Mbunge ahofia uhaba wa wataalamu sekta ya afya nchini
Na, Mwandishi Maalum
Sauti ya Mnyonge, Dodoma
MBUNGE wa Hanang Dk.Mery Nagu (CCM) ameonesha kuwa na wasiwasi kuwa kuna uwezekano wa viongozi kuhamasisha ujenzi wa vituo vya afya pamoja na zahanati lakini wasiwepo wataalamu wa sekta ya afya kutokana na kutokuwepo kwa watumishi wa kutosha.
Akiuliza swali jana bungeni Dk.Nagu aliitaka Serikali ieleze ina mikakati gani ya kuongeza watumishi wa sekta ya afya katika vituo mbalimbali vya afya na zahanati kutokana na kukosekana kwa wataalam.
“Je si kazi bure kama wananchi watajenga vituo vya Umma vya afya na zahanati lakini havitumiki je serikali ina mpango gani wa kuongeza watumishi katika vituo hivyo licha ya kuwepo kwa upungufu mkubwa wa watumishi katika sekta hiyo” alihoji Dk.Nagu.
Awali katika swali la msingi la mbunge wa Busanda Lolensia Bukwimba (CCM) alitaka kujua serikali ina mkakati gani wa kuondoa uhaba wa watumishi wa sekta ya afya katika mkoa wa Geita kutokana na tatizo hilo kuwa kubwa.
“Tatizo la uhaba wa watumishi katika sekta ya afya kwenye halmashauri ya wilaya ya Geita ni mkubwa sana, je serikali ina mkakati gani wa dharula wa kuondoa tatizo hilo” alihoji Bukwimba.
Akijibu swali la nyongeza la Dk.Nagu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora,George Mkuchika,alisema kuwa ni kweli upo uhaba mkubwa wa watumishi katika sekta ya afya.
Alisema baada ya uhakiki wav yeti feki ilionekana kuwepo kwa uhaba mkubwa wa watumishi hususani katika sekta ya afya na kusababisha vituo vingi na zahanati kutokuwepo kwa watumishi wa kutosha na kufikia hatua ya vituo hivyo kufungwa.
Hata hivyo alisema kuwa serikali imeisha toa kibali cha ajira zaidi ya 50,000 na kipaumbele zaidi ni katika sekta ya afya na kuwataka wabunge kumwandikia moja kwa moja barua ya maombi ya kuomba watumishi wa sekta ya afya kwa halmahauri ambayo haina watumishi wa kutosha.
Hata hivyo aliwataka wabunge na jamii kwa ujumla kuendelea na juhudi ya uhamaishaji wa ujenzi wa majengo ya zahanati pamoja na vituo vya afya kwa maelezo kuwa watumishi watapatikana wa kutosha na kufanya kazi nzuri.
Naye Waziri WA Nchi Ofsi ya Rais –TAMISEMI Josephati Kandege,akijibu swali la msingi alisema halmashauri ya wilaya ya Geita ina mahitaji wa watumishi sekta ya afya 465 ambapo waliopo ni 225 na kuna upungufu wa watumishi 240.
“Upungufu huu unatokana na sababu mbalimbali ikiwemo uhamisho,vifo,kustaafu pamoja na zoezi la kiserikali ya uhakiki wav yeti feki pamoja na kuondoa watumishi hewa” alisema Kandege.
Comments
Post a Comment