Waandishi wakana kuwa chanzo cha machafuko nchini

Na Haji Nassor
Sauti ya Mnyonge, Zanzibar

WAANDISHI wa habari nchini, wamesema wao sio chanzo cha migogoro na machafuko yanayojitokeza, kabla au baada ya kumalizika chaguzi, bali ni baadhi ya wanasiasa kushindwa kuwa na uvumilivu kisiasa.

Walisema kwa vile wapo baadhi wamekuwa ndio wamiliki wa vyombo vya habari, ndio wanaovitumia vibaya vyombo vya hivyi vya habari, na kueleza wapendavyo hata kama maelezo hayo, yanaashiria uvunjifu wa amani.

Wakizungumza kwenye mkutano wa siku mbili wa kuangalia masuala ya utawala bora, uchaguzi na demokrasia kwa nchi za Afrika, uliofanyika Kunduchi beach hotel jijini Dar-es Salaam, ulioandaliwa na shirika la Actionaid walisema wao wanafanyakazi zao kwa kufuata misingi na sheria.

Walisema wanasiasa, ambao baadhi wanamiliki vyombo vya habari wamekuwa wakisababisha machafuko na kisha mzigo huo kuelemezwa wanahabari, jambo ambalo sio sahihi.

Mwandishi wa habari Ghania Jumbe kutoka TBC, alisema hakuna mwandishi hata mmoja, anaependa kujitokeza kwa machafuko, hasa kwa vile hutumia uweledi wakati wanapotengeneza vipindi na habari zao.

Alisema suala la machafuko ndani ya nchi na hasa baada ya kumalizika kwa uchaguzi, limekuwa likichangiwa kwa kiasi kikubwa na wanasiasa, kwa kule kutoa matamshi yanayoelezea ukosefu wa utawala bora na utawala wa sheria.

Nae Kibwana Dachi wa Chanel Ten, alisema dhana ya kufinywa kwa demokrasia wakati mwengine, ndio inayoamsha ari na hisia nyengine tofauti kwa wafuasi wa vyama vya kisiasa nchini.

Suleiman Rashid Omar wa ITV/Redio One Pemba, alisema sio vema habari kuzifanya kama biashara, hasa kama zinaviashiria vya uchochezi kwa wananchi.

“Dhana ya kuwania soko la kihabari lisipewe kipaumbele hapa Tanzania, hata kama habari au vipindi hivyo vinapenda lazima kwanza tuangalie nchi kisha ndio habari,”alieleza.

Kwa upande wake Mkufunzi wa masuala la habari Valarie Msoka, alisema lazima waandishi wa habari wajiangalie mara mbili wanapoandika habari  zao, ili kuibakisha salama Tanzania.

Alieleza kuwa, sheria kanuni na misingi ya kihabari inatakiwa ifuatwe wakati wote, kwa vile nchi inapoelekea uchaguzi au baada ya kumalizika, huwa katika kipindi kizito kwa walioshindwa.

“Kila mfuasi wa chama ambae chama chake hakikushika hatamu, huwa na mtazamo mwengine kwa chama kilichoshinda, sasa kama waandishi wakiandika habari za upande mmoja, lolote linaweza kujitokeza,”alieleza.

Mapema Kalore Kadege kutoka Actionaid, alisema lazima waandishi wa habari wawasaidie wananchi, pale serikali inapotoa matamko ya kufuta mfano wa michango ya skuli au pungozo la kodi.

Mafunzo hayo ya siku mbili, ambayo yamewashirikisha waandishi wa habari wapatao 20 kutoka Tanzania bara na Zanzibar, yaliandaliwa na Actionaid, yakilenga kuangalia dekorasia kwa nchi za Afrika.

Comments

Popular posts from this blog

Wananchi wajenga wodi baada ya kuchoshwa na kujifungulia sakafuni

Sita wapotea katika mazingira tatanishi wilayani Wete

Jaji Mkuu Zanzibar awashukia mahakimu wanaonyanyasa watuhumiwa