Wananchi Pemba walia uchakavu wa barabara
Na, Haji Nassor,
Sauti ya Mnyonge, Zanzibar
WANANCHI wanaotumia barabara za Wambaa, Kengeja, Kangani, Tundauwa, Chambani na Pujini mkoa wa kusini Pemba, wameiomba wizara husika kuangalia uwezekano wa kuzifanyia matengenezo ya haraka barabara hizo, kabla jazijaongezeka mashimo makubwa.
Walisema kwa sasa barabara hizo, zimeshaanza mashimo yenye ukubwa tofauti jambo ambalo huwapa usumbufu wakati wanapozitumia kwa shughuli zao mbali mbali.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti walisema, ni vyema kwa wizara hiyo kuwahi mapema kabla kuharibika zaidi kwa mvua zinazoendelea kunyesha.
Walisema baada ya barabara hizo kutumika zaidi ya miaka saba sasa, wakati umefika wa kuzifanyia matengenezo kwa kuziba viraka haraka kabla ya kuchakaa zaidi.
Mmoja katia ya wananchi hao Hassan Makame Omar wa Mwambe, alisema sasa barabara yao imeanza kurudi kwenye ubovu wa uwasili wake kutokana na kuzidiwa na mashimo.
“Mashimo yameanza kuwa mingi, jambo ambalo hupata mtikisiko mkubwa wanapokuwa safarini.
Nae Asha Faki Haji wa Wambaa alisema, mashimo yaliomo kwenye barabara yao kama yakiachwa bila ya kuzibwa yanaweza kuisababishia uchakavu zaidi.
Kwa upande wake Mwanajuma Haji Mjaka wa Tundauwa, alisema wao wanawake wamekuwa wakipata tabu hasa wanapokwenda hospital nyakati za usiku, kutokana na mashimo yaliomo.
“Twashukuru serikali ilitujengea barabara na kuitumia vyema, lakini sasa imeanza kuchakaa, ni vyema jitihada za kuifanyia matengenezo ya haraka zifanywe’’,alisema.
Mapema Afisa Mdhamini wizara inayoshughulikia barabara Hamad Ahmed Baucha, alisema serikali inalo lengo la kuzifanyia matengenezo barabara hizo ili zisiendelee kuchakaa.
Barabara za hizo za Mizingani- Wambaa, Mtambile –Mwambe, Chanjamjawiri- Tundauwa, Mtambile- Kangagani, Chanjaani- Pujini na Kenya- Chambani zilifunguliwa mwaka 2012 na rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi.
Comments
Post a Comment