Makamu wa Rais Zanzibar, atahadharisha wakandarasi
Na, Biabu Zume
Sauti ya Mnyonge, Zanzibar
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe:Balozi Seif Ali Iddi, amewaomba Wakandarasi na wasimamizi wanaopata kazi za Ujenzi katika Taasisi za Serikali, kufanya kazi zao kwa uadilifu wa hali ya juu, kinyume chake Serikali haitokubali kukabidhiwa majengo yasiyokuwa na kiwango.
Alisema Serikali italazimika kutumia sheria za ujenzi, zilizopo katika njia na Utaratibu wa kukataa kazi yoyote ile, iliyokuwa chini ya kiwango kinachokubalika kimikataba.
Balozi Seif Ali Iddi, alitoa ombi hilo wakati akiweka Jiwe la Msingi wa Ofisi Tatu Pacha za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambazo ni Wizara ya Kazi Uwezeshaji, Vijana, Wazee, Wanawake na Watoto, Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, huko Gombani Gombani Chake Chake Pemba.
Alisema haikubaliki kuona muda mfupi tu, baada ya kukamilika kwa Ujenzi na kukabidhiwa Majengo hayo yanaanza kuharibika, kuvuja, kupasuka, kupoteza haiba na hadhi inayokusudiwa.\
Balozi Seif alisema hivi sasa yapo Mjengo mengi hasa yale ya Skuli, katika maeneo tofauti Nchini yaliyojengwa chini ya kiwango, zimeanza kuvuja kama chungio jambo ambalo Serikali Kuu, tayari imepata fundisho kutoka kwa baadhi ya Wakandarasi, hivyo hapana budi sasa kuchukuwa tahadhari.
Alieleza kuanzishwa kwa ujenzi wa majengo pacha, kwa ajili ya matumizi ya Ofisi za Wizara Tatu za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambao zote ni muhimu kumefungua fursa za ujenzi wa jengo jengine, kwa ajili ya matumizi ya Ofisi ya Bodi ya Mapato Zanzibar(ZRB) litakalokuwepo Mkabala na Majengo hayo.
Balozib Seif alisema ujenzi huo, utazidi kulifanya eneo hilo la Gombani kuwa na haiba nzuri zaidi na matarajio ya Wananchi, wanaoishi jirani na maeneo hayo, wanaweza kunufaika kwa kuitumia fursa hiyo, kwa kuanzisha biashara ndogo ndogo.
“Biashara itakayoanzishwa itasaidia kutoa ajira kwa Wananchi, itaweza kuwahudumia Wafanyakazi wengi watakaokuwa wanapita katika maeneo yao, wakati wakielekea au kutoka kazini”alisema.
Aidha Balozi Seif, aliwapongaza Wananchi na Vijana
wote waliokuwa wakilitumia eneo hilo, kwa uamuzi wao wa kizalendo waliouonyesha wa kuamua kuondoka wenyewe kwa hiari yao, ili kupisha shughuli za ujenzi wa Ofisi za Serikali.
“Kulikuwa na Vijana waliolitumia eneo hilo kibiashara, uoshaji wa Magari pamoja na Wakulima, waliojishughulisha na kilimo cha mboga mboga, ambao walikubali kuhama kupisha mradi wa maendeleo bila ua usumbufu” alisema.
Hata hivyo aliwataka Wananchi wa maeneo mengine ya Pemba na Unguja, ambao wanatumia ardhi ya Serikali kwa kufanya shughuli zao binafsi, wanapaswa kujifunza kutoka kwa Wananchi wa Gombani, kwa kuondoka bila ya malalamiko kupisha ujenzi wa Serikali.
Aliongeza kukamilika kwa ujenzi wa Ofisi hizo Tatu Pacha na kuanza kutumika kwake, kunatarajiwa kuimarisha huduma zinazotolewa na Wizara hizo Kisiwani Pemba.
Alisema katika kuimarishwa huduma hizo, kwa Wananchi Serikali imepanga kuweka mifumo ya Kisasa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, ambayo kwa kiasi kikubwa huwa inachochea utendaji kazi.
Comments
Post a Comment