TASAF yawezesha wengi kufikiwa na huduma za Afya Sikonge
Na Mwandishi Wetu
Sauti ya Mnyonge, Sikonge
MPANGO wa serikali wa kuwezeshaji kaya maskini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) awamu ya tatu umewezesha familia nyingi maskini wilayani Sikonge Mkoani Tabora kupata huduma za afya.
Wakizungumza na gazeti hili wakati wa zoezi la ugawaji fedha kwa kaya maskini baadhi ya wanafamilia wanaonufaika na mfuko huo wamesema mradi huo umewasaidia sana kwani wana uhakika wa kupata matibabu muda wowote ule.
Walisema mradi huo umewasaidia kuanzisha miradi midogo midogo ya kujikimu ikiwemo ufugaji bata, kuku, mbuzi na kilimo na wanapokuwa na shida yoyote ile ikiwemo magonjwa huuza sehemu ya mifugo au mazao na kwenda hospitalini.
Bibi Dainess Leonard (67) Mkazi wa kitongoji cha Kitimbashi katika kijiji cha Mkolye kata ya Mkolye wilayani humo alisema sh 40,000 anazowezeshwa na mradi huo zimemsaidia sana kupata matibabu katika zahanati ya kijiji na afya yake imeboreka zaidi tofauti na awali.
Mnufaika mwingine Asha Mohamed (49) mkazi wa kijiji cha Mlogolo alisema alipoingizwa katika mradi huo alinunua mbuzi 2 na kuku 3, wamezaliana na kufikia mbuzi 5 na kuku 17, mwaka jana aliuza mbuzi 2 ili kumtibia mumewe na mtoto wake na hali zao zinaendelea vizuri.
Alibainisha kuwa kabla ya kuingizwa katika mpango huo hakuwa na uwezo wowote wa kupata milo 3 kwa siku wala kwenda hospitalini na alishakata tamaa ya kuishi kutokana na hali yake kiuchumi na kuugua mara kwa mara lakini sasa ananunua dawa na afya yake imeimarika.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Mkolye Salumu Jonathan na Mtendaji wa kijiji hicho Yolata Michael walisema mpango huo ni mkombozi kwa wananchi kwani umebadilisha hali zao kiuchumi na afya zao sasa zinapendeza na wanashiriki shughuli za maendeleo.
Kutokana na umuhimu wa mpango huo waliomba serikali iboreshe mfuko huo ili kuwafikia wananchi wengi zaidi walio katika kaya maskini maeneo ya vijijini kwani kaya nyingi hazikuingizwa katika mpango huo.
Aidha walifafanua kuwa wanufaika wote wa mpango huo katika kijiji hicho wameshahamasishwa kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili waweze kupata matibabu katika zahanati, vituo vya afya na hospitali yoyote ile na wote wamekubali.

Comments
Post a Comment