Walimu Sikonge wagomea taarifa ya fedha ya SACCOs yao
Na Mwandishi Wetu
Sauti ya Mnyonge, Sikonge
WAJUMBE wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Kuweka na Kukopa (SACCOS) cha walimu Wilayani Sikonge MkoaniTabora wamegoma kupokea taarifa ya fedha ya chama hicho kwa kutoweka wazi mchanganua wa mapato na matumizi yote.
Wakichangia mada baada ya Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya SACCOS hiyo Mashaka Faru kuwasilisha taarifa yake, wajumbe hao walisema taarifa hiyo haiko sawa, imeficha mambo mengi, haijachanganua kwa uwazi mapato na matumizi yote yaliyofanywa na viongozi waliopita.
Afisa Elimu Kata ya Sikonge Estomih Hilal alisema haiingii akilini Kiongozi kutumia mamilioni ya fedha za wanachama kwa mambo yasiyo ya kimaendeleo wakati walimu wana hali ngumu, na hata matumizi yenyewe hayakuidhinishwa na wanachama husika.
Alisema taarifa ya Mwenyekiti inaonesha dhahiri kuwa fedha zao zimehujumiwa na viongozi waliopewa dhamana, na kitendo cha Kaimu Mwenyekiti kusoma taarifa isiyo fafanua matumizi yote ni kupindisha ukweli, hatuwezi kuipokea, ikaandikwe upya.
Mwalimu Onesmo Bakete wa shule ya msingi Usunga alisema nidhamu ya matumizi ya fedha za michango yao haikuwepo ndio maana wameandika kimafumbo mafumbo tu pasipo mchanganuo wowote, hatuwezi kupokea taarifa ya namna hiyo, wameficha nini.
Katibu wa Chama Cha Walimu (CWT) wilayani humo Acheri Manjori alisema kuwa taarifa iliyosomwa ni kavu mno haikusema chochote kuhusu mishahara ya watendaji wa SACCOS, walikuwa wanalipwa fedha kutoka wapi, na kuongeza kuwa baadhi ya mikopo inaonesha kulipwa watu wasio wanachama ikiwemo walinzi.
Manjori alitaja mambo mengine ambayo hayakuainishwa kuwa ni taarifa za fedha, akiba za wanachama, michango ya NSSF, marejesho ya benki ya CRDB, mikopo ya ndani, posho, usafiri, masaa ya ziada, gharama za kimahakama na gharama za kibenki.
Mlezi wa chama hicho ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo,Simon Ngatunga alisema ni aibu sana kwa Viongozi tena wasomi kuandika taarifa ya juu juu kiasi hicho ambayo kiuhalisia imeficha mambo mengi.
‘Hii taarifa haijaandikwa kisomi, mfano kipengele kimoja kimeandikwa vikao viwili sh milioni 11 pasipo kufafanua uhalisia wa matumzi hayo na mengine mengi tu, huu ni udanganyifu, na kwa kifupi hii ripoti haifai nendeni mkaiandike upya’, alisema.
Alibainisha kuwa SACCOS hiyo ni ya wasomi, ndo maana wanataka haki zao zipatikane, na yeye kama Msimamizi Mkuu wa Maendeleo ya halmashauri hayuko tayari kuona walimu wanadhulumiwa haki zao.
Alifafanua kuwa kesi ya matumizi mabaya ya fedha za SACCOS hiyo inayowakabili waliokuwa Viongozi wa Ushirika huo iko mahakamani, na wote watakaobainika kutumia vibaya uongozi wao au kutafuna fedha hizo watachukuliwa hatua stahiki.
Meneja Uhusiano wa Benki ya CRDB anayesimamia Mikoa ya Tabora na Kigoma Luhende Boazi alibainisha kuwa kukosekana kwa uwazi katika taarifa ya viongozi hao ni matokeo ya kutoshirikisha wanachama na awali alishauri wafanye hivyo.
Alitaka kuainishwa vizuri mapato yote na matumizi wanayofanya na kutenganisha michango ya kawaida, marejesho, hisa na riba za wanachama.
Mwalimu Farida Aloyce kutoka Ofisi ya Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) wilayani humo alisema tatizo kubwa la Viongozi wa Ushirika huo ni kukosa weledi na kutokuwa na nidhamu kwenye fedha za walimu, ndo maana wameua SACCOS yao.

Comments
Post a Comment