibar ‘OCHZ’ ambayo imeanzisha mwaka jana, ipo kisiwani Pemba ambapo pamoja na mambo mengine, inaangalia uwezekano wa kuanzisha huduma za maradhi ya moyo katika hospitali za wilaya ambapo huduma hizo kwa sasa zinapatika hospitali ya Mnazi mmoja pekee.
Comments
Post a Comment