Wananchi wadai kuvamiwa na Askari wakimsaka alietoroka chuo cha Mafunzo
WANANCHI wa kijiji cha Kwamgogo shehia ya Mkungu wilaya ya Mkoani, akiwemo mzee wa miaka 55, walijikuta katika mazingira ya taharuki, baada ya kudai kuvamiwa na Askari wa Chuo cha Mafunzo kambi ya Kengeja, muda mfupi baada ya kudai kutorokewa na mwanafunzi wa chuo hicho.
Wananchi hao walisema, kati ya Disemba 18 na 19 ya nyakati tofauti, walivamiwa na wapigaji hao wapatao 15 wakiwa na silaha kwa kuanza msako wa nyumba kadhaa hadi kwenye dari, ili kujiridhisha iwapo mwanafunzi wao alietoroka, amefichwa na wananchi hao.
Wakizungumza na waandishi wa habari hizi kwa njia ya simu, mwanachi Abass Fumu Omar (55), alisema yeye alipigwa ngumi tatu za mgongo na teke na watu aliodai kuwa ni askari, wakati alipowauliza kwamba kwanini wanamchukua kijana wao wa mtaani.
Alisema tukio hilo lilitokea majira ya saa 2:30 usiku, kabla ya yeye kupewa kichapo hicho, aliona kundi kubwa la Askari hao, wakiwa na silaha, huku wakiwa wamemshikilia kijana alietambulika kwa jina la Mwalimu Juma Silima, kwa lengo la kumpeleka kambini kwao.
Mzee huyo alieleza kuwa, pamoja na kupigwa huko alilazimishwa kuwenda mwendo wa chura “kichura” na alipomaliza alianguka chini kutokana na machofu na maumivu aliokuwa nayo, ingawa walifanikiwa kuondoka na kijana mmoja wa mtaani kwao.
“Kwa kweli mimi nipo hapa mwaka wa 50 sasa, lakini sijaona madhila na manyanyasao haya, na wameshatoroka wanafunzi zaidi ya wanne (4), na kisha huja hapa askari kutuuliza na kuondoka, lakini mwaka huu wa 2017 kwetu sisi wananchi wa kijiji cha Kwamgogo, unamalizika vibaya”,alieleza.
Nae mwalimu wa skuli ya sekondari ya Mwambe anaeishi kijiji hicho, Simai Juma Simai, alisema yeye wakati akiwa amelala alisikia mabishano makali, nje ya nyumba yake, ndipo alipoamka na kushudia baadhi ya askari hao wengine wakiwa na silaha akimuhojia mdogo wake Mwalimu Juma Simai (39).
Alieleza kuwa, mara baada ya kuona mjadala huo, alijaribu kusogea karibu na kisha baada ya mabishano makali, waliondoka na mdogo wake, na ndipo alipotokezea mzee Abass Fumu Omar (50) akiwa na embe na tochi mkononi, na kumpiga wakidhani amebeba mawe.
“Nilimshuhudia mzee Abass pamoja na ugonjwa alionao, lakini alitakiwa aende mwendo wa chura, baada ya kupigwa ngumi za mgongo na kuanguka chini, wakieleza kuwa anataka kuchafua amani kwa kubeba mawe”,alifafanua.
Mjumbe wa sheha wa shehia ya Mkungu kwenye kijiji hicho, Fatma Simai Ali, alithibitisha kufanyiwa uavamizi huo na askari aliodai kuwa ni wa Chuo cha Mafunzo kambi ya Kengeja, na mwananchi huyo kupigwa na mwengine kuchukuliwa kambini, kuanzia majira y ass 2:30 usiku na kuachiwa majira ya saa 5:30 usiku huo.
Mjumbe huyo wa sheha, alisema usiku wa Disemba 19, walikuja na kuendesha msako makali wa nyumba tatu, ambazo wenyewe walikuwa na wasiwasi, kwamba mwanafunzi alietoroka amefichwa ndani ya kijiji hicho, ingawa waliondoka bila ya mafanikio.
“Nilishangaa walipokuja tena siku ya pili, eti wakanitafuta mimi kutaka ruhusa, nilipowauliza kwamba jana walivamia bila ya ruhusa yangu, wakanitolea maneno makali, na kuniambia hawataki kufundishwa kazi na mimi, kumbe walijua wameshaomba ruhusu ya sheha wa Kengeja, ingawa kijiji hicho sio shehia yake”,alifafanua.
Katika hatua nyengine, Mjumbe huyo wa sheha wa shehia ya Mkungu, alisema kitendo hicho kimewadhalilishaji na kuwavua nguo, maana hawakufuata taratibu na sheria, ingawa wao ndio wanaopaswa kulinda sheria za nchi na wananchi.
Naibu sheha wa shehia hiyo, Faki Othaman Juma, alikiri kupokea taarifa hiyo kutoka kwa naibu wake, ingawa yeye hadi uvamizi huo unafanywa na Askari wa chuo cha Mafunzo hakuwa na taarifa rasmi.
“Mimi sikuwa na taarifa kwamba kunafanyika msako wa mwanafunzi alietoroka, kumbe wale Askari walimpigia simu sheha wa shehia ya Kengeja, wakidhani kuwa ni shehia yake”,alifafanua.
Hata hivyo, Naibu huyo alikiri kuwa wapo baadhi ya wananchi waliopigwa na mwengine kuchukuliwa chuo cha Mafunzo, wakati wa usiku chini ya ulinzi mkali, wakituhumiwa kumficha mwanafunzi alietoroka.
Katibu tawala wilaya ya Mkoani Miza Hassan Faki, alisema hadi sasa wilaya haijapokea taarifa rasmi za tukio hilo la wananchi kuvamiwa na wengine kupigwa, kulikosababishwa na kutoroka kwa mwanafunzi huyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa kusini Pemba, Shehan Mohamed Shehan, alisema hajapokea taarifa zozote, juu ya tukio hilo la wananchi kuvamiwa na askari wanaodaiwa kuwa ni wa Chuo cha Mafunzo kambi ya Kengeja.
“Hadi sasa sina taarifa zozote za tukiol hilo lakini ngoja nifuatilie kwa kwa kamanda wa Poilisi wilaya ya Mkoani, nione kama yeye amaeshapa taarifa hizo”,alisema Kamanda Shehan.
Kamisha wa Vyuo vya Mafunzo Zanzibar Ali Abdalla Ali, alimueleza mwandishi wa habari hizi kuwa, hizo ni siri za serikali na wala hazipaswi kutolewa kwenye vyombo vya sheria juu ya kutoroka kwa mwanafunzi.
“Wewe mwandishi tokea uanze kazi hii ni mara yako ya ngapi kuandika habari za mwanafunzi kutoroka, basi kama hujawahi kuandika na hii kama ni ya kwanza, ujue kuwa hii ni siri ya serikali, haipaswi kuandikwa ingawa kwenye vyombo vya hata kama ni ya kweli”,alifafanua.
Aliongeza kuwa, kama ziko siri za serikali na ambazo hujitokeza na hazipaswi kutangaazwa hasa kwenye vyombo vya habari, moja wapo ni hiyo ya kutoroka mwanafunzi alie chuo cha mafunzo.
Awali Naibu Kamishna wa vyuo hivyo Zanzibar dk Haji, alikiri kuwa taarifa hizo za kutoroka kwa mwanafunzi huyo, zimeshafika mezani kwake, lakini yeye sio msemaji wa Chuo cha Mafunzo.
“Ni kweli kuwa mwanafunzi ametoroka kambi ka Kengeja, lakini mimi sio msemaji, na wala sina taarifa kuwa, wananchi wanaoishi karibu na kambi kwamba wamepigwa”,alifafanua.
Alipoulizwa Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe: Omar Othman Makungu, alisema hana hakika sana kuwa tukio la kutoroka mwanafunzi ni sehemu ya siri ya serikali, maana sheria mpya ya vyuo vya mafunzo hajaisoma kujua hilo kuwa limo.
“Mimi niko likizo muda huu, na hiyo sheria yao inayoeleza kuwa ni siri ya serikali, sina hakika sana, maana mimi sio semaji wa vyuo vya mafunzo Zanzibar, hivyo sina hakika na hilo, inawezekana ni kweli ni siri za utawala”,alieleza.
Baadhi ya wananchi ambao hawakupenda majina yao yachapishwe, walisema kutoroka kwa wanafunzi wa chuo cha mafunzo kwenye Kambi ya Kengeja, imekuwa ni jambo la kawaida, maana ndani ya miaka 30 sasa wameshafikia wanafunzi wanne.
“Mimi nipo hapa Kengeje kwa muda mrefu sasa, lakini kusikia mwanafunzi katoroka mbona ni kawaida, haipiti miaka 10 utasikia kishindo huyo huyo”,alieleza mwananchi huyo.
Hata hivyo wananchi hao, wamewataka wapiganaji hao wa vyuo vya mafunzo kukaa vyema na wananchi, ili wanapohitaji msaada iwe rahisi kwao.
Chuo cha mafunzo kambi ya Kengeja kimekuwa ni sehemu ya kuwapokea wanafunzi, ambao wameshahukumiwa kutumikia adhabu, na kwa sasa wameshajengea jengo jipya la kuhifadhi wanafunzo hao, ambapo pia taarifa zinaeleza kuwa, wapiganaji hao wanajipanga kwenda kijijini hapo kuomba radhi kwa kufanya tukio hilo.
Comments
Post a Comment