TASAF yahifadhi chanzo cha maji Mkiang’ombe Pemba

Na, Haji Nassor,
Sauti ya Mnyonge, Pemba

WANANCHI 250 wa kijiji cha Mkiang’ombe shehia ya Tondooni wilaya ya Micheweni kisiwani Pemba, sasa watakuwa na uhakika wa kutumia maji yasiyochanganyika na ya bahari, kama ilivyokuwa nusu karne iliopita, baada ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania, awamu ya tatu (TASAF III), kukijengea kianzio hicho.

ENEO la kianzio cha maji kilichopo kijiji cha Mkiang’ombe shehia ya Tondooni wilaya ya Micheweni Kisiwani Pemba, ambapo kwa sasa kimehifadhiwa na TASAF III, na kuzuia uwezekano wa kuingia maji ya baharai kama ilivyokuwa miaka 50 iliopita, ambapo mradi huo umeibuliwa na walengwa waliomo kwenye mpango wa kunusuru kaya maskini shehiani humo
Awali wananchi  wa eneo hilo, walikuwa wanatumia maji ya matumizi ya kawaida yanayochanganyika na ya bahari, kutokana na kianzio chao kilichopo pembezoni mwa ufukuwe, kuingiliwa na maji ya bahari wakati yanapokuja juu.

Sheha wa shehia hiyo Abdalla Bakar Dawa, alisema wananachi wake walikuwa wakihangaika kwa nusu karne, maana kila maji ya bahari yanapojaa, ndio wananchi kwa kipindi hicho nao hukosa huduma hiyo.

MTOTO wa miaka mitatu na nusu mkaazi wa kijiji cha Mkiang’ombe shehia yake shehia Tondooni wilaya ya Micheweni kisiwani Pemba, akirudi kuchota maji kwenye chemchem iliohifadhiwa na TASAF, na sasa kuwawezesha hata watoto  na wazee kuchota maji, bila ya usumbufu wowote
Alieleza kuwa, tayari wananchi hao walishaamini kuwa wao shinda ya maji haitowandokea, kutokana na baadhi ya viongozi wanaowatembelea kuwapa ahadi wasioitekeleza.

Anasema baada ya TASAF II,I kuingia ndani ya shehia yake na kupatikana kwa walengwa wa kunusuriwa na umaskini, ndio walipoibua mradi huo, ambao kwa sasa unanuwafaisha wananchi wote.

Sheha huyo wa shehia ya Tondooni alieleza kuwa, mradi huo ambao uliendeshwa na TASAF, ulikijengea kisima hicho na kukizungurushia ukuta maalum, kwa ajili ya kuzuia maji ya bahari yasivamiwe kama ilivyokuwa zamani.

“Walengwa wetu waliomo kwenye mpango wa kunusuru kaya maskini, lazima tuwapongeze maana mradi huu wa kuhifadhi chanzo cha maji, ni tatizo tulilokuwa nalo kwa miaka 50 zaidi sasa,”alieleza.

Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho, alisema kwa sasa roho na hamu yao ya kukihifadhi kianzio hicho, zimeshatulia maana wanauhakika wa kuwa huduma endelevu ya maji.

Mwananchi aliejitambulisha kwa jina la Asha Hamad, alisema kwa sasa hawana wasiwasi tena, kwa kuhangaika huku na kule kutafuta huduma hiyo, kama ilivyokuwa zamani.

Nae Mtumwa Haidar alisema, kianzio hicho kwa sasa baada ya kuhifadhiwa, wanampango wa kwenda ZAWA ili huduma hiyo iwafikie wanakoishi.

“Hapa ilipo chem chem, hadi tunakoishi pana mlima mkubwa, hivyo ni usumbufu kwa sisi akinamama, kupandisha na ndoo, sasa taratibu za kuwatafuta ZAWA tumeshazianza,”anaeleza.

MRATIBU wa TASAF Pemba Mussa Said Kisenge, alieko mbele akiwaongoza wananchi wa kijiji cha Mkiang’ombe shehia ya Tondooni wilaya ya Micheweni, kupandish kwenye vigazi maalum, vilivyojengwa na TASAF, ili kuwasaidia wananchi kuondokana na utelezi wakati wanapopandisha na ndoo za maji kwenye mlima huo
Mratibu wa TASAF III Pemba, Mussa Said Kisenge alisema wao huwa hawana ugumu wa kuingiza fedha kwenye mradi wowote, ambao walengwa wenyewe waliomo kwenye mpango wameamua kuwa ndio changuo lao.

“Ndio maana mradi huo tumeingiza zaidi ya shiligi milion 13, pamoja na malipo ya walengwa waliopata ajira ya muda wakati wa ujenzi wa kuta za kukikihifadhi chanzo hicho,”anafafanua.

Hata hivyo, alisema mradi huo ambao pia ulihusisha ujenzi wa vigazi, ni vyema kwanza wananchi wakautunza ili uwe endelevu na ikiwezekana wawatumie wabunge, wawakilishi na halmashauri, kuomba fedha za kukamilisha.

“Inawezekana kwenye baadhi ya miradi kama huu wa kijiji cha Mkiang’ombe, bado zipo kasoro kama za vidaraja, sasa lazima na wananchi nao wajipange, kuwatafuta na viongozi wao wa majimbo, ili kuona wanakamilisha miradi yao,”alifafanua.

Hata hivyo Mratibu huyo wa TASAF Pemba, aliwashauri wananchi wote walioibuliwa miradi kupitia kwa walengwa wa kaya maskini, waelewa kuwa miradi hiyo inatakiwa kuwa endelevu kila siku.

Miongoni mwa miradi ilioibuliwa na walengwa waliomo kwenye mpango wa kaya maskini, ni pamoja na ukulima wa mboga mboga Chonga, Kibokoni, Mjini ole, ujenzi wa matuta ya kinga maji ya bahari Shidi, Kengeja na Shehia ya Ndagoni.

Comments

Popular posts from this blog

Wananchi wajenga wodi baada ya kuchoshwa na kujifungulia sakafuni

Sita wapotea katika mazingira tatanishi wilayani Wete

Jaji Mkuu Zanzibar awashukia mahakimu wanaonyanyasa watuhumiwa