Serikali visiwani Zanzibar, yakana kuwepo utawala wa mabavu
Na, Haji Nassor
Sauti ya Mnyonge, Pemba
MAKAMU wa Pili wa rais Zanzibar Mhe: Balozi Seif Ali Idd, amesema Serikali ya Mapinduzi wa Zanzibar, kuridhia dhana ya ugatuzi wa madaraka, ni kuonyesha kwa vitendo kuwa, hakuna uongozi wa kimabavu kama wengine wanavyofikiria
Alisema wapo wanaopita pita wakisema kuwa serikali iliopo madrakani, inaongozwa kimabavu, bila ya kujua kuwa tayari sasa madaraka yanapelekwa kwa wananchi ili wawe na mamlaka ya kujiamulia mambo yao.
Makamu huyo wa Pili, ameleza hayao jana, baada ya kulifungua ramsi jengo jipya la Baraza la mji wa Chake chake kisiwani Pemba, ikiwa ni shamra shamra za miaka 54 ya Mapinduzi Zanzibar yalioasisiwa mwaka 1964.
Alisema lengo la kukasimu madaraka na sasa kuyapeleka kwa wananchi, ni ishara ya kuwaumbua wale wanaofikiria kwamba Zanzibar hakuna utawala wa kidemokrasia.
Alisema lengo hasa la ugatuzi wa madaraka ni pamoja na kuimarisha dekorasia, kurahisishwa upatikanaji wa huduma za kijamii, jambo ambalo hapo awali zilikuwa zikipatikana serikali kuu pekee.
Balozi Seif alisema, kwa dhana hiyo sasa serikali kuu itaendelea kusimamia yale mambo ya jumla ya nchi, kama vile utungaji wa sera, sheria na kusaini miradi mikubwa yanayokwenda serikali moja kwa moja.
“Leo tukiwa ndani ya miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar, kila mmoja ni shahidi kuwa, sasa madaraka yanapelekwa ngazi ya vijijini, na hayo yote ni ishara kuwa, ni waongo wanaosema Zanzibar kuna utawala wa mabavu”,alifafanua.
Katika hatua nyengine, Makamu huyo wa Pili wa rais Zanzibar Mhe: Balozi Seif Ali Idd, alisema moja ya malengo makuu ya Mapinduzi Zanzibar ni kuondoa pia ubaguzi.
Alieleza kuwa, ufunguzi wa jengo hilo jipya la Baraza la mji Chakechake, lazima watendaji watakaobahatika kufanya kazi humo, hilo walizingatie maana wao ndio wanaotegemewa kuwaletea maendeleo wananchi.
Alifahamisha kuwa, ikiwa watatoa huduma kwa njia ya ubaguzi, basi wasitarajie kufikia ndoto za wananchi za kupokea huduma bora na kwa wakati, ambazo hapo awali zilikuwa zikiwasumbua.
“Sitaki kusikia kuna mfanyakazi wa baraza la mji Chakechake anatoa huduma kwa njia ya ubaguzi, maana kufanya hivyo ni kudhofisha ufanisi, na hatutosita kufukuzwa kazi mara moja”,alieleza.
Hata hivyo, Makamu huyo wa Pili, amesisitiza kwa watendaji wa Baraza la mji, kuhakikisha wanalitunza jengo hilo, ili liweze kudumu kwa miaka kadhaa ijayo.
Aidha amewataka wananchi kuendelea kuyathamin, kuyaenzi, kuyadumisha na kuyalinda mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, kwani ndio mkombozi wa wazanzibari.
Mkuu wa Mkoa wa kusini Pemba Hemed Suleiman Abdalla, amerejea kauli yake, kwamba atawashughulikia hata kama ni viongozi, watakaofanya vitendo vya udhalilishaji ndani ya mkoa wake.
Alisema anazo taarifa rasmi, kwamba wapo baadhi ya viongozi kwa kutumia nafasi zao, wamekuwa wakizifanyia sulhu, kesi za aina hiyo, na kuwataka wenye tabia hiyo kutafuta mkoa mwengine haraka wa kuhamia, kama hawawezi kuacha uovu wao.
Akisoma taarifa za ujenzi huo, Katibu mkuu wizara ya Nchi, Afisi ya Rais, Tawala za Mikoa, serikali za mitaa na Idara maalum za SMZ, Khamis Mussa Omar, alisema ni sehemu ya mradi mkubwa uliochini ya Benki ya dunia kwa mkopo nafuu.
Alisema huo ni mradi wa maendeleo ya jamii Zanzibar ZUSP, ambapo jengo hilo lenye ghorofa mbili likiwa na vyomba 20, na kumbi tatu za mikutano, limegharimu shilingi milioni 944.3 hadi kuweza kutumika.
Ujenzi wa jengo sambamba na ukarabati mkubwa kwa baadhi ya maeneo, ulianza mwezi April mwaka 2015 na kumalizika mwezi Novemba mwaka jana chini ya mjenzi kampuni Noe Investment ya Dar-es Salaam.
Comments
Post a Comment