Ahadi za JPM ujenzi wa barabara Manyara, zaanza kutekelezwa
Na Joseph Lyimo
Sauti ya Mnyonge, Manyara
Ahadi za ujenzi wa barabara zilizotolewa na Rais John Magufuli wakati wa kampeni ya kugombea urais mwaka 2015 alipotembelea Mkoani Manyara, zipo kwenye mchakato wa utekelezaji wake.
Pia, utekelezaji wa miradi ya barabara za mkoa huo zilizopo kwenye ilani ya uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa mwaka 2015/2020 unafanyiwa kazi.
Meneja wa wakala wa barabara nchini Tanroads mkoani Manyara, mhandisi Bashiri Rwesingisa aliyasema hayo kwenye kikao cha bodi ya barabara ya mkoa huo, kilichofanyika juzi mjini Babati.
Mhandisi Rwesingisa alisema barabara ya Arusha-Kibaya-Kongwa, yenye urefu wa kilometa 336.6 inayopitia Losinyai wilayani Simanjiro na Dosidosi wilayani Kiteto, inafanyiwa upembuzi na usanifu wa kina.
Alisema kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina inaendelea kutekelezwa na mhandisi mshauri M/S Cheil Engeneering co Ltd ya Korea kaskazini na M/S Inter-consult Ltd ya Tanzania.
Alisema barabara ya Karatu-Mbulu-Haydom-Singida ya urefu wa kilometa 190 inafanyiwa upembuzi na usanifu wa kina kupitia mhandisi mshauri M/S H.P. Gauff Ingenieure akishirikiana na wenzake watatu.
Alisema Tanroads imeingia mkataba na mkandarasi M/S China Railway Seventh Group kwa gharama ya sh12.6 bilioni ajili ya ujenzi wa daraja la Magara linalounganisha wilaya za Babati na Mbulu.
"Pia kazi ya upembuzi na usanifu umefanyika kwa barabara ya barabara ya Handeni-Kiberashi-Kondoa-Singida ya kilometa 460 ambapo kilometa 120 zitakuwa kati ya Kiberashi na Olboloit, Wilayani Kiteto," alisema mhandisi Rwesingisa.
Awali, mbunge wa jimbo la Mbulu Vijijini, Flatei Massay akizungumza juu ya ahadi hizo za Rais Magufuli za ujenzi wa barabara za lami, alisema bado utekelezaji haujafanyika kwenye barabara ya Haydom kilometa tano na Dongobesh kilometa tano.
Mbunge wa jimbo la Mbulu mjini Paul Isaay alisema ahadi ya Rais ya kilometa tano za barabara za mji wa Mbulu bado haujatekelezwa na pia barabara ya mlima Magara bado ina changamoto kubwa.
Mbunge wa Babati mjini Pauline Gekul alisema Rais Magufuli alitoa ahadi akiwa uwanja wa Kwaraa kuwa zitajengwa kilometa 20 za lami, hivyo utekelezaji unapaswa kufanyika.
Mbunge wa jimbo la Simanjiro James Ole Millya alisema Rais mstaafu Jakaya Kikwete aliagiza barabara za makao makuu yote ya wilaya nchini iwekwe lami lakini Orkesumet hadi sasa haina hata kipande cha lami.
Hata hivyo, mkuu wa mkoa huo, Alexander Mnyeti alisema atahakikisha anasimamia ahadi zote zilizotolewa kwa nyakati tofauti na viongozi hao wawili wakuu wa nchi zinatekelezwa kwa wakati.
"Najua utekelezaji ukifanyika ipasavyo mwaka 2020 tukienda kwa wananchi ni hiyena hiyena tunachukua nchi na wengine tunaendelea kuwa wakuu wa mikoa," alisema Mnyeti.
Comments
Post a Comment