Wenye matatizo ya uzazi wataka Mbunge awasaidie kupata wataalamu wa tatizo linalowakabili
Na, Florence Sanawa
Sauti ya Mnyonge, Mtwara
WANAWAKE wa Kijiji cha Mkahara Halmashauri ya Mji Nanyamba wamemuomba Mbunge wa Jimbo hilo Abdallah Chikota (CCM) kuwatafutia wataalam wa afya ili kuwapatia ufumbuzi wa tatizo la ugumba linalowakabili kwa miaka mingi.
Akizungumza kwa niaba ya wanawake wenzie Salma Dosi Mkazi wa Kijiji cha Mkahara alisema kuwa tatizo hilo limekuwa likitafutiwa ufumbuzi kwa muda mrefu baada ya kupata malalamiko hayo kutoka kwa wanawake ambao hawajabahatika kupata ujauzito hivyo kuhisi kuwa ni wagumba.
Alisema kuwa wanawake hao wamekuwa wakitoa malalamiko yao kwa viongozi mbalimbali wanaofika kutembelea katika kijiji hicho ambacho kipo katika Halmashauri ya Mji Nanyamba.
“Hawa wanawake wanaumia kukosa watoto ndio maana wamekuwa wawazi ili waweze kupata ufumbuzi wa tatizo linalowakabili kwa muda mrefu sio hawa watano tu wapo wengi hawa ni wawakilishi tu wa wenzao tungependa kujua tatizo hasa nini kinachopelekea wanawake wengi kuwa wagumba katika kijiji hichi” alisema Dosi
Blogi hii ilifanya jitihada za kuwatafuta watalaam na kufanikiwa kukutana na mtalaamu wa magonjwa ya wanawake Kelvin Nandonde ambapo anasema kuwa tatizo la ugumba halipaswi kuangaliwa kwa upande mmoja wa mwanamke tu huenda tatizo hilo lipo pia kwa wanaume.
"Ingawa kitendo cha kuziba kwa mirija ama kupata uvimbe kwenye shingo ya kizazi na shida ya mfuko wa uzazi pia vinaweza kuchangia kwa mwanamke kuwa mgumba lakini pia yapo mambo ambayo yanaweza yakachangia wanaume kushindwa kumbebesha mwanamke mimba kwa suala la huko mkahara inabidi uchunguzi ufanyike tujue tatizo hasa liko kwa akina nani ili kupata ufumbuzi zaidi" alisema Nandonde
Comments
Post a Comment