Ahukumiwa kifungo cha miaka 11 kwa kubaka na kumpa ujauzito mwanafunzi

Na, Haji Nassor,
Sauti ya Mnyonge, Zanzibar

MAHAKAMA ya mkoa Chakechake, imemtupa chuo cha mafunzo miaka 11 kijana Yassir Mohamed Nassor miaka 19, wa Machomane, baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka na kisha kumpa ujauzito mtoto wa miaka 13.

Hakimu wa mahakama hiyo Hussein Makame Hussein, alitoa adhabu hiyo, baada ya kijana huyo kupatikana na makosa mawili sambamba, ambapo kosa la kwanza la ubakaji atatumikia miaka saba (7) na kutoa fidia ya shilingi laki 600,000.

Ambapo kosa hilo ni kinyume na kifungu cha 125 (1), (2) (e) na 126 (1) cha sheria no 6 ya mwaka 2004 sheria ya Zanzibar.

Kosa la pili alilobainika nalo kijana huyo mbakaji, ni kumpa ujauzito mtoto huyo wa miaka 13, ambapo kinyume na kifungu cha 3 (3), (4) sheria ya kuwalinda wari na wajane no 4 ya mwaka 2005.

Kosa hilo, Hakimu Hussein baada ya kuwasikiliza mashahidi tisa akiwemo Mchunguzi mkuu na mtaalamu wa vina saba DNA, mtoto mwenyewe, daktari, mpelelezi, mama mzazi ndipo alipotumia sheria na kumpeleka chuo cha mafunzo miaka minne (4) na kulipa fidia ya shilingi laki 600,000.

Mapema Mwendesha Mashitaka, kutoka Afisi ya Mkurugenzi wa Mashiataka Ali Haidari baada ya kufunga ushahidi kwa upande wake, aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali.

Haidari aliimbia mahakama hiyo, matendo ubakaji na kuwapa mimba watoto, limekuwa ni janga ndani ya nchi, na kisha kuwapelekea watoto hao kupata athari za kimwili na akili.

“Muheshimiwa Hakimu naiomba mahakama yako, kutoa adhabu kali kwa mashitakiwa huyu, maana vijana katika miaka hii wamekuwa watukutu na kuwasababisha wanaowadhalilisha kukatisha ndoto zao, hivyo adhabu ikiwa kali itakuwa fundisho na kwa wengine,”aliomba PP.

Akitoa ushahidi wake, Mchunguuzi Mkuu kutoka Afisi ya Mkemia Mkuu Fidel Segumba, aliiambia mahakama kuwa, sampuli za damu alizokabidhiwa kwa ajili ya uchunguzi zimehalalisha kuwa, damu ya baba mzazi na ya mtoto zinashabihiana.

“Muheshimiwa hakimu, naomba niiambie mahakama yako kuwa, sampu ya baba na hii ya mtoto zinakubaliana kwa asilimia 99.99 kuwa hawa ni mtu na mwanawe na vipimo havina shaka,’’alieleza.

Nae muathirika wa kesi hiyo mtoto miaka 13, alikiri mahakamani hapo kuwa, Yassir Mohamed Nassor alimchukua kutoka nyumbani kwao na kumpeleka Batini na kisha kumuingilia.

Daktari wa hospitali ya Chakechake, aliemfanyia uchunguuzi mtoto huyo, aliithibitishia mahakama kuwa, vipimo vilionesha alikuwa na ujauzito wa wiki 21 kwa wakati huo.

Nae mama mzazi wa mtoto huyo alieleza kuwa, ni kweli mwanawe mwezi wa 11, mwaka 2013  majira ya saa 8:30 jioni alitoweka nyumbani kwake, na kwenda sehemu asikokojua yeye.

“Ni kweli mwanangu baada ya kumuhoji alimtaja mshitakiwa kuwa ndie aliekuwa nae, na alimpa ujauzito na miezi tisa baadae alijifungua,”aliiambia mahakama mama huyo mzazi.

Kabla ya kupewa hukumu huyo, Hakim Hussein alimpa nafasi mshitakiwa huyo, kujitetea na aliomba mahakama kupewa mtoto wake,ili amlea jambo ambalo akiwa chuo cha mafunzo atalikosa hilo.

“Unajua Hakim mtoto ni malezi ya baba na mama, sasa naiomba mahakama yako tukufu, inipunguzie adhabu maana nnalengo la kufunga nae ndoa mama mzazi, ili kuendeleza malezi ya mtoto na akuwe katika misingi inayokubalika,”aliomba .

Utetezi huo ulipigwa na chini mahakamani hapo, na kupewa adhabu ya miaka 11, ambapo miaka saba kwa ubakaji na miaka minne kwa kosa la kumpa ujauzito, ambapo adhabu hizo atatumikia moja baada ya nyengine na fidia ya shilingi milioni 1.2.

Hata hivyo Makama hiyo, haikumtia hatiani mshitakiwa huyo kwa kosa la tatu la utoroshaji, bada ya ushahidi ualiowasilishwa mbele ya mahakama hiyo, kuwa lege lege.
Haki ya rufaa ndani ya siku 30, imetolewa mahakamani kwa yeyote ambae hakuridhika na adhabu hiyo.

Wiki mbili zilizopita Mahakama hiyo, ilitoa adhabu ya kifungo cha miaka saba chuo cha mafunzo, kwa mshitakiwa Omar Haji Ali miaka 28, aliepatikana na kosa la ubalaji kwa mtoto wa miaka 12.

Comments

Popular posts from this blog

Wananchi wajenga wodi baada ya kuchoshwa na kujifungulia sakafuni

Sita wapotea katika mazingira tatanishi wilayani Wete

Jaji Mkuu Zanzibar awashukia mahakimu wanaonyanyasa watuhumiwa