Afariki dunia kwa kujinyonga akiwa msikitini
Na, Haji Nassor,
Sauti ya Mnyonge Zanzibar
KIJANA mmoja Azani Abdalla Suleiman (28)mkaazi wa Ole Mchanga Mrima Mkoa wa Kaskazini Pemba, amefariki dunia usiku wa kuamkia jana, kwa kujinyonga katika Msikiti ulipo kijiji cha Machomane Wilaya ya Chakechake mkoa wa Kusini Pemba.
Akithitisha kutokea kwa tukio hilo, kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa kusini Pemba Sheihan Mohamed Sheihan alisema, tukio hilo limegundulika wakati waumini wa dini ya kiislamu, walipofika msikitini kwa ajili ya kusali sala ya alfajiri.
Alieleza kuwa mara baada ya watu hao kuingia Msikitini kwa ajili ya kutekeleza ibada hiyo, ndipo walipokutana na mkasa huo na kuona maiti ya kijana huyo ikiwa inaninginia kutokana na kamba aliojifunga.
Sheihan alisema taarifa walizobaini kwa haraka sana ni kwamba juzi kijana huyo alifika kwa Babu yake ambae ni Omar Hamad Bakari mkaazi wa Machomane Chake Chake na kumpatia taarifa juu ya adhama yake ya kutaka kufunga ndoa.
‘’Tumeambiwa kwamba hakukua na mafahamiano mazuri na babu yake mara baada ya kumpa taarifa hio na ndipo usiku ulipofika akamtaka mjukuu wake huyo aongozane na kijana wake mwengine wende wakapumzike, lakini badae ndipo kijana huyo alitoka na kwenda kujitundika Msikitini hadi kifo chake,’’aliongezea Sheihan.
Kamanda alilitaja tukio hilo ni la kusikitisha huku akisema si miongoni mwa matukio ambayo yamezoeleka kutokea katika Mkoa wake kiasi ambacho yeye mweye anahuzunika.
Alisema jamii hususani wazazi wawe na utaratibu wa kuzungumza lugha nzuri na watoto wao ili kuepusha matukio ya aina hio ambayo alidai anaamini yanaweza kupatiwa suluhu yake ili kuepusha vifo visivotarajiwa.
Katika hatua nyengine alisema wamefikisha mwili wa marehemu huyo katika hospitali ya Chake chake na mara baada ya kufanyiwa vipimo hakuonekana na jeraha lolote lile linaloashiria kupiga au kuteswa kabla ya kifo chake.
Salim Juma ambae ni miongoni mwa watu walioshuhudia maiti hio ikiwa ndio kwanza inaningia alisema walishtuka sana uwepo wa maiti hio kwenye nyumba ya ibada.
Alieleza kuwa mara baada ya kuona maiti hio walifanya jitihada za kuwasiliana na jeshi la polisi kwa hatua nyengine zaidi.
Babu wa marehemu huyo kwa hatua za awali hakupatikana kuzungumzia tukio hilo, kutokana na kushughulikia mazishi na likuwa nje ya kijiji cha Machomane.
Comments
Post a Comment