Kiwango kidogo cha ufaulu wa mitihani chamtia wasi wasi mkuu wa mkoa



MKUU wa Mkoa wa kusini Pemba, Hemed Suleiman Abdall amesema, amekiri kutoamini sababu ya wilaya ya Mkoani kutofanya vyema kwenye mitihani ya taifa kwamba  kumechangiwa na uhaba wa waalimu, bali ana mashaka na hamu na ari ya ufundishaji wa baadhi ya waalimu hao.
Alisema anashangaa kuona baadhi ya skuli kama Mizingani sekondari na nyengine pana masomo hayana waalimu, ingawa ufuaulu wake ni mkubwa ukilinganishwa na yale masomo kama ya dini, Kiswahili na kiarabu ambayo yanawaalimu wa kutosha lakini ufaulu wake ni mbovu,
Mkuu huyo wa Mkoa, ameeleza hayo skuli ya Mohamed Juma Pindua, alipokuwa akizungumza na waalimu wakuu, wa msingi, sekondari na wenyeviti wa kamati zao, kwenye mkutano wa kutathimi, kufuatia wilaya hiyo kutofanya vyema kwenye mitihani ya taifa iliopita.
Alisema, yeye binafsi anamashaka na aria na hamu ya waalimu iwapo wanajua wanchokifanya wanapokuwa  madarasani bali kuna jambo jengine, ambalo lilisababisha ubovu wa matokeo hayo ya taifa na sio uhaba wa waalimu pekee.
Mhe Hemed alieleza kuwa, baada ya matokeo ambayo yalimshitu sana, aliomba idadi ya waalimu na viwango vyao ya elimu, alishangaa baada ya kuona idadi kubwa ya waalimu wenye shahada ya kwanza na ya pili, ingawa alipopekua kuangalia masomo wanayoyasomesha yameanguka.
Aliongeza kuwa, yeye mashaka yake zaidi kwamba iwapo hao wanaokwenda vyuoni  na kurudi na shahada, na kama wapefaulu vyema na wako tayari kwa ajili ya kazi ya kufundisha au kama ni kwa ajili ya kuongezea mshahara.
“Mimi waalimu nimewasikia kuwa, uhaba wa waalimu ndio miongoni mwa tatizo, lakini mbona yapo masomo yana waalimu kamili, yameshindwa kuibuka na ushindi, lazima tujithamini kwa hili,”alieleza,
Katika hatua nyengine, Mkuu huyo wa Mkoa, aliwataka waalimu wakuu ambao hawako tayari kubadilika wajiondoe mapema kwenye nafasi zao, na kuwapisha wengine.
Alisema anawasiwasi  kuona mwalimu mkuu anakuwa na nafasi hiyo kwa muda wa miaka zaidi ya saba au nane kwenye skuli kama msingi, lakini hana kumbu kumbu ya kupasisha michepuo kwa madarasa husika.
Hata hivyo alisema, lazima kwa wenyeviti hao wa kamati, wabuni mbinu na mikakati kambambe ili kuhakikisha wanakuwa bega kwa bega na wazazi, kuona ufaulu wa wanafunzi unaongezeka.
Mapema Kaimu Afisa Elimu wilaya ya Mkoani Nassor Hakim alisema changamoto kubwa hasa inayokabili kwa skuli kadhaa ni uhaba wa waalimu hasa wa sayansi na kusababisha wilaya hiyo kutofanya vibaya.
Alisema jambo jengine, ambalo linawakabili ni wazazi na walezi kutowaunga mkono waalimu katika usomeshaji, na kusababisha utoro mkubwa hasa kwa yale madarasa yenye mitihani.
Afisa elimu Mkoa wa kusini Pemba mwalimu Haji Kombo, alisema lazima waalimu kwa kushirikiane na kamati za wazazi wabuni mbinu nzito, ili kuwapata wanafunzi na kuwasomesha.
Hata hivyo Mwenyekiti wa kamati ya wazazi skuli ya Wambaa sekondari Abdalla Salum Juma, alisema wapo baadhi ya waalimu wamekuwa watoro skulini.
“Mwalimu anaingia darasani saa 9:00 jioni na akifika hana mkao anataka kurudi, au mapaka tarehe ya jana yapo masomo hayajasomeshwa hata siku moja na mwalimu yupo, sasa nao waalimu lazima wajielewa wanafanya nini,”alieleza.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu skuli ya msingi Mtangani Mohamed Rashid, alisema ushirikiano mbovu uliopo baina ya waalimu na wazazi unaweza kupelekea skuli hiyo kukosa maendeleo kwa muda mrefu.
Mapema Mkurugenzi wa Baraza la Mji Mkoani Abdalla Rashid, aliuahidi uongozi wa skuli ya Kengeja, kuwaongezea nguvu, ili kukamilisha ujenzi wa skuli yao.
Wilaya ya Mkoani Pemba kwenye matokeo ya mitihani ya taifa yaliotoka hivi karibu, kati ya skuli 10 zilizofanya vibaya kitaifa ilikuwepo skuli ya Chokochoko, huku kwa darasa la nne skuli chambani ilishika mkia, sawa na Mtangani ilioshika nafasi ya pili kutoka mwisho kwa dara la sita.

Comments

Popular posts from this blog

Wananchi wajenga wodi baada ya kuchoshwa na kujifungulia sakafuni

Sita wapotea katika mazingira tatanishi wilayani Wete

Jaji Mkuu Zanzibar awashukia mahakimu wanaonyanyasa watuhumiwa