Polisi Zanzibar wamsaka mama aliyetelekeza kichanga benchi la wagonjwa hospitalini

Na Haji Nassor, 
Sauti ya Mnyonge, Pemba

JESHI la Polisi Mkoa wa kusini Pemba, limesema linaendelea kuweka mitego ya aina mbali mbali, ili kumnasa mama mzazi aliemtelekeza mtoto wake mchanga wa siku moja, kwenye mvungu wa bao la kukalia ndani ya hospitali ya Chambani wilaya ya Mkoani wiki iliopita.

Jeshi hilo limesema tayari limefanya uchunguuzi wa shehoa kadhaa kisiwani Pemba na hata kuwatumia baadhi ya masheha, ili kuulizia iwapo  kuna mzazi aliejifungua na kisha mtoto kutoonekana.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu, Kamanda huyo wa Polisi mkoani humo Shehan Mohamed Shehan alisema, bado jeshi lake halijakata tamaa juu ya kumpata mama huyo, na ndio maana linaendelea na uchunguuzi.

Alisema, wanaweka mitego kwenye vijiji, mitaa, shehia a wilaya mbali mbali, kwa lengo la kujua habari zake na akipatikana ,baada ya kuhojiwa atafikishwa mbele ya vyombo vya sheria kujibu shitaka lake.

Hivyo, ameitaka jamii kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi na wasisite kutoa taarifa wakati wowote, iwapo watapata taarifa za mama huyo aliemtelekeza mwanawe.

“Jeshi la Polisi, bado liko mafichoni likiendelea kumsaka na kumtegea mitego mbali mbali mama huyo, lakini lazima jamii na makundi yote ya watu, washirikiane na sisi, ili kutimiza malengo yetu,”alisema Kamanda huyo.

Katika hatua nyengine Kamanda huyo wa Polisi Mkoa wa kusini Pemba, amewataka wazazi na walezi wanapokuwa na vijana wao wenye ujazito kila zikikaribia siku za kujifungua kuwa nao karibu.

Baadhi ya wananchi walioshuhudia tukio hilo, walisema wakati wanasubiri huduma kwenda kwa daktari kwa ajili ya kupata huduma, ndipo waliposikia sauti ya mtoto mchanga.

Walisema, baada ya hapo walichungulia mvunguni mwa benchi waliokua wamekaa, ndipo walipomuona mtoto huyo, akiwa amevungwa kanga na kuchukuliwa na madaktari kwa uchunguuzi.

Kwa sasa tayari mtoto huyo ameshapelekwa Unguja kwenye kituo cha kulelea watoto, ingawa awali walijitokeza wasamaria wema aidi ya 10 wakiomba kupatiwa mtoto huyo.

Comments

Popular posts from this blog

Wananchi wajenga wodi baada ya kuchoshwa na kujifungulia sakafuni

Sita wapotea katika mazingira tatanishi wilayani Wete

Jaji Mkuu Zanzibar awashukia mahakimu wanaonyanyasa watuhumiwa