Kama baba anaweza kubaka mwanawe usalama wa watoto upo wapi?

Imeandaliwa na Zuhura Jumaa
Sauti ya Mnyonge, Pemba

Kwa kawaida mtoto akiumia, anapoona ameonewa au akitaka kitu hukimbilia kwa mzazi au yule anayehisi yupo karibu naye.

WARATIBU wa wanawake na watoto wa shehia sita za wilaya ya Wete, masheha pamoja na wadau wengine wakiwa  katika moja ya mkutano wa kupinga vitendo vya udhalilsihaji  dhidi ya wanawake na watoto, uliofanyika uwanja wa Gombani
Ni kwa mzazi ndipo anapoamini upo usalama wake na kupata mahitaji yake na mzazi hutarajiwa kuonyesha malezi mazuri na kumpatia mtoto anachostahili.

Lakini baadhi ya hao waliopewa utukufu uliotukuka wa kuitwa watoto wa Adam na Hawa (binaadamu) sifa hii ya utu haipo na hufanya mambo zaidi ya wanyama.

Hali hii ndio iliopelekea mtu anayefanya ushenzi au ujahili wa aina moja au nyengne kuitwa mnyama.

Hivi karibuni tumesikia mambo ya kinyama yakifanywa sehemu mbali mbali za Unguja na Pemba na baadhi ya matukio kuwashitua watu na hata kutoamini waliyoyasikia.
Katika orodha ya mtukio ya aina hii ni lile la kijiji cha Kiungoni, wilaya ya Wete, Pemba.

Kwa lengo la kujuwa kilichotokea, nilifika kijijini kama saa 5:00  asubuhi , ukimya ulitawala na juu ya miti nilisikia sauti za ndege, hasa kunguru na kwa mbali mlio wa ng’ombe.

Nilifika katika nyumba ya mama niliyetaka kumuona, ili anielezee tukio liliotikisa visiwa vyetu na hasa kijiji hicho.

Nilimkuta huyo mama  wa  miaka 39 akiwa na kitoto  cha miezi miwili mikononi akimbembeleza kwa wimbo wa kizamani wa…Njuguni rembwe, alienyuma atangulia mbele wa usoni twende.

Nilivutiwa na nyimbo, lakini niliona bora nimkatize ili kumueleza kilinichonifikisha nyumbani kwake.

Nilimjulia hali na alinikaribisha ndani kwa unyonge, kukaa juu ya mkeka wa ukili alioukunuta vumbi.

Baadhi ya mambo aliyonieleza naona aibu kusimulia, lakini kwa ufupi aliniambia mumewe alimsaliti yeye na Mola, kwa kufanya mambo ambayo mtoto wa Adam na Hawa na hasa muumini wa dini ya Kiislamu hatarajiwi kuyafanya.

Aliniambia, mume wake wa ndoa alifanya unyama wa kuwabaka watoto wake watatu aliozaa na mume mwengine.

Alipokuwa anaelezea alinimaliza nguvu na kunikumbusha hadithi za zama za ujahilia, Nilibaki kutikisa kichwa na kusema…Yaa rabi... Yaa rabi…

Aliniambia, mmoja wa watoto watatu wa kike aliowabaka, ambaye alikuwa na miaka 16 alikuwa mjamzito, wengine ni miaka 15 na miaka minane (8).

Nikiwa siamini niliosimuliwa na kuweka ushungi wangu ulioporomoka nilipotikisa kichwa, mtoto mwenye mimba ya baba wa kambo alikuja kukichukua kile kichanga kiliokuwa kinabembelezwa na mama yake.

“Unamuona huyu ndiye aliyepewa mimba na mume wangu ambaye ni baba yake wa kambo”, alisema kwa masikitiko mama huyo. 

“Wallahi sina pa kuuficha uso wangu, aibu tupu…hii ni laana, sina nguvu ya kutoka nje kutokana na unyama alionifanyia mwanaume huyo” alizidi kusikitika.

“Nilimuamini, lakini hayo ndio aliyonifanyia mimi na wanangu”, aliniambia kwa unyonge.

Alinielezea jinsi yule bwana alivyomposa kwa heshima, nidhamu na taadhima zote za Kiislamu na kuonyesha imani ya kuwapenda watoto kama vile alizaa yeye, kumbe lengo lake ni kuwafanyia unyama.

Alisema, alitumia ushirikina kuwalaghai watoto na alipendelea kusimulia kilichitokea kwa tabu na masikitiko, alikatiza kwa bubujikwa na machozi.

Baadhi ya wakati nilijiambia ningejuwa hali ni hio nisingekwenda kumuona, lakini kilichonifariji ni kwamba unyama kama ule lazima ufichuliwe, ili wasitoke wengine kuurudia.

 “Naona uchungu kunidhalilishia wanangu kiasi hiki, sina imani naye hata kidogo, kweli baadhi ya wanaume hawaaminiki ”, alisisitiza.

Kwa mujibu wa simulizi, huyu bwana alitumia mbinu ya kupandisha mizuka na kuwatishia watoto maisha yao, wakati alipojitayarisha kuwabaka.

Alisema asingeujuwa unyama alioufanya, kama mtoto wake mkubwa hakupata uja uzito ambao aligundua kutokana na uzoefu wa kukaa na watu wa aina hiyo.

Aliona ishara za mwanawe kuwa mchofu na hakuwa na bashaha ya kucheza na wenzake na wakati mwengine alilala mapema.

SHEHA wa shehia ya Kiungoni wilaya ya Wete Pemba,  Omar Khamis Othman akiwa na wadau wengine,  katika mkutano wa kupinga vitendo vya udhalilishaji kwa wanawake na watoto, mkutano huo uliwashirikisha wadau mbali mbali
Hali hio ilimtia wasiwasi na siku moja alimwita chumbani kumdadisi kilichosumbua na kumuuliza kama alishafanya kitendo cha kijituzima, lakini alimkatalia.

Lakini alipozidi kuwa na mashaka alimpeleka hospitali kwa nguvu kupimwa na huko ndipo ilibainika kuwa ni mja mzito wa miezi sita.

Baada ya kupata matokeo ya hospitali na aliyoeleza yule binti ikaufatia hatua ya kurpioti tukio kituo cha Polisi cha Micheweni na watoto wote watatu walipohojiwa ndio ikagundulika kuwa walibakwa na baba wa kambo.

Kesi ipo mahakamani inaendelea kusikilizwa mashahidi.

Huyu mtoto amedai kuwa baba yake alimdhalilisha wakati mama yao alipokuwa hayupo nyumbani kwa kujidai kupandisha mizuka na kumtishia maisha yake.

Siku moja alimwita chumbani kuchukua pesa, ili amtume dukani na alipoingia akaukomea mlango na kumbaka.

Mtoto alijitahidi kuushikilia mlango ili aufungue, lakini alizidiwa nguvu na kubakwa.

 “ Huyu ni adui kabisa, si wakuishi hapa duniani kwa jinsi alivyotudhalilisha mimi na ndugu zangu, lakini Allah atamlipa”, msichana alieleza huku machozi yakimtiririka.

Alilazimika kacha skuli mwanzoni mwa mwaka 2017 akiwa darasa la 10.

Mdogo wake mwenye miaka (14) ambaye naye aliwahi kubakwa na baba huyo, alisema ilikuwa kawaida mama yao akitoka nyumbani, yule bwana ambaye hutengeneza dawa za miti shamba, ndipo alipojidai kupandisha shetani aliyetaka watoto waridhie walichoambiwa na baba yao wa kambo.

Mara nyingi hawa watoto waliingia woga na kutekeleza amri za huyo “ shetani”.

Mara nyengine aliwachukuwa pwani katika maeneo sio sana watu kufika na huko alipandisha shetani na baadaye kuwaburura ufukweni kufanya ujahili wake.

Siku moja yule mtoto wa miaka minane (8) alikuwa akicheza rede na wenzake na aliitwa na baba yake akachukue mzigo.

Alimfuata na alimchukua  kichakani na kumtolea kisu na kumtishia kumuuwa kama ataelezea uchafu aliofanyiwa, mtoto aliogopa kumwambia mama yake.

Matukio ya ubakaji yamekuwa yakiripotiwa katika vyombo vya sheria, ambapo kesi 193 za ubakaji zilisajiliwa katika Wilaya ya Wete kutoka mwaka 2015 hadi 2017.

Idara ya Ustawi wa jamii ziliripotiwa kesi 47 za ubakaji, kituo cha mkono kwa mkono ni kesi 38, dawati la kijinsia la wanawake na watoto 91 na shehia sita za mradi wa GEWE kuliripotiwa kesi 17.

Katika shehia sita zilizofikiwa na mradi wa kukuza usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake GEWE zimeripotiwa kesi 17, ikiwa Kangagani tatu, Mjiniole tano, Kinyikani mbili, Shengejuu mbili, Mchangamdogo mbili na Kiungoni tatu.

Haroub Suleiman Hemed wa Ustawi wa Jamii, Wilaya ya Wete, anasema tabia chafu ya huyo baba kuwabaka watoto wake watatu ni ukatili ulioleta picha mbaya katika jamii.

Alisema hukumu zisizostahiki kwa kiasi fulani zinarejesha nyuma juhudi za serikali na taasisi mbali mbali katika kupinga udhalilishaji kwa wanawake na watoto na ndio maana katika ofisi hiyo wamepokea kesi za ubakaji 47.

Haroub amesema kesi tano (5) zilikuwepo Polisi, moja (1) kwa Mkurugenzi wa mashitaka, 12 mahakamani, 17 kwenye upelelezi, saba (7)zinasubiri kipimomo cha vijinasaba (DNA), mbili (2) hazikuwa na tatu (3) zilifutwa kwa kukosekana mashahidi.

Licha ya kutolewa elimu kwa jamii, vitendo vya udhalilishaji vinaendelea kufanywa siku hadi siku, kwa hivyo, ipo haja ya kuongezwa juhudi.

Khadija Henock Maziku, mmoja wa waratibu wa mradi wa GEWE, anasema inachukua muda mrefu kesi za ubakaji kushughulikiwa. 

Alitoa mfano wa kesi tano (5) ziliorpotiwa katika shehia yake kuanzia mwaka 2015 hadi Oktoba mwaka huu, ambazo zote zipo kituo cha Polisi Mchangamdogo.

Katika dawati la kijinsia la wanawake na watoto Mkoa wa Kaskazini Pema ilipokea kesi za ubakaji 191 kuanzia mwaka 2015 hadi oktoba 2017 kati ya kesi 209 za udhalilishaji zilizofikishwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa huo Haji Khamis Haji anasema kati ya kesi hizo, 32 zipo mahakama, kesi 35 zipo kwenye upelelezi na kesi 24 zimefungwa.

Anaeleza kuwa, matukio ya ubakaji yanaongezeka kutokana na wanajamii kuwa na muhali na badala yake kusuluhishana, jambo ambalo linawapa nguvu wakosaji.

Makala hii ilibisa hodi hadi ofisi ya kituo cha Mkono kwa Mkono Wilaya ya Wete, ambapo Asma Mohamed Fasihi mratibu wa kituo hicho anasema alipokea kesi 38 za kubaka kuanzia Agosti 2015 hadi mwaka huu.

“Matukio ya ubakaji yamekuwa mengi, hii ni kutokana na kuwepo kwa hukumu zisizostahili kwa watendaji wa makosa, maana mtuhumiwa wa kubaka utaona anafungwa niaka mitano, jambo ambalo haliwatii hofu wakosaji”, alifahamisha.

Mtaalamu wa masuala ya uchunguzi wa magonjwa katika Hospitali ya Mnazimoja, Dk: Msafiri Marijani alipotoa mafunzo kwa waandishi wa habari alisema, mtoto anapodhalilishwa huathirika kiafya na hata uwezo wa kufanya kazi huwa mdogo.

Moja ya athari kubwa kwa mtoto aliyebakwa ni kupata michubuko kwenye sehemu za siri ambazo zinaweza kusababisha saratani ya shingo ya kizazi, ambayo athari yake ni kukosa kizazi kabisa, vile vile upo uwezekano wa kuharibu fuko la uzazi. 

Omar Khamis Othmanm Sheha wa Kiungoni aliwataka wazazi na walezi kutekeleza wajibu wao wa kuwa walinzi na sio waangamizi wa watoto.

Tujiulize kama watakuwepo wazazi wanaofanya ujahili kama ulioelezewa hapa, watoto waelekee wapi kwa matunzo na ulinzi?.

Mtuhumiwa Hamad Omar Hamad, alikimbia na kukamatwa Fuoni, Unguja, na kurejeshwa Pemba kujibu mashitaka.

Katika kupinga vitendo vya udhalilishaji serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ilisaini mkataba wa kimataifa wa haki za watoto wa mwaka 1989 unaotaka wanachama kuwalinda watoto na udhalilishaji.

Comments

Popular posts from this blog

Wananchi wajenga wodi baada ya kuchoshwa na kujifungulia sakafuni

Sita wapotea katika mazingira tatanishi wilayani Wete

Jaji Mkuu Zanzibar awashukia mahakimu wanaonyanyasa watuhumiwa