MAMCU yaonya viongozi waweka mawe kwenye magunia ya korosho

Na, Florence Sanawa, 
Sauti ya Mnyonge, Mtwara


Kuelekea mwishoni mwa msimu wa korosho Chama kikuu cha ushirika cha Masasi, Mtwara Cooperative Union MAMCU kimetoa onyo kali kwa vyama vya msingi kuacha udanganyifu unaofanywa wa kuweka mawe katika magunia ya korosho ili kuongeza uzito wa bidhaa hiyo.

Kaimu Meneja wa Chama hicho Potency Rwiza ansema  kuwa udanganyifu huo unaweza kuharibu soko la korosho kwa misimu iliyobakia.

Hofu hiyo imejitokeza katika chama cha msingi cha Umoja ni Nguvu kilichopo wilayani Masasi na kufanikiwa kukuta moja ya magunia yaliyojazwa katika chama hicho yakiwa yamewekewa mawe katikati.

 “Suala hilo sio mara ya kwanza kujitokeza katika kipindi cha ununuzi wa zao hilo, ambapo msimu uliopita liliwahi kulalamikiwa na wanunuzi ndio maana tuliamua kufanya uchunguzi na kubaini hilo na pia tulikuta korosho na mawe zimechanganywa ndio maana tuliamua kuwachukulia hatua na kuwakabidhi katika vyombo vya ulinzi ili hatua zingine ziweze kuendelea” alisema Potency


Kwa upande wake Sharafi Mtondo  alisema kuwa serikali iwachukulie hatua wanaofanya udanganyifu ili kutoruhusu kuharibu jina la nchi kwa kuchanganya mawe na uchafu kwenye magunia ya korosho.

“Wakati wa msimu wa korosho kumekuwa kukijitokeza matukio mengi ya udanganyifu ikiwemo kuwekewa uchafu ikiwemo mabibo, mawe hali ambayo inapunguza uaminifu wa viongozi wa vyama vya msingi na wakulima wenyewe…

“Njaa ndio inawaumiza hawa watu wa vyama vya msingi ndio maana wanafanya mambo ya ajabu ambayo yanaweza kuharibu soko na yanaweza pia kukimbiza wanunuzi tunaomba serikali ichukue hatua ili kukomesha tatizo hilo ambalo litakapofumbiwa mambo linaweza kuharibu sifa ya bidhaa hii” alisema Mtondo

Comments

Popular posts from this blog

Wananchi wajenga wodi baada ya kuchoshwa na kujifungulia sakafuni

Sita wapotea katika mazingira tatanishi wilayani Wete

Jaji Mkuu Zanzibar awashukia mahakimu wanaonyanyasa watuhumiwa