Shule yafungwa kwa muda usiojulikana Singida
Na Mwandishi Wetu
Sauti ya Mnyonge, Singida
Viongozi wa shule ya SAFINA TUNAJAA ISLAMIC AND ENGLISH MEDIUM SEMINARY, iliyoko Ikungi, wakitoa maelezo kwa Mratibu Elimu kata ya Sepuka,Chitaeli Philipo Kisombo
WIZARA ya elimu,Sayansi na Teknolojia imeifunga kwa muda usiojulikana shule ya msingi ya Taasisi ya madhehebu ya dini ya kiislamu ya Safina Tunajaa Islamic and English Medium iliyopo tarata ya Sepuka,wilaya ya Ikungi,Mkoani Singida kutokana na shule hiyo kutokuwa na usajili kwa zaidi ya miaka mitatu tangu ilipoanzishwa.
Akithibitisha kufungwa kwa shule hiyo kufuatia ukaguzi alioufanya siku ya kwanza ya kufungua shule zote,Mratibu wa elimu wa kata ya Sepuka,mwalimu Chitaeli Philipo Kisombo alisema kuwa kwa sababu shule hiyo haina usajili,hivyo wanafunzi wangeendelea kukaa bure mpaka darasa la saba.
“Shule kwa hali halisi tangu ianzishwe haina usajili wanafunzi wangekaa bure bila sababu mpaka wafike darasa la saba wangekuwa hawajui la kufanya kwa maana hiyo shule imejifunga kwa utaratibu mpaka itakapokamisha taratibu zinazotakiwa kisheria.”alisisitiza Mratibu elimu kata huyo.
Hata hivyo Kisombo alifafanua kwamba wanafunzi waliokuwa wakisoma darasa la tatu na la nne katika shule hiyo watahamishiwa katika shule msingi mama ya Mnang’ana kuanza masomo ya mfumo wa Memkwa na walioandikishwa kuanza darasa la kwanza wataandikishwa katika shule ya msingi Mnang’ana.
Kwa mujibu wa afisa huyo mwenye dhamana ya kusimamia sekta ya elimu wanafunzi hao watarudi na kuendelea na masomo katika shule ya Safina mara tu baada ya uongozi wa shule hiyo kukakamilisha taratibu za usajili wake,na wala siyo vinginevyo.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa shule hiyo,Idrisa Juma Mpinji aliweka bayana kwamba pamoja na kwamba siku ya jumatatu ilikuwa ni siku ya kufungua shule lakini kutokana na barua waliyopokea kutoka wizarani imewazuia kabisa kufungua shule mpaka hapo maelekezo waliyotoa yatakapokamilishwa.
Mwalimu mkuu huyo hata hivyo alibainisha pia kwamba barua za kuomba usajili zipo wizarani,lakini kutokana na sheria ya wizara ili shule iweze kupata usajili haina budi kutimiza vigezo maalumu vinavyotakiwa.
Alivitaja vigezo walivyoagizwa kuvitekeleza kuwa ni kukamilisha ujenzi wa vyumba sita vya madarasa,ofisi tatu,stoo,bwalo la chakula pamoja na maatundu ya vyoo ya kutosha.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mnang’ana,Paskali Juma Mdimi kwa upande wake alisema kwamba shule hiyo iliyoanzishwa mwak 2015,ilikuwa na jumla ya walimu wanne na ilifuata taratibu zote za Kijiji,ikiwemo kuomba eneo lenye ukubwa wa ekari 12 ambazo zilipimwa na kamati ya huduma za jamii.
Aidha Mdimi aliweka wazi kuwa awali uongozi wa taasisi hiyo ulianzisha msikiti na ndipo baadaye wakaanzisha shule ya awali na hivi sasa imeshindwa kukamilisha usajili wake kutokana na kuwa na vyumba vya madarasa machache.
Mwenyekiti huyo hata hivyo aliweka bayana mikakati ya Kijiji hicho juu ya ukamilishaji wa taratibu walizowekewa na wizara ni kwamba uongozi wa Kijiji unaendelea kuwasisitiza uongozi wa shule hiyo kuhakikisha unakamilisha taratibu zote za kisheria walizoagizwa na wizara.
Katibu Mkuu wa Taasisi ya Safina Tunajaa Islamic and English Medium Seminary ,Shabani Saidi Jimbi alibainisha mikakati iliyowekwa na Kijiji hicho kuwa ni pamoja na kuanzisha michango kwa wazazi wa wanafunzi hao ili ifakapo mwezi wa tano,mwaka huu waweze kukamilisha masharti yaliyowekwa na wizara hiyo.
Comments
Post a Comment