Waliotubu kutengeneza mkaa, wataka wenzao wanaoendelea wadhibitiwe
Na Haji Nassor
Sauti ya Mnyonge, Pemba
VIJANA kisiwani Pemba, walioamua kuachana na kazi ya upigaji mkaa, wameiomba wizara husika, kuwashughulikia vijana kutoka Tanzania bara, wanaoshirikiana na wenyeji, kuendelea na kazi hiyo kwa kasi.
Walisema, wao wameshakubali kuacha na kazi hiyo, hasa kwa vile athari yake ni ya muda mrefu inayotokana na ukataji miti, ingawa wapo wengine, wakishirikiana na wageni wakifanya kazi hiyo.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti, walisema kisiwa cha Pemba, kimekuwa kikipoteza miti kadhaa siku hadi siku, kutokana na ukataji hasa kwenye sekta ya utengenezaji mkaa.
Walisema lazima wizara husika, iingilie kati juu ya vijana hao, ili kuwadhibiti kwa lengo la kukinusuru kisiwa cha Pemba na upotevu wa mkubwa wa miti.
Mmoja kati ya vijana hao, Ali Mkubwa Hussein, alisema wao wameshaachana na kazi hiyo na kuelekea kwenye kilimo cha mboga mboga, na hasa baada ya kuelimishwa juu ya athari za ukataji miti.
“Sisi tuliitwa kwenye semina na kuelezwa athari za ukataji miti, na tukaombwa tuachane na kazi hiyo, lakini wenzetu hapa Pemba wanashirikiana na wengine wakifanya kazi hiyo bila ya kujali athari”,alieleza.
Haji Mohamed Omar wa Tundauwa, alisema wapo vijana kutokana Tanzania bara, wamekuwa wakiendesha kazi hiyo, kwa kukata miti kama Miembe na Mizambarau, jambo ambalo linahatarisha upotevu wa miti.
Nae Mohamed Juma Machano wa Chanjamjawiri, alisema wakati umefika kwa wizara husika, kuwatumia wale walioacha kazi ya kupiga mkaa, kuwasaka wanaofanya kazi hiyo kinyume na taratibu.
“Wapo wanaovamia misitu na kuikata bila ya kibali, sasa lazima mikakati ya kweli iwekwe, maana misitu ya Pemba, inaendelea kupotea siku hadi siku”,alifafanua.
Mapema Afisa anaeshughulikia misitu kisiwani Pemba, Said Juma Ali, alisema kimsingi kila mtu aliepo Zanzibar anatakiwa kufuata taratibu za kuheshimu sheria za nchi.
Alisema sheria za kuomba kibali kabla ya kukata miti na kuwa na kibali ya usafirishaji wa mkaa, linamuhusu kia mmoja awe mtanzania bara au mzanzibari.
“Sheria za kuomba kibali cha kukata miti, usafirishaji mkaa na ruhusa ya kufanya kazi hiyo, ni kwa watu wote, sasa sisi tutawashughulikia hata kama ni wazanzibar au wageni”,alifafanua.
Katika hatua nyengine Afisa huyo wa Idara ya Misitu Pemba, aliwataka wananchi kuendelea kushirikiana na Idara hiyo, ili kuwadhibiti wanaoendesha biashara ya mkaa pasi na kuwa na kibali husika.
Kwa mujibu wa utafiti wa “bioanuwai” uliofanywa mwaka 2012 umebaini kuwa msitu wa Zanzibar unapotea kwa asilimia 1.2 kila msitu wa ekari 100.
Comments
Post a Comment