Mkuu wa mkoa ataka madarasa kusakafiwa ili kuepusha vumbi kwa wanafunzi
Na, Haji Nassor
Sauti ya Mnyonge, Pemba
MKUU wa Mkoa wa kusini Pemba, Hemed Suleiman Abdalla ameliharakisha Baraza la mji wa Chakechake, kuweka saruji chini, kwenye vyumba vinne vya madarasa ya skuli ya msingi Mgelema, ili kuwaepusha na vumbi wanafunzi wanaoyatumia madarasa hayo.
Alisema elimu bora haitafutwi kwa mtindo wa wanafunzi kukaa kwenye vumbi, jambo ambalo wanaweza kukosa elimu na hata kupata athari za kiafya kama wakiendelea kuyatumia madarasa hayo.
Mkuu huyo wa Mkoa ameeleza hayo skulini hapo, alipokuwa akizungumza na wananchi, waalimu na kamati za wazee wa skuli hiyo, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku moja ya kuikagua miradi nane ya maendeleo, inayoendeshwa na Baraza la mji wa Chakechake.
Alisema, lazima juhudi za haraka zichukuliwe na baraza la mji kwa kushirikiana na Kamati husika ya skuli hiyo, ili kuharakisha uwekaji wa saruji, maana wanafunzi wa madarasa ya pili wanaotumia, wanaendelea kuathirika kwa vumbi.
Alieleza kuwa, hakuna namna bali ndani ya wiki zisizodi tatu, iwe tayari hali hiyo imeshakaa vyema, ili wanafunzi wapate fursa ya kupata haki yao ya elimu, wakiwa katika mazingira salama.
“Hali ya madarasa yale nilioyatembelea kwa kweli hairidhishi, na ni lazima kwa uongozi wa baraza la mji, kamati ya skuli na wananchi wa Mgelema washirikiane vyema, ili litiwe saruji kwa haraka,”alisema,
Mwalimu Mkuu wa skuli hiyo Mohamed Issa, alisema tayari waanchi kwa kushirikiana na uongozi wa skuli, wameshajipanga na ndani ya wiki moja, tayari itakuwa limeshajazwa kifusi.
“Tayari wananchi kwa kushirikiana na sisi, tumeshajipanga na ndani ya wiki moja, itakuwa tumeshakweka kifusi kwa ajili ya utiaji wa lami.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa akikagua ujenzi wa vyoo sita kwa ajili ya wananchi wa shehia ya Mjini Ole, na ametoa wiki mbili kwa Baraza la mji wa Chakechake, kukamilisha ujenzi huo, ili wananchi waanze kuvitumia.
Alisema mvua za masika tayari zimeshaanza na ndio ambazo mara nyingi, husababisha magonjwa ya aina mbali mbali kama vile kipundu pindu, hivyo ni nafasi ya kwa Baraza la mji kukamilisha kazi hiyo.
Wakati huo huo akizungumza kwenye kikao cha majumuisho kilichofanyika Machomane, Mkuu huyo wa Mkoa wa kusini Pemba, alilipongeza baraza la Mji wa Chakechake kwa kazi wanayoifanya ya kuwahudumia wananchi.
Alisema baraza hilo, limekuwa kiungo kikubwa katika kuwaletea maendeleo wananchi kwa mtindo wa kuitekeleza Ilani ya Chama, bila ya ubaguzi wowote.
Hata hivyo aliipongeza kamati ya wazazi ya skuli ya Furaha kwa hatua ya kusaidia kwa kiwango kikubwa, hadi kukamilishwa kwa ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa.
Mapema Mkurugenzi wa baraza la mji wa Chakechake Nassor Suleiman Zaharan, alisema wamekuwa wakizihama ofisi na kwenda kwa wananchi, ili kusikiliza shida zao na kuzitelekeza.
Alisema ushirikiano wanaoupata huwapa nguvu na ari ya utendaji wao wa kazi, jambo ambalo husabisha miradi kadhaa wanayofanya kufanikiwa.
Kwa upande wake Diwani wa wadi Ole, Khadija Henock Maziku alilipongeza baraza la mji kwa kukubali ombi lake la ujenzi wa vyoo vya jamii shehia ya mjini Ole.
Miradi iliotembelewa na Mkuu huyo wa Mkoa pamoja na Katibu tawala wake ni ujenzi wa egesho kuu la gari za abiria Tibirinzi, ujenzi wa vyumba vya madarasa Mgelema, Furaha, mradi wa maji safi na salama hospitali ya Shungi na matengenezo ya hospitali ya Tundaua.
Comments
Post a Comment