Lions Club na Kanisa Katoliki wasaidia matibabu kwa wanyonge wilayani Babati
Na, Joseph Lyimo
Sauti ya Mnyonge, Arusha
Wananchi wanyonge 744 wa Wilaya ya Babati Mkoani Manyara, wamepatiwa huduma ya vipimo vya macho, kisukari na shinikizo la damu, kwa muda wa siku mbili kwenye kituo cha afya Magugu.
Mbunge wa jimbo la Babati vijijini, Vrajilal Jituson akizungumza kwenye kituo cha afya Magugu, alisema huduma hiyo imeletwa kwa ushirikiano na madaktari wa hospitali ya Kanisa Katoliki ya St Magreth ya jijini Arusha na Lions Club.
Jituson alisema huduma hizo zilitolewa bila wananchi hao wanyonge kuchangia fedha, ambapo wagonjwa 54 watafanyiwa upasuaji na 36 watasubiri hadi mwezi wa tatu.
Alisema hao wanyonge 36 watasubiri hadi mwezi Machi ili waende kufanyiwa upasuaji kwenye hospitali ya mji wa Babati (Mrara) kwani tatizo lao la mtoto wa jicho halijafikia hatua ya upasuaji.
"Wataalamu hao wa afya kutoka hospitali ya St Magreth na Lions Club pamoja na kutoa huduma ya upimaji macho, pia walitoa elimu juu ya kisukari na shinikizo la damu ," alisema Jituson.
Alisema mara baada ya kufanyika kwa vipimo hivyo, wataalamu hao wamebaini kuwa baadhi ya vijana wadogo wa eneo hilo, wana tatizo la ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu.
Alisema vijana hao walipatiwa elimu ya namna ya kuishi na kuepukana na magonjwa hayo ya kisukari na shinikizo la damu kwani siyo maradhi ya kurithi.
Mmoja kati ya mgonjwa mnyonge aliyefanyiwa vipimo vya macho, Husna Ramadhani alishukuru kutolewa huduma hiyo kwani yeye asingeweza kusafiri hadi jijini Arusha kwa ajili ya kupata huduma hiyo kutokana na ukata.
"Sisi wanyonge tusiokuwa na uwezo wa fedha tunashukuru sana kwa watoa huduma na mbunge wetu Jituson kwani kwa muda mrefu tumekuwa tunapata huduma hii bila kulipia chochote, tunaomba waendelee hivi," alisema Ramadhani.
Mnyonge mwingine John Mosses alisema kuna wagonjwa wengi wamefanyiwa vipimo kwa gharama ambazo wasingeweza kutimiza kutokana na kipato chao kidogo ila sababu ya huduma hiyo ya bila malipo wamefanikiwa.
"Wanyonge wengi wamefaidika kupitia huduma hii, kwani hawajatoa fedha lakini wamepatiwa vipimo kwa wataalamu waliobobea, tunashukuru mno kwa wote waliofanikisha tukio hilo," alisema Mosses.



Comments
Post a Comment