Wizara yasikia kilio cha madereva kuhusu alama tata ya barabarani

Na Haji Nassor
Sauti ya Mnyonge, Pemba

BAADA ya malalamiko ya madereva kutoifahamu alama ya barabarani, iliopo eneo la Chamanangwe wilaya ya Wete Mkoa wa kaskazini Pemba, na kusababisha askari wa usalama barabarani kuwakamata, wizara ya Ujenzi, Miundombinu na Mawasiliano, imesema itaibadili alama hiyo.

Akizungumza na mwandishi wa habari, hizi Mhandisi ujenzi wa kutoka wizara hiyo, Pemba Khamis Massoud, alisema inawezekana hao askari wanawakamata madereva kwa kutoifahamu matumizi yake.

Alisema eneo hilo lenye usawa mrefu, na kutanguliwa na alama ya kumruhusu dereva aende mwendo atakao, lakini wapo baadhi ya askari huwakamata madereva pale wanapopindukia alama 40.

Alisema inawezekana kweli, wapo baadhi ya madereva wamekuwa hawazielewi alama hizo, na wengine kwenda mwendo wa pole au wa kuibia hadi wa alama 60 ay 70 na wanapokamatwa hushindwa kujitetea.

“Ni kweli unaweza kupishana na dereva anaendesha mwendo wa alama 40 katika eneo hilo,  kama kule aliokotokea kwenye mipindo na mikusanyiko ya watu, lakini eneo la Chamanangwe ambapo pana alama ya 40 iliolaliwa na michoro minne meusi ni ishara ya dereva kwenda atakavyo,”alieleza.

Hata hivyo Mhandishi huyo, alisema lipo kosa jengine kuanzia skuli ya Mbuzini ukitokea Wete kwenda Chakechake, napo wanakusudia kuparekebisha, ili kuwapa ruhusa madereva kuongeza mwendo.

Katika hatua nyengine, amewataka wamiliki wa gari kuhakikisha madereva wanaowapa gari zao wanazifahamu vyema sheria za barabarani, ili kuepusha ajali zisizokuwa za lazima.

Dereva mmoja wa gari ya mzigo, Khamis Mtumweni alisema, pamoja na kuzisoma alama za barabarani, lakini iliopo eneo la Chamanangwe haifahamu matumizi yake.

“Katikati ya usawa uliopo eneo hilo, utakuta askari wa usalama barabarani wapo, na wakishakumulika kwa tochi yao, wanakushitaki kwa kwenda mwendo kasi, sasa twashangaa ni wao au sisi tusiojua matumizi ya alama ile,”alieleza.

Nae Kombo Hamad Hamad wa gari ya abiria, alisema kuanzia eneo la meli tano kwenda barabara ya Konde, kumejaa alama za barabarani, zinazowataka kwenda mwendo wa alama 40.

“Mimi nikifika eneo la Chamanangwe, huwa najiuliza alama hii 40 iliozibwa kwa michoro meusi, ina maana gani, mara naongeza na mara napunguza, maana siijuwi lengo lake,”alisema.

Omar Haji Msabaha aliiomba wizara husika, kwanza kuwaelimisha askari wa usalama barabarani, ili kujua matumizi sahihi ya alama hizo, maana alishawahi kukamatwa eneo hilo.

“Mimi nilikuwa sijui matumizi sahihi ya alama ile, lakini niliwapa mtihani askari baada ya kunikamata, nikawambia kuwa nimeruhusiwa kuongeza, lakini walikuwa wakali,’’alisema.’

Katika hali iliotajwa ya kupunguza ajali zisizokuwa za lazima, ndio maana wizara husika kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, limeweka alama mbali mbali kuanzia eneo la meli tano kuelekea Konde.

Comments

Popular posts from this blog

Wananchi wajenga wodi baada ya kuchoshwa na kujifungulia sakafuni

Sita wapotea katika mazingira tatanishi wilayani Wete

Jaji Mkuu Zanzibar awashukia mahakimu wanaonyanyasa watuhumiwa