Wanawake Pemba waaswa kuhusu matumizi sahihi ya simu

Na Hanifa Salim
Sauti ya Mnyonge, Pemba

WANAWAKE wametakiwa kuhakikisha wanatumia simu kwa kufuata sheria sambamba na kujua haki na wajibu huku wakijua sehemu sahihi za kulalamika pindi tatizo la mtandao linapojitokeza.

Wito huo umetolewa na Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA Zanzibar Esuwatie Aisa Masinga, wakati alipokua akizungumza na wanawake wajasiriamali katika semina ya siku moja iliyofanyika katika ukumbi wa Maktaba kuu Mjini chake chake Pemba.  

Alisema kuwa, ipo haja ya kutoa elimu kwa wanawake ili kujua sheria za mitandao pamoja na kujua maana ya mamlaka ya mawasiliano Tanzania kwani wanawake wamekua wakifanyiwa makosa mengi katika mitandao ya kijamii.

Alieleza kuwa, pamoja na udhalilishaji wa wanawake unaofanywa katika mitandao lakini bado jamii imekua ikishindwa kujua sehemu sahihi za kuripoti makosa hayo.

“ Lengo ni kuwapa uelewa wanawake kuhusiana na mtandao wanapopata tatizo hasa katika mitandao ya kijamii hushindwa sehemu sahihi ya kulalamika kinachotakiwa ni kufika kwa mtoa huduma pia unaweza kufika katika ofisi zetu Chukwani Zanzibar” alisema.  

Hata hivyo aliwataka wanawake kutumia simu katika kuwaletea faida kwa kujitangaza mitandaoni kupitia biashara zao na sio kutumia kinyume na sheria.

Afisa Sheria mwandamizi wa Mamlaka ya Mawasailiano Tanzania TCRA Zanzibar Alhassan Mbwanga, alisema pamoja na sheria ya kumlinda mtumiaji, pia zinatoa adhabu kwa makosa yanayotokana na matumizi ya mabaya ya huduma na bidhaa za mawasiliano kama vile wizi, utapeli, vitisho, unyanyasaji na kutumia huduma kunyume cha sheria.

“Baadhi ya makosa na adhabu kama zilivo katika sheria ni pamoja na kifungo jela, faini au vyote kwa matumizi ya laini ya simu bila ya kuisajili mwenyewe” alisema.
Hata hivyo aliitaka jamii kuripoti makosa ya jinai yanapojitokeza katika mitandao katika vituo vya Polisi kwani makosa ya aina hiyo sio jukumu la Mamlaka ya Mawasiliano.

Kwa upande wake Injinia wa Mamlaka hiyo Zanzibar Mtende Hassan Mhandisi, alisema ni lazima kila mtumiaji wa mtandao kufuata sheria na haki zake ili kujiepusha na adhabu kali za makosa hayo.

Nao baadhi ya wajasiriamali hao ambao walipatiwa mafunzo hayo waliishukuru Mamlaka ya Mapato kwa kuwapa elimu ya mitandao ambayo walikua hawakuweza kuielewa hapo awali na kuwataka waendelee kutoa elimu kwa wengine ili jamii iweze kuelewa zaidi.

Comments

Popular posts from this blog

Wananchi wajenga wodi baada ya kuchoshwa na kujifungulia sakafuni

Sita wapotea katika mazingira tatanishi wilayani Wete

Jaji Mkuu Zanzibar awashukia mahakimu wanaonyanyasa watuhumiwa