Mkuu wa Wilaya aagiza TAKUKURU kuchunguza mapato mgodi wa dhahabu wa Kitunda

Na Mwandishi Wetu
Sauti ya Mnyonge, Sikonge

MKUU wa wilaya ya Sikonge Mkoani Tabora Peresi Magiri ameagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani humo kwenda kuchunguza upotevu wa mapato ya mgodi wa dhahabu Kitunda ili wahusika wote wawajibishwe.

Amelitoa agizo hilo jana kwenye kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo baada ya madiwani kutoridhishwa na makusanyo ya ushuru wa mgodi huo na kulalamikia uwepo wa mianya mingi ya upotevu wa mapato hayo.

Alisema lisemwalo lipo, haiingii akilini mapato ya mgodi wa dhahabu Kitunda yawe kiduchu kiasi hicho, kuna kitu hapa, ni lazima uchunguzi wa kina ufanyike ili kubaini fedha hizo zinaenda wapi na wahusika ni akina nani na hatua zichukuliwe.

‘Nimesikia malalamiko ya madiwani, naagiza uchunguzi wa haraka na wa kina ufanyike pale mgodini, TAKUKURU nenda kafanye hiyo kazi, na unipe taarifa haraka ili tuchukue hatua kwa watakaobainika’, alisema.

DC alibainisha kuwa suala la ukusanyaji mapato sio la DC au DED pekee yake, bali watumishi na madiwani wote, ushirikiano ni muhimu sana katika hili ili kubaini mianya yote ya wizi wa mapato ya halmashauri na hatua stahiki kuchukuliwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Simon Ngatunga aliunga mkono agizo la DC la kutaka uchunguzi wa kina ufanyike katika mgodi huo ili kubaini mianya yote ya upotevu wa mapato hayo na wahusika wote wawajibishwe.

Alimwagiza Mkaguzi wa ndani wa halmashauri hiyo Hamza Mbongo kuungana na TAKUKURU  kukagua mapato yote yatokanayo na mgodi huo ili kubaini mianya ya upotevu wa fedha hizo na wahusika ni akina nani.

Alishauri wanasiasa kutoingiza maslahi binafsi katika mapato ya mgodi huo na kuwataka kufichua mianya yote ya upotevu wa mapato, aidha alisema wajibu wake nikuhakikisha ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi inatekelezwa kwa vitendo na si kufumbia macho uharibifu.

‘Madiwani msikae kulalamika tu, yeyote mwenye ushahidi wa wizi wa mapato ya halmashauri alete taarifa ili sheria ichukue mkondo wake, serikali ya Rais Dk John Pombe Magufuli haina mchezo na wabadhirifu wa mali ya umma,’alisema.

Alifafanua kuwa mfumo unaotumika kukusanya mapato ya halmashauri ni ule wa mashine za kielekroniki na mashine zaidi ya 60 zipo katika kata zote ikiwemo kule mgodini na kila fedha inayokusanywa inasomeka moja kwa moja katika komputa.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Peter Nzalalila alisema hawako tayari kufumbia macho mtu yeyote anayeiba fedha za halmashauri, ni lazima hatua za kisheria zichukuliwe haraka iwezekanavyo, TAKUKURU na Mkaguzi fanyeni uchunguzi haraka, taarifa iwe tayari ndani ya wiki moja.

Wakiongea kwa masikitiko makubwa madiwani Juma Mdullah wa kata ya Mpombwe, Fred Masamalo (Usunga), Mbaruku Mgaywa (Mole), Mbwana Seif (Kitunda) na Juma Ikombola (Misheni) walisema mgodi huo una ubadhirifumkubwa sana na hata mapato yalioandikwa sio sahihi.

Walibainisha kuwa uwiano wa mapato yaliyopatikana haviendani na uhalisia wake, ni lazima hatua zichukuliwe haraka iwezekanavyo,waliafiki agizo la DC la kupeleka TAKUKURU pale mgodini na kutakauchunguzi wa kina.

Comments

Popular posts from this blog

Wananchi wajenga wodi baada ya kuchoshwa na kujifungulia sakafuni

Sita wapotea katika mazingira tatanishi wilayani Wete

Jaji Mkuu Zanzibar awashukia mahakimu wanaonyanyasa watuhumiwa