Walimu watakiwa wasitumie wabunge kuomba uhamisho
Na, Mwandishi Maalum
Sauti ya Mnyonge, Dodoma
WALIMU pamoja na watumishi wengine wametakiwa kuacha mara moja kutumia viongozi wakiwemo wabunge kuwaombea uhamisho wa vituo vya kazi.
Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Joseph Kakunda alipokuwa akijibu swali la Rehema Migill Viti Maalum CUF
Kakunda alisema serikali inatambua kwamba uhamisho wa watumishi wa umma ni haki ya mtumishi endapo atazingatia utaratibu uliowekwa .
Alisema kuanzia Julai 2017 hadi sasa, serikali imetoa vibali vya uhamisho kwa walimu 2,755.
Naibu huyo alilieleza Bunge kuwa taratibu za kutoa vibali vya uhamisho kwa walimu wengine walioomba zinaendelea.
“Nachukua nafasi hii kuwaelekeza walimu pamoja na watumishi wengine wote, kuzingatia utaratibu na waache kutumia viongozi mbalimbali wakiwemo wabunge kuwaombea uhamisho” alisema.
Aidha Naibu Waziri alisema hakuna vikwazo kwa walimu wanaotaka kuhama vituo vyao vya kazi kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kufuata wenza wao au ugonjwa.
Hata hivyo alisema katika kuhamisha walimu , serikali inazingatia ikama ili kutoathiri taaluma kwa kuhakikisha wanafunzi wanaendelea kufundishwa masomo yote.
"Kwa mujibu wa mitaala ya elimu iliyoidhinishwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia hitaji hilo ndilo linalosababisha katika baadhi ya maeneo walimu kusubiri apatikane mwalimu mbadala kwanza kabla ya kutolewa kwa kibali cha uhamisho” alisema.
Katika swali lake Rehema alitaka kujua ni lini serikali itaondoa vikwazo kandamizi kwa walimu wanaotaka kuhama vituo vyao vya kazi kwa hiari yao kutokana na sababu mbalimbali.
Comments
Post a Comment