Shirika la Umeme Zanzibar lakusanya bilioni 5 kwa siku 150 kwa wateja wake

Na, Haji Nassor,
Sauti ya Mnyonge, Zanzibar

SHIRIKA la Umeme Zanzibar ZECO tawi la Pemba, lenye wastani wa wateja 31,313 limeshakusanya shilingi bilioni 5 na milioni 183 kwa kip
indi cha miezi mitano, ilioanzia mwaka jana, hadi mwezi Febuari mwaka huu.

Taarifa kutoka ZECO zinaeleza kuwa, idadi ya wateja imekuwa ikiongezeka siku hadi siku, kutokana na huduma bora na imara wanazozitoa kwa wananchi na wakati wowote wananchi 200 waliobakia katika mita za zamani, watahamishiwa mita za kisasa.

Meneja wa shirika hilo Pemba, Mohamed Juma Othman alisema wamekuwa wakikusanya fedha zenye kiwango toafuti kutokana na mahitaji ya wateja wao kwa kila mwezi.

Alisema, kwa mfano katika mwezi wa Oktoba Shirika lilikusanya wastani wa shilingi milioni 961, ambapo mwezi Novemba kwa mikoa yote miwili ya Pemba lilikusanya shilingi milioni 975, ingawa mwezi Disemba mwaka jana, liliongeza na kukusanya shilingi bilioni 1.105.

Aidha katika kipindi cha miezi miwili iliopita ndani ya mwaka huu wa 2018 na kwenye mwezi wa Januari tayari wameshaingiza shilingi bilioni 1.025 wakati mwezi uliomalizika kwa Febuari, waliuza uniti za shilingi milioni 917.

Alisema anaamini serikali imeongeza pato lake katika kipindi cha mwaka mmoja sasa, baada ya visiwa vya Shamiani, Makoongwe, Kisiwa panza na Fundo kufikishiwa umeme na rais wa Zanzibar dk Ali Mohamed Shein.

“Kwenye visiwa hivyo pekee kuna wateja wetu karibu 627, sasa nguvu ya dk Shein ya kuwafikishia umeme wananchi hao, ni njia moja wapo ya kuongeza pato na kuimarisha maisha ya wananchi hao,’’alisema Meneja huyo.

Alisema kisiwa cha Fundo pekee kina wateja 340, Makoongwe 154, Shamiani Mwambe 20 na Kisiwa panza kimetoa wateja 113, ambapo kasi ya wananchi wanaoomba kuingiwa umeme inaendelea kuongezeka siku hadi siku.

Baadhi ya wananchi wa kisiwani Pemba wamelitaka shirika la umeme kisiwani humo, kuharikisha upatikanaji wa vifaa mara mteja anapokamilisha taratibu za malipo.

Saada Ismail wa kisiwa Panza alisema, wakati umefika kwa ZECO, kununua vifaa vya kutosha ili mwananchi anapomaliza taratibu asicheleweshwe.

“Mimi niwaombe ZECO kwamba kwa sisi wa visiwani pia tuwekewe kibanda cha malipo huku huku, maana tunapata tabu tukitaka lipa, sio wote wenye kujua kutumia mwamala wa simu,”alisema.

Nae Mati Haji Mwadini miaka 85, wa kisiwa cha Makoongwe, alilipongeza ZECO kwa kuamua kuwafikishia huduma ya umeme kisiwani huko na kufanikiwa kuunga kwa njia ya mkopo.

Aidha sheha wa shehia ya Fundo Khamis Abeid, amewataka wananchi wake kuendelea kubuni njia mwafaka za kuitumia nishati hiyo kwa maendeleo.

“Wananchi wanaweza kuanzisha sehemu za kuhifadhi samaki, uuzaji wa vinywaji baridi na viwanda na wakaongeza pato, hapo ndio watakapoona faida ya umeme,’’alieleza.

Katika hatua nyengine baadhi ya wananchi kisiwani Pemba, wamelitaka shirika la Umeme kufuatilia miundo mbinu yake hasa katika kipindi hichi cha mvua.

Visiwa vya Makoongwe, Fundo, Shamiani na Kisiwa panza vimefikishiwa huduma ya umeme hivi karibuni, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya rais wa Zanzibar dk Ali Mohamed Shein alioitoa kwa wananchi hao wakati wa kampeni.

Comments

Popular posts from this blog

Wananchi wajenga wodi baada ya kuchoshwa na kujifungulia sakafuni

Sita wapotea katika mazingira tatanishi wilayani Wete

Jaji Mkuu Zanzibar awashukia mahakimu wanaonyanyasa watuhumiwa