Wananchi Mtwara watakiwa kuacha utegemezi wa zao la korosho pekee
Na Mwandishi Wetu
Sauti ya Mnyonge, Mtwara
Wananchi na wakulima wa korosho wilayani Tandahimba mkoani Mtwara wametakiwa kulima mazao mbadala na kuondokana na kutegemea zao la korosho pekee ambalo huvunwa kwa msimu mmoja.
Pia imeleezwa kutokana na wakulima wengi kutegemea korosho pekee huishia kuishi maisha ya kutegemea fedha za korosho pindi msimu unapoanza na wengine hulazimika kuuza korosho zikiwa mashambani ili kupata fedha za kujikimu kabla ya kuanza kwa msimu.
Hayo yameelezwa na mbunge wa Tandahimba, Katani Katani wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika jana wilayani humo na kueleza mazao mbadala kama muhogo kwa sasa soko lake ni la uhakika na mbegu zake ni za kisasa zenye uwezo wa kuhimili ukame kama wakulima watatumia wataalamu wa kilimo.
“Kama mwakalishi wa wananchi nitahakikisha mbegu zinapatikana kwa urahisi katika maeneo yote na kuwafikia wahitaji kwa wakati, sasa kinachotakiwa ni wakulima kuwa tayari kulima zao la muhogo na soko lipo ndani na nje ya nchi na tayari madiwa wanapatiwa mafunzo maalumu kwa hiyo mjiandaeni kulima muhogo,”amesema Katani
“Kwa muda mrefu tumekuwa tunashughulika na zao moja la koshoro ambazo fedha zake ni za msimu na kulima muhogo kidogo kwa ajili ya chakula, sasa nataka tukafanye kilimo cha muhogo kuwa cha biashara zaidi ya matumizi yetu ya nyumbani, ”amesema Katani
Mkulima wa korosho, mzee Omari Salumu amesema kilimo cha zao la muhogo lilikuwa likilimwa kwa wingi miaka ya themanini na kupata soko la ndani nan je ya nchi lakini badae wakulima wengi waliachana nalo.
“Miaka ya themanini zao la muhogo lilipata sana umaarufu katika hii mikoa ya kusini,lakini,sasa hivi wakulima wengi tunalima muhogo ili kupata chakula kama unga na kutafuna,lakini kama tukiletewa mbege za kisasa kama anavyosema mbunge mimi binafsi niko tayari kulima kwa ajili ya biashara ili tusisubirie fedha ya korosho pekee ambayo ni ya msimu,”amesema Salumu
Mkuu wa kitengo cha mazao jamii ya mizizi kutoka kituo cha Utafiti Naliendele, Benadetha Kimata amewashauri wakulima wote nchini kuyatunza mazao ya jamii ya mizizi hasa zao la muhogo na kukitumia kituo hicho kupata ushauri wa kitaalamu unaotolewa bure.
“Kwa sasa kanda ya ziwa ndiyo inayongoza kwa uzalishaji wa muhogo kwa asilimia 37 ikifuatiwa na kanda ya kusini asilimia 28 na kanda ya mashariki asilimia 12, hivyo basi sisi kama kituo cha utafiti tunawakaribisha wakulima na wananchi wote kwa ujumla kututumia wataalamu tuliopo ili walime kilimo chenye mafanikio zaidi,”amesema Kimati

Comments
Post a Comment