Wazazi walalamikia utaratibu mbovu uhamisho wa wanafunzi
Na, Mac Ngaiza
Sauti ya Mnyonge, Kanda ya Ziwa
Wazazi na walezi wameendelea kushinda na wengine kueleza kuwaa wamelala katika ofisi ya mkuu wa mkoa wa Kagera wakitafuta uhamisho wa watoto wao waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika shule mbalimbali mkoani humo.
Baadhi ya wazazi wameiomba serikali kuboresha mfumo unaotumika kwa sasa kusajili wanafunzi hasa wakati wa kufanyiwa uhamisho, ili kuwaondolea usumbufu wanaokumbana nao wakati huu.
Waliozungumza na sautiyamnyonge, baadhi ya wazazi na walezi hao Raulian Kabakama kutoka halmashauri ya Misenyi na Crezensia Banobi kutoka Ushirombo mkoani Shinyanga, wamesema kuwa mfumo unaotumika kwa sasa sio rafiki kwani unachukua muda mrefu kukamilisha tarifa zao.
Kutokana na mfumo huo, wameuambia mtandao huu kuwa imekuwa siku ya tatu sasa tangu wafike katika ofisi za mkuu wa mkoa, na bado hawajapewa barua wanazoshughulikia kama uhamisho ili kuthibitishwa kwenye shule wanazolenga kuhamishia watoto wao.
Wamesema kuwa maelezo waliyopewa yanawataka kuwa wavumilivu, kwamba wahusika wanaendelea kuhakiki majina na kuchapa barua hizo.
Sautiyamnyonge imemtafuta afisa elimu mkoani Kagera Aloyce Kamamba, aliyethibitisha uwepo wa suala hilo, na kwamba ofisi hiyo inaendelea na taratibu za kuwahudumia wazazi hao, angawa amesema kuwa pamoja na kazi hiyo kufanyika taratibu sababu ya miundombinu inayotumika, amesema kuwa wazazi wengi wanaleta barua ambazo zimekosewa majina ya wanafunzi, na kuanza upya kazi ya uhakiki.
Pamoja na hayo, Kamamba amewasihi wazazi hao kuwa wavumilivu wakati suala lao likishughulikiwa, kwamba wote watapata huduma bila kukwama, kwa kuwataka kuhakikisha wanahakiki majina ya watoto wao kabla ya kuandika barua ya maombi.

Comments
Post a Comment