Walimu wa Madrasa Pemba wahimizwa kusaidia jamii
Na, Zuhura Juma
Sauti ya Mnyonge, Pemba
WALIMU wa madrasa Kisiwani Pemba, wametakiwa kufanya kazi ya kuisaidia jamii katika kuendeleza Uislamu, sambamba na kuwa na Ikhlas, ili kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza.
Akizungumza na walimu hao, Ofisa Fatwa na utafiti wa mambo ya Kiislamu kutoka Ofisi ya Mufti Kisiwani Pemba, Said Ahmad Mohamed ,katika mkutano wa kuelimisha walimu wa madrasa kuhusu vitendo vya udhalilishaji vinavyofanyika katika jamii, uliofanyika katika shehia ya Kiungoni Wilaya ya Wete, alisema hawatofikia lengo iwapo walimu hao hawatokuwa na Ikhlas.
Alisema walimu wa madrasa ni kigezo cha kufikisha ujumbe kwa jamii na ndie anaefundisha Uislamu, hivyo waogope ubaya wa vitendo vya udhalilishaji duniani na akhera na waisaidie jamii katika kuamrishana mema, ili kuepusha madhara na athari ya vitendo hivyo.
“Mwalimu aepuke riyah, awe anamkusudia Allah anapofanya shughuli zake, pia Ikhlas ithubutu, ili kuepuka changamoto zote”, alisema Ofisa huyo.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati ya Ulamaa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Sheikh Jamal Mohame Abeid aliwataka walimu hao kuwa na hadhari ya hali ya juu kuhusiana na vitendo hivyo, kwani linapomfika mmoja wao linakuwa kubwa na kukuzwa, kwa vile wao ni watu mashuhuri na wanaoaminiwa katika jamii.
“Kwa kweli zinapotokea shutma hizi huwa ni aibu kubwa kwetu, hivyo tuache mambo yasio na msingi na tuwe karibu na Allah (Subuhanahu Wataala) ili atuepushe na tujitahidi kuielimisha jamii yetu juu ya madhara ya vitendo hivyo”, alisema Sheikh Jamal.
Nae, Ofisa Mipango kutoka Ofisi ya Kituo cha Huduma za Sheria Pemba, Siti Mohamed, aliwataka walimu kuzitii na kuzifuata sheria, ili kuepuka migogoro inayoweza kuepukika.
“Walimu wana nafasi kubwa ya kuelimisha sio kubomoa, hivyo waache kujihusisha na vitendo vya ukatili kwa watoto, kwani bado suala hili linaendelea kuiangamiza jamii”, alisema.
Mwalimu wa Madrasa ,Yussuf Khamis Ali, alisema kila mmoja achukue juhudi ya kumkumbusha mwenzake, ili waweze kuwaendeleza vijana katika kuupeleka mbele Uislamu.
Kwa upande wake ,Sheikh Mohamed Massoud Said, aliomba Ofisi ya Mufti madrasa zitambuliwe na walimu wachaguliwe na jamii, ili kuweza kupata walimu bora watakoendeleza dini ya kiislamu.
Mkutano huo wa siku moja uliowashirikisha walimu wa madrasa, ambao umeandaliwa na Ofisi ya Mufti Pemba, ukiwa na lengo la kuelimisha walimu hao juu ya kukemea na kuondosha vitendo vya udhalilishaji kwa watoto katika jamii.
Comments
Post a Comment