Mzigo wenye utata wasababisha meli ya uvuvi ya Malaysia kutozwa faini

Na Florence Sanawa
Sauti ya Mnyonge, Mtwara

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ameitoza faini meli ya uvuvi ya Kampuni ya Buah Naga 1 ya nchini Malaysia na kuitoza faini ya Dola za kimarekani 350,000 sawa na shilingi milioni 770 kwa kosa la kukutwa na mapezi ya samaki aina ya papa yenye uzito wa Kilo 90 bila miili yake.

Kauli hiyo ameitoa leo mkoani mtwara baada ya kufanya ziara ya siku moja ambapo ilibainika kuwa meli hiyo imevunja sheria kinyume cha Kanuni ya 66 ya kanuni za Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu pamoja na kifungu cha18 (2) cha Sheria ya Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu ya mwaka 1998 na marekebisho yake ya mwaka 2007.

Alisema kuwa meli hiyo ilikamatwa Januari 26 mwaka huu baada ya kufanyika ukaguzi uliosimamiwa na kikosi maalum cha kupambana na kudhibiti uvuvi haramu na utoroshaji wa samaki na mazao yake wakati ikifanya shughuli za uvuvi katika ukanda wa Bahari Kuu kati ya Mkoa wa Lindi na Mtwara.

Mpina alisema kuwa pamoja na kukutwa na mapezi hayo ya papa meli hiyo ilikutwa pia na bastola aina ya Bereta ikiwa na risasi 10 bila ya kuwa na nyaraka za umiliki wake.

Aidha Mpina ameagiza fedha hizo zilipwe ndani ya siku saba huku akitoa onyo kali kwa wamiliki wa meli waliopewa leseni za uvuvi wa bahari kuu kufuata masharti vibali vyao na kwamba katika zama hizi za utawala wa Rais Dk John Magufuli watachukuliwa hatua kali zaidi.

“Unajua hizi meli zimekuwa zikitumika vibaya ikiwemo kufadhili biashara nyingine haramu ikiwemo kusafirisha dawa za kulevya ,usafirishaji haramu wa  binadamu pamoja na biashara ya silaha huku zikitumika pia kutorosha nyara za Serikali ikiwemo meno ya tembo, samaki na madini serikali ya awamu ya tano haitavumilia hilo” alisema Mpina

“Hata hiki kitendo cha wamiliki wa meli hiyo kuwakata samaki hao mapezi na kisha kutupa miili yao baharini kimeleta athari kubwa kwa Taifa kwani samaki hao wangeweza kutumika kwa matumizi mengine ya binadamu na kuchochea uchumi wa nchi ndio maana  samaki wasioruhusiwa tumeruhusu wataifishwe na kugawiwa kwa wananchi wa maeneo jirani ya Manispaa ya Mtwara”

Nae Kamishna wa Oparesheni wa Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na Dawa za kulevya, Luteni Kanali Fredrick Milanzi alisema meli hiyo baada ya kukaguliwa imekutwa na mapezi kilo 90 ya samaki aina ya papa pamoja na bastola yenye risasi 10 ambayo inaendelea kushikiliwa na Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Mtwara hadi hati za umiliki zitakapowasilishwa.

Pia mwenye meli atatakiwa kuhakikisha anawasafirisha mabaharia kurudi nchi zao kwa madai hawataki kuendelea kufanya kazi kutokana na kukiukwa kwa mikataba yao ya kazi.

Aidha samaki wasioruhusiwa kuvuliwa kwa mujibu wa leseni ya uvuvi iliyopewa meli hiyo ( Bychatch) watabaki kuwa ni wa Tanzania na watauzwa kwa mnada na fedha zitakazopatikana kiasi cha sh milioni 12 zitaingizwa kwenye Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu (DSFA).

Comments

Popular posts from this blog

Sera ya Viwanda iendane na mabadiliko ya soko la wakulima

Ziara ya Jaji Mkuu Zanzibar mhe. Omar Othman Makungu katika picha

Mrajisi ataka wananchi kufika mahakamani kutoa ushahidi