Ushirikiano wahimizwa ili kulinda utamaduni wa Zanzibar

Na Haji Nassor
Sauti ya Mnyonge, Zanzibar

JAMII imetakiwa kushirikiana kwa pamoja, katika kulinda utamaduni wa nchi yao, huku wakijiepusha na matendo ambayo huiondoa hadhi na maadili ya kizanzibari. 

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Zanzibar Mshibe Ali Bakar, wakati alipokua akizungumza na wananchi katika semina ya siku moja, iliyofanyika katika ukumbi wa Mkuu wa Wilaya Mkoani Pemba. 

Alisema, iwapo jamii itakua tayari kushirikiana na serikali katika kulinda utamaduni wa kizanzibari, itaweza kupiga hatua kubwa na kuweza kuirejesha hadhi ya nchi yao. 

"Serikali ni watu, na watakapo kuwa madhubuti na serikali nayo itakua madhubuti kwani hakuna serikali inayotaka wananchi wake wapate shida, tupinge kwa kauli moja tutaweza kuirejesha Zanzibar yetu katika utamaduni wetu," alisema. 

Hata hivyo alieleza, hata sheria iwe nzuri kama dhahabu kama watumiaji wa sheria ni wabaya, haitoweza kufanya kazi kwani lengo lao ni kuona nchi inaendelea katika ustawi mzuri. 

Nae Mwanasheria kutoka Tume hiyo ya Kurekebisha Sheria Zanzibar Sabra Mohamed Iddi, akiwasilisha rasimu ya sheria ya kuhifadhi utamaduni wa Kizanzibari, alisema uwepo wa sheria hiyo utasaidia kutunza utamaduni wa Mzanzibar kwa kizazi hadi kizazi. 

"Kwa mujibu wa sheria hii, kuna mavazi hayaruhusiwi, ambayo yatazidi zaidi ya nchi mmoja kutoka shingoni kuelekea begani, kubana na kuonesha mwili wake pia kuvaa wigi au nywele za kuunga kwa mwanamke wa Kizanzibar,"alisema. 

Hata hivyo alisema kuvaa suruali ambayo imeruka kutoka nchi moja katika magoti kuelekea juu na kuonesha sehemu za siri, suruali yenye kubana, kuonesha sehemu za ndani ya mwili makosa kwa mwanamme wa Kizanibar kwa mujibu wa sheria hiyo. 

Mwananchi Mohamed Ali Bakar kutoka Kangani Mkoani alisema, katika sheria ya uvaaji wa mawigi na kuunga nywele, ni vyema tume ikaweza kuengeza sheria kwa wanaokata mikato hasa viduku ili kudhibiti na kulinda maadili ya Kizanzibar. 

Afisa sheria kutoka baraza la mji Mkoani Zubeir Awamu Zubeir aliunga mkono sheria ya kulinda utamaduni wa Zanzibar, huku akiomba kuekwe sheria kwa wageni wanaoingia nchini kupewa elimu ya uvaaji wa nguo ili kulinda maadili na utamaduni.

Nae Chumu Abdalla kutoka Kisiwa Panza, alisema lazima jamii isimamie matendo ya udhalilishaji ikisirikiana na vyombo vya sheria kwani ndio wanaoongoza katika kuzipatia suluhu kesi za aina hiyo. 

Tume ya Kurekebisha Sheria Zanzibar ipo kisiwani Pemba kwa ziara ya siku nne kwa lengo la kukutana na wananchi ili kukusanya maoni kuelekea kutunga sheria za utamaduni Zanzibar.

Comments

Popular posts from this blog

Sera ya Viwanda iendane na mabadiliko ya soko la wakulima

Ziara ya Jaji Mkuu Zanzibar mhe. Omar Othman Makungu katika picha

Mrajisi ataka wananchi kufika mahakamani kutoa ushahidi