Mkuu wa Mkoa Manyara, ataka mahakimu kuwajali wanyonge
Na, Joseph Lyimo,
Sauti ya Mnyonge, Simanjiro
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti amewataka mahakimu wa mkoa huo kutekeleza wajibu wao ipasavyo wakati wanaposikiliza kesi na kutoa hukumu kwa haki ili kuepuka malalamiko yanayotolewa na wananchi wanyonge.
Akizungumza kwenye ziara yake wilaya ya Simanjiro, Mnyeti alisema kupitia nafasi yake ya Mwenyekiti wa kamati ya maadili, hatakubali kuona wananchi wanalalamikia kukosa haki.
Mnyeti alisema baadhi ya mahakimu wanajigeuza kuwa miungu watu na kushindwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo hivyo kusababisha malalamiko kwa wananchi wanyonge.
"Hatuwezi kukubali kuona mambo kama hayo, yakifanyika kama kuna mtu anaona kuna mahakimu siyo wahadilifu wanakula rushwa na kushindwa kutoa haki nijulisheni," alisema Mnyeti.
Alisema hatakubaliana na kitendo cha wananchi wake wanyonge kulalamikia kunyanyaswa na mahakimu, kwani hakuna mtu aliyekuwa juu ya sheria na kuwanyanyasa.
"Hii hali sitaikubali kwani sisi tumepewa dhamana ya kuwatumikia wananchi hasa wanyonge, haiwezekani polisi wafanye kazi yao vizuri ya kuwakamata wahalifu kisha wengine wanapokea rushwa bila kutenda haki," alisema Mnyeti.
Awali, mkazi mnyonge wa mtaa wa Njiro, Theopista Paulo alisema amekuwa akinyanyasika wakati akidai haki yake.
Theopista alisema mmoja kati ya mahakimu wa eneo hilo alikuwa anamwambia hata kama akimkataa na kesi yake kuhamishwa kwenye mahakama nyingine hawezi kushinda chochote.
Hata hivyo, Mwanasheria wa ofisi ya mkuu wa mkoa huo, Peter Mangala alisema mwananchi yeyote ana haki ya kumkataa hakimu endapo atakuwa na sababu za msingi.
Mangala alisema endapo mwananchi akiwa na hoja za msingi anazozipinga anaweza kumkataa jaji au Hakimu atakapobaini kuwa hawezi kutendewa haki.

Comments
Post a Comment