Daktari ajitolea kutibu watoto wa wasiojiweza kwa pesa zake mwenyewe

Na, Haji Nassor,
Sauti ya Mnyonge, Pemba

MKUU wa Kituo cha Afya kisiwa cha Makoongwe wilaya ya Mkoani Pemba, Rajab Juma Seif, ameamua kununua asali kwa fedha zake, ili kuwasaidia watoto wenye kuumwa na kifu kwa muda mrefu.

Alisema, aliamua kufanya hivyo ili kuwasaidia watoto na hasa ambao wazee wao hawana uwezo, ili kuponya kifua kwa pale wanapohitaji matumizi ya dawa hiyo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi hospitalini hapo, alisema zipo dawa ambazo hushabihiana na asali matibabu yake, ambapo pia kama mgonjwa akikosa dawa husika akitumia asali anaweza kupona na ndio maana ameamua kuwa nayo.

Alisema asali hiyo huwauzia wanaohitaji kati ya shilingi 2,500 hadi shilingi 3,000 na wale wasio kuwa na uwezo kabisa wakati mwengine huwapa bila ya malipo yoyote.

Mkuu huyo wa Kituo cha Afya cha kisiwa cha Makoongwe, alisema sio wote wanaoumwa kama wanauwezo wa kununua dawa zinazokosekana hospitali, na ndio maana ameaandaa utaratibu huo, ikiwa ni njia ya kuwasaidia wananchi.

“Wapo watoto wamekuwa wakiuumwa na kifua kwa muda mrefu na pengine kwa dawa za hospitali kifua hicho hakipoi, sasa huwapa asali mwenye uwezo na asiekuwa nao, na wote wanapoa,”alieleza.

Katika hatua nyengine daktari huyo, alisema kwa sasa huduma kwenye kituo hicho zinaendelea vizuri na changamoto za hapa za pale ni jambo la kawaida, kwa vile hakuna jambo lililokamilika ulimwenguni.

Kuhusu huduma za kuzalishia wajazito, alisema kwa sasa bado na hawazalishi hata kwa dharura ambapo huwataka akinamama kuvuuka bahari na kwenda hospitali ya Mkoa ya Abdalla Mzee Mkoani.

“Umeme kwenye kituo chetu kwa miaka miwili sasa upo, lakini hatujaona matunda yake, maana hatuzalishi na wala hatuna huduma ya kung’oa meno ni kumchemshia sindano tu na kuonea,”alifafanua.

Baadhi ya wananachi wa kisiwa hicho, wameiomba wizara ya Afya wasijejaribu kumuondoa daktari huyo na kumpeleka sehemu nyengine, kutokana na utendaji wake wa kazi ulivyo mzuri.

Dhamir Kombo Foum (60), alisema hata kama kituo chao kina uhaba wa madaktari, lakini mkuu wa kituo aliepo amekuwa akitoa huduma saa 24.

Nae Asha Ali Mussa muhamasishaji wa mama wajazito kwenda klinik na kujifungulia hospitali, alisema kwa sasa wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa, kuwahamasisha wajawazito kwenda klinik.

Kuhusu huduma ya ziada inayotolewa na daktari huyo ya asali kwa watoto wenye kuumwa na kifua, alisema ni jambo jema na ndio ambalo limewafanya wananchi wa kisiwa hicho kupendezewa na huruma zake.

Kwa upande wake sheha wa shehia ya Makoongwe Silima Hija, alisema kazi iliobakia kwa wizara ya Afaya Zanzibar, ni kukipandisha hadhi ya huduma kituo chao, ili wajawazito wajifungulie hapo.

“Ni jambo la kawaida mjamzito kujifunguali baharini, au kenye gari wakati akipelekwa hospitali ya Mkoa, maana ndio kituo chetu hakina huduma hiyo, ni usumbufu,”alieleza.

Kwa upande wake Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed alisema, suala la kuimarisha huduma za uzazi kwenye visiwa, ndio miongoni mwa vipaumbele vyao.

Alisema wizara inawapenda wananchi wote, na ndio maana imekuwa ikisambaaza huduma za aina mbali mbali, ambapo na hizo za kujifungulia nazo watapelekewa sio muda mrefu.

Hata hivyo amwataka wananchi kuendelea kusisitizana juu ya kwenda klinik na kisha kujifungua hospitali ikiwa ni njia moja ya kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), limeweka mikakati na miongozo mbalimbali kuzitaka nchi zote kuhakikisha zinatenga bajeti za kutosha kwa ajili ya wizara za afya hasa kwa upande wa huduma za mama na mtoto.

WHO, linasaidia uimarishaji wa huduma hizo kwa kutoa misaada kuanzia fedha, vifaa na wataalamu hasa katika nchi zinazoendelea ili kuokoa maisha ya mama na mtoto Zanzibar ikiwemo.

Bajeti ya mwaka 2016/17 ya Wizara ya Afya imeweka wazi muongozo wa kutoa elimu kwa mama wajawazito kuhusu vidokezo vya hatari pamoja na lishe.
  
Wafanyakazi 70 wamepatiwa mafunzo ya kutumia muongozo huo, ili kuhakikisha wajawazito wanajifungua hospitali, ambapo wizara imeanzisha mpango maalumu wa ufuatiliaji kwa baadhi ya wilaya.

Kisiwa cha Makoongwe wilaya ya Mkoani Pemba, kina wakaazi 2, 225 wanawake wakiwa 1,196 wanaume 1,029 ambapo kati ya hao watoto ni 1,172 ambapo hadi sasa akinamama wajazito wanalazimika kuvuuka bahari wakati wanapotaka kujifungua hadi hospitali ya Abdalla Mkoani.

Comments

Popular posts from this blog

Wananchi wajenga wodi baada ya kuchoshwa na kujifungulia sakafuni

Sita wapotea katika mazingira tatanishi wilayani Wete

Jaji Mkuu Zanzibar awashukia mahakimu wanaonyanyasa watuhumiwa