Wananchi watakiwa kufika mahakamani kusaidia kutoa ushahidi

Na Haji Nassor, 
Sauti ya Mnyonge, Pemba

MRAJISI wa mahakama kuu jimbo Pemba Hussein Makame Hussein
MRAJISI wa Mahakama kuu jimbo Pemba, Hussein Makame Hussein, amesema ili mtenda kosa aweze kutiwa hatiani,  suala la jamii kufika mahakamani kutoa ushadi, ni moja ya njia ya kuishahiwisha mahakama kufikia hatua hiyo.

Alisema sio kweli kuwa, mwenye uwezo wa kifedha ndie anaeshinda kesi, kama baadhi ya dhana za watu zilivyo, bali kila shauri linalofikishwa mahakamani, ushahidi ndio kigezo cha hukumu.

Mrajisi huyo, alieleza hayo jana skuli ya ufundi Kengeja wilaya ya Mkoani, alipokuwa akizungumza na waalimu na wanafunzi wa skuli hiyo, akiwa na kamati yake ya maandalizi ya siku ya sheria Zanzibar.

Alisema yanapofanyika matendo kama ya jinai au madai, mahakimu na majaji huwa hawapo, hivyo mashauri hayo yanapofikishwa mbele yao, wa kuyatolea  maelezo ni mashuhda, na kisha kuiachia mahakama kufanya uamuzi.

Katika hatua nyengine, Mrajisi huyo ambae pia ndie Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya sherehe ya siku ya sheria Zanzibar, alieleza kuwa uwepo wa dhana kuwa mwenye fedha ndio pekee anaeweza kushinda kesi sio sahihi.

“Mahakamani hakuendeshwi kesi kwa alienacho kwamba lazima ashinde, bali ushahidi ndio unaotazamwa mbele ya mahakama na sio jambo jengine lolote”,alifafanua.

Katika hatua  nyengine Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Maandalizi ya siku ya sheria Zanzubar kisiwani humo, alisema tayari matayarisho yote kwa ajili ya sherehe hizo zimekamilika.

Kwa upande wake Mjumbe wa kamati hiyo ambae ni Mratibu wa Kituo ch a Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC tawi la Pemba, Fatma Khamis Hemed, alisema kituo hicho kipo kwa ajili ya kutoa msaada na ushauri wa kisheria bila ya malipo.

Hivyo amewataka wanafunzi na waalimu hao, kukitumia ili wajifunze sheria mbali mbali, kwa ajili ya kujua haki na wajibu wao kwa taifa.

“Kwa vile kutokujua sheria sio kinga mbele ya mahakama kwa aliefanya kosa, sasa njooni kwenye kituo chetu, mjisomee na masuala ya kisheria au mpate ushauri na maelekezo, ili mujikinge na kujiingiza kwenye makosa yasiokuwa ya lazima”,alisema.

Katibu wa Kamati hiyo Ali Haidari Mohamed, aliwataka wanafunzi hao, kujikita kwenye kusoma ili watimize malengo yao ya baadae.

Wakili wa kujitegema wa mahakama kuu, kisiwani Pemba Zaharan Mohamed Yussuf, aliwatahadharisha wanafunzi hao, kwamba, sasa kisiwani Pemba, ipo mahakama ya watoto, hivyo wanaweza kufikishwa mahakamani kama wakifanya kosa.

Alisema, lazima wajiweke kwenye kufuata maadili na maagizo mema, na wajikinge na mambo maovu ambayo yanaweza kuwafikisha mbele ya mahakama.

MKUU wa Mkoa wa kusini Pemba Mhe: Hemed Suleiman Abdalla
Hakimu wa mahakama ya ardhi Chakechake Salum Hassan Bakar, aliwataka wanafunzi na waalimu hao, kuwa makini na ununuzi wa ardhi, kutokana na kujaa matapeli wa rasilimali hiyo.

“Kesi kadhaa zinazoletwa mahakamani hivi sasa zinahusu, utapeli wa uuzaji wa ardhi mara mbili au zaidi, na nyengine ni kuhusu mipaka, hivyo lazima jamii iwe makini, ili wajitumbuikize kwenye migogoro isiokuwa ya lazima,”alifafanua. 

Baadhi ya wanafunzi wa skuli hiyo, walisema bado elimu inahitajika zaidi, ili wananchi wapate taaluma ya mambo ya kisheria, ili wajue na haki na wajibu wao.

Siku ya sheria Zanzibar inatarajiwa kuadhimishwa Febuari 12, uwanja wa Tenis Chakechake kisiwani Pemba, na shamra shamra zake zilianza Febuari 5 kwa shughuli mbali mbali, ikiwa ni pamoja na matembezi ya chuo cha mafunzo Wete na mkutano na wadau.

Comments

Popular posts from this blog

Wananchi wajenga wodi baada ya kuchoshwa na kujifungulia sakafuni

Sita wapotea katika mazingira tatanishi wilayani Wete

Jaji Mkuu Zanzibar awashukia mahakimu wanaonyanyasa watuhumiwa