Wanufaika wa TASAF waamua kupanda miti kuondokana na kero ya maji
Na Mwandishi Wetu
Sauti ya Mnyonge, Mtwara
Kutokana na wakazi wa wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara kukabiliwa na ukosefu wa huduma ya maji baadhi ya wanufaika na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tasaf kwa kushirikiana na baadhi ya wananchi wameanza kupanda miti ili kutunza mazingira na kurudisha uoto wa asili.
Kwa mujibu wa wataalam wa maji mkoa wa Mtwara ni asilimia 39.4 tu ya wakazi wote 107,117 ndiyo wanaopata huduma ya maji wilayani Nanyumbu.
Mradi huo wa uhifadhi wa mazingira unatekelezwa na wanufaika wa mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) awamu ya tatu kwa kushirikiana na baadhi ya wananchi baada ya kuona kukosekana kwa huduma ya maji ndio kikwanzo cha shughuli nyingine za kimaendeleo.
Akizungumza mratibu wa Tasaf wilayani humo ,Kilonzo Rajabu amesema katika utekeezaji wa mradi wa tatu wa Tasaf wananchi waliibua mradi wa utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti sehemu mbalimbali zenye ukame ili kurudisha uoto wa asili na tayari wameshapanda miti 60,000.
Mmoja wa wanufaika mzee Siamini Chiwata mkazi a kijiji cha Kazimoyo amesema miaka ya zamani kulikuwa na hali nzuri ya maji ambayo yalkuwa yakitiririka katika mito lakini baada ya mazingira kuharibiwa maji yamekuwa ya shida.
Akiwa wilayani Newala Januari 18 mwaka huu,Waziri wa maji, Mhandisi Isack Kamwele alisema mkoa wa Mtwara unatarajiwa kupokea dola za kimarekani 87.4milioni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji ikiwa ni sehemu ya dola za kimarekani 500 milioni zitakazotolewa na serikali ya India kutekeleza miradi 16 ya maji nchini.

Comments
Post a Comment